Global Voices inayapitia kwa haraka maandamano ya Siku ya Wafanyakazi Mei Mosi kwenye nchi za Cambodia, Filipino, Indonesia na Singapore. Mikutano, ambayo iliandaliwa kudai haki za wafanyakazi na makundi mengine ya utetezi, yalifanyika kwa amani katika bara lote la Asia ya Kusini Mshariki.
Nchini Cambodia, zaidi ya wafanyakazi 6,000 wa kiwanda cha nguo waliungwa mkono na wanafunzi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, na wakazi masikini wa mijini katika Jiji la Phnom Penh ambao wote kwa pamoja waliandamana kutokea Viwanja vya Freedom Park kuelekea kwenye Bunge la nchi hiyo kutoa wito wa kuboreshewa maslahi yao pamoja na mazingira bora zaidi ya kazi.
Katika video hii iliyowekwa na Kituo cha Jamii cha Elimu ya Sheria, muhutasari wa madai makubwa na hali ya wafanyakazi wa Cambodia ulikuwa:
Nchini Indonesia, maelfu ya wafanyakazi waliandamana mbele ya Ikulu ya nchi hiyo jijini Jarkata kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi. Baadhi ya madai yao, yalikuwa “kuongezwa kwa kima cha chini cha mshahara, bima ya afya na usalama kwa wafanyakazi, pamoja na kukataa misaada ya nje.”
Nchini Ufilipino, kikundi cha wafanyakazi kiitwacho Kilusang Mayo Uno kilikatishwa tamaa na sera za kazi zinazotekelezwa na serikali:
TUnaadhimisha mwaka wa 127 wa Siku ya Wafanyakazi Kimataifa na mwaka 110 wa maadhimisho hayo nchini Ufilipino kwa maandamano ya kitaifa kupinga utawala usiojali maslahi ya mfanayakazi na unaoshabikia ubepari wa Rais Noynoy Aquino.
Aquino ameyakataa madai ya wafanyakazi ya kupandisha mishahara yao, kuachana na mfumo wa ajira za mkataba na kusimamishwa kwa ukandamizaji unaofanywa na vyama vya wafanyakazi. Amejitetea kwa kutengeneza mfumo wa kuwanufaisha wafanyakazi pamoja na juhudi za serikali kuzalisha ajira.
Dondoo za matukio ya Mei Mosi jijini Manila zilikusanywa katika video hii iliyowekwa mtandaoni na EJ Mijares:
Nchini Singapore. Gilbert Goh wa tovuti ya transitioning,org aliandika kuhusu maandamano hayo ya kihistoria ya wafanyakazi nchini Singapore:
Tumejua kuwa nasi pia tunatengeneza sehemu nyingine ya historia nchini Singapore kwa kuwa haikuwa kutokea mtu akahamasisha tukio la siku ya wafanyakazi kutokea chini kabisa -haijawahi kutokea na tunajisikia fahari kufanya hivyo kwa mara ya kwanza!
Kwa sasa tunaweza hata kupanga kufanya maandamano ya wafanyakazi wakati wa Mei Mosi kuanzia sasa -kama inavyofanyika katika nchi nyinginezo kwa miongo sasa.
Tukio hili ni kupinga tukio la mwezi Februari lililowakusanya maelfu ya wa-Singapore waliokuwa wanapinga pendekezo la serikali kuhusu sera ya mpya ya idadi ya watu. Katika video hii, wa-Singapore wanaeleza sababu zao za kuandaaa na kuunga mkono tukio hilo.