Wanachama wa kikundi cha Kiislamu nchini Bangladesh Hifazat-e Islam, waliwashambulia waandishi habari wanawake wakati walipokuwa wakifanya matembezi ya umbali mrefu katika mji mkuu Dhaka kushinikiza sheria kali za kiislam , ikiwa ni pamoja na kuzuia watu wa jinsia tofauti kuchanganyikana pamoja na kupinga adhabu ya “wanablogu waliodaiwa kuonesha kutoamini uwepo wa Mungu na kukashifu dini”.
Kikundi hicho cha Kiislam cha Hefazot kilitangaza madai yao 13 wakati walipoandamana mnamo tarehe 6 Aprili, 2013 huko Dhaka, maandamano yaliyokuwa yanashinikiza adhabu kali kwa vitendo vya kukashifu dini, kuifanya elimu ya dini ya Kiislam kuwa ya lazima kwa kila mtu, na kusitishwa kwa “vitendo vyote vya utamaduni usiokubalika kama vile kujipamba kupita kiasi, kuvaa kikahaba, tabia mbovu, utamaduni wa kuchangamana kwa jinsia, kuwasha mishumaa kwa kisingizio cha uhuru binafsi wa mtu na uhuru wa kuongea.”
Siku ya matembezi hayo ya umbali mrefu, kikundi hicho cha Kiislam cha Hifazat-e sio tu kuwa kiliwazuia wanawake wasishiriki tukio hilo, lakini pia waliwadhalilisha kimwili na kwa maneno Baadhi ya waandishi wa habari wanawake walipokuwa wakitekeleza kazi zao wakati tukio lile likiendelea. Wanaharakati kadhaa wa Hifazat walimkimbiza na kumdhalilisha kimwili mwandishi wa taarifa za habari wa Televisheni ya Ekushey ajulikanaye kwa jina la Nadia Sharmin huko Bijoynagar, katika eneo la mkutanao huo, walimvamia mwandishi Arafat Ara wa Duru za Kiuchumi huko Paltan, akiwa karibu na eneo hilo akielekea ofisini kwake.
Sharmin alivurumishiwa maneno ya kashfa na kutupiwa chupa za maji na alitupwa chini na kisha kupigwa. Alipelekwa hospitali kwa ajili ya kupata matibabu na kuruhusiwa baada ya siku tatu .
Kesi zilifunguliwa dhidi ya watu 60. video hii ilipakiwa katika mtandao wa YouTube naProfessorZiauddin inamwoonesha Sharmin akishambuliwa na genge la Hifazat:
Mama mmoja mzee mmoja aliyekuwa akiokota chupa za maji katika eneo la kushanyiko hilo alitimuliwa mbali kwa kisingizio kuwa “siyo sehemu kwa ajili ya wanawake”
Hata hivyo, wakati maandamano ya waandishi wa habari yakiendelea nchi nzima, yaliyohimiza kususia habari pamoja na kutorusha matangazo ya habari za waislam, wawakilishi wa chama cha Hifazat walitoa tamko kwamba, kundi hilo lilijutia shambulizi hilo , kwa kusema “watu waovu ndio waliofanya mashambulizi hayo dhidi ya waandishi wa habari”.