Aliyekuwa mchezaji maarufu wa kriketi na kisha kuamua kuwa mwanasiasa Imran Khan, ambaye kampeni yake yenye tumaini kubwa la kupata “Pakistani Mpya” imeshavuta makundi makubwa ya vijana pamoja na wapiga kura wa mijini kwenye mikutano yake katika harakati za kuelekea kwenye uchaguzi mkuu , alivunjika vifupa vitatu vya uti wa mgongo pamoja na mbavu baada ya kuanguka kutoka kwenye winchi iliyokuwa katika kimo cha futi 15 mda mfupi kabla ya kuhutubia.
Khan, aliyekuwa katika mkutano katika jiji la Lahore, alikimbizwa haraka kwenye Hospitali ya Kumbukumbu ya Shaukat Khanum. Ndani ya masaa machache ya kulazwa hospitalini, alipata tena fahamu na kuweza kutoa hotuba ya kisiasa yenye mashiko kwa waandishi wa habari waliokuwa pembeni mwa kitanda chake.
Kwa kuzingatia uchaguzi huu ulio na ushindani mkubwa unaotarajiwa kufanyika Mei 11, 2013, siku chache zijazo, kuanguka ghafla kwa Khan kunatokea wakati wa harakati za mwisho za kampeni. Yeye ndiye anayekiongoza chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI), mwanasiasa mgeni ambaye anaweza kuwa mgombea shupavu atakayewawakilisha watu kwenye chaguzi za hivi karibuni.
Lakini, jambo kubwa kabisa ni kuwa, tukio hili linaonesha ishara ya kuwepo kwa hali ya umoja pamoja na kuwepo kwa mpasuko hatari wa kisiasa uliotapakaa nchini kote kwani washindani, wakosoaji na wapinzani wanaweka tofauti zao kando na kumtakia Khan siha njema.
Habari hii kwa haraka kabisa ilibadilisha vichwa vya habari vingine kwenye vituo vya televisheni na pia mitandao mingi ya kijamii ghafla ilihanikizwa na habari hii. Watu mbalimbali kuanzia washirika wake wa kisiasa, washindani wake wakubwa Nawaz Sharif na Shahbaz Sharif hadi watu maarufu duniani kama vile Brian Lara walimwombea Imran Khan kupona haraka.
Mchezaji wa kriketi wa kutoka Indies ya Magharibi, Brian Lara (@BrianLara) alitwiti katika ukurasa wake mnamo tarehere 8 May, 2013:
@BrianLara: Imran Khan aliumia wakati wa mkutano kwa kuanguka kutoka jukwaani… balaa limemuepuka, Asante mungu! Upone kwa haraka ndugu uliye muhimu. Endelea kukipigania kile unachokiamini.
Kiongozi wa Pakistan Muslim League Nawaz (PML-N), Shahbaz Sharif aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook:
Si muda mrefu nimetoka hospitalini kumjulia hali Imran Khan na kufikisha salamu za kumtakia siha njema kutoka kwa Mian Nawaz Sharif…Alhumdulillah yeye hajambo na anaendelea vizuri mashaaAllah… tunamwombea yeye na familia yake!!!
Maryam Nawaz Sharif (@MaryamNSharif), mtoto wa kike wa kiongozi wa chama cha PML-N, Nawaz Sharif, pia alitoa hisia zake:
@MaryamNSharif: Alipata bahati mbaya wakati kampeni zikiendelea. Tunamuombea na kumtakia kila lenye kheri Imran Khan Sahib apone haraka; awe na siha njema kabisa.
Dr. Tahirul-Qadri (@TahirulQadri), ambaye siku za hivi karibuni aliongoza kundi kubwa la watu kukipinga Chama cha Watu wa Pakistan (PPP) chama cha serikali inayomaliza muda wake, alisema:
@TahirulQadri: huruma ya moyo wangu ni kwa mwenyekiti wa PTI, ndugu Imran Khan kwa kujeruhiwa. Ninamuombea awe na siha njema.
Rehman Malik (@SenRehmanMalik), aliyekuwa Waziri wa mambo ya ndani katika serikali inayoondoka madarakani ya chama cha Watu wa Pakistan (PPP), alitwiti:
@SenRehmanMalik: Ninamuombea Imran Khan apone haraka. Mwenyezi Mungu amjalie Baraka za kupona haraka.
Huko Punjab, chama cha Khan kinakabiliana na hali ngumu ya ushindani wa kisiasa dhidi ya chama cha Pakistan Muslim League (PML-N). pamoja na hali hii, kiongozi wa PML-N, Nawaz Sharif, alionesha kuguswa kwake na tukio hili na hivyo kuamua kusitisha kampeni za chama chake kwa siku moja kama namna ya kuonesha hali ya umoja kati yake na Khan.
Wengi wameeendelea kusema kuwa, kwa kuanguka kwake, Khan ameliunganisha tena taifa. Hammad Siddiqui (@hammads) aliandika na pia kudokeza kuwa, wanasiasa wa Pakistan wameerevuka kisiasa:
@hammads: Altaf Bhai ndiye aliyekuwa wa kwanza kusitisha hotuba yake na kumuombea Imran Khan – akifuatiwa na NS, hii inaonesha kupevuka kisiasa #
UpatenafuuharakaIK
Tukio hili pia limechochea idadi kubwa ya watu kukihurumia na kukiunga mkono chama cha siasa cha Khan, huku wengi wakitabiri kuwa, hali hii inaweza kuwa kuwa msaada mkubwa kwa chama cha Khan. Hassan Belal Zaidi (@mightyobvious_), mshauri wa vyombo vya habari,” Anguka Kutoa baraka” za Kura za watu wa Pakistan . katika makala hii, Zaidi aliandika:
Ukweli ni kuwa, Imran anaweza kuibuka mshindi katika chaguzi hizi. Ninaweza kunusa harufu ya ushindi maili chache hivi kwa mcheza kriketi huyu. Unaweza usiwe ushindi wa kishindo, inawezekana usiwe ushindi wa moja kwa moja, lakini kwa chama kipya, bila mashaka yoyote, utakuwa ni ushindi mkubwa. Ninatumai kuwa, kugongwa huku kichwani, utakuwa ni wito wa kuamshwa ambao watu wengi katika nchi yetu wanauhitaji. Siungi mkono chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaaf, na wala sitawapigia kura yangu. Lakini nakitakia chama chao na kiongozi wao mafanikio mema.
Wakati, watu wengi walimkosoa Imran Khan kuwa ameegemea siasa za mrengo wa kulia, kuanguka kwa bahati mbaya, kumeonesha tena uthibitisho kuwa taifa limeamshwa tena kisiasa na hususani kwa vijana. Na yote yakishasemwa na yakaisha, muhamasisho wa aina hii ni mabadiliko yanayohitajika sana kwenye demokrasia inayokua.
1 maoni