Mpiga picha wa Kireno Eduardo Leal ameweka mkusanyiko wa picha mtandaoni ambao unakusudia “kupaza sauti za wafuasi wa pande zote, yaani wafuasi wa [Hugo] Chávez na wale wa [Henrique Capriles].” Katika ‘Sura na Sauti za Uchaguzi’, Eduardo anavuta hisia na mawazo ya watu wa Venezuela anapowapa fursa ya kueleza ni mgombea yupi watamchagua katika uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili, Oktoba 7, 2012.
Anafungua utangulizi wa mkusanyiko wa picha hizo za mtandaoni kwa maelezo mafupi ya siku 14 za mwisho za serikali ya Rais Hugo Chávez:
Akiwa madarakani, serikali mpya ya kijamaa inabadilisha (ilibadilisha) uso wa nchi ambayo mwanzoni ilifahamika zaidi kama sehemu ya kihistoria nzuri na sehemu alipozaliwa mpigania uhuru wa Latini Amerika, Simón Bolivar.
Mabadiliko ya kijamii yalianzishwa, yaliyowasaidia watu masikini kuimarisha hali zao za kimaisha na mipango ya shule. Sauti za wale ambao hawakuwahi kuipata fursa hii ziliwezeshwa kusikika kwa mara ya kwanza.
Eduardo anaendelea kueleza kuwa, kwa miaka mingi,Chávez aliongoza bila kuwa na upinzani wa maana. Upinzani huu “mara nyingi uliundwa kwa tabaka la matajiri na wasomi ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakila matunda ya kuishi katika nchi yenye hazina kubwa ya mafuta” anasema. Lakini pia, Eduardo anaonyesha kuwa, kwa miaka mingi, upinzani unaolekezwa kwa Chávez umeongezeka kadiri matatizo yanapoendelea kuwa dhahiri.
Machafuko katika mitaa yamefikia kiwango ambacho hayakuwahi kushuhudiwa, yakiliweka jiji la Caracas katika nafasi ya juu kabisa kwa kuwa miongoni mwa majiji hatari kabisa duniani. Upungufu wa nishati ya umeme na chakula, ongezeko la bei za bidhaa na hotuba kali za Rais zinaanza kutengeneza uelekeo mpya na fursa nzuri kwa upinzani.
Eduardo anaendelea kuujadili mgawanjiko ulioko hivi sasa miongoni mwa jamii ya Venezuela:
Wafuasi wa Chávez, wajulikanao kama Chavistas, kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, wale wa upinzani, sio tu unaundwa watu wa tabaka la kati na lile la juu linalojumuisha matajiri na wasomi kama ilivyokuwa awali, bali pia walalahoi wanaodhani nchi hiyo inahitaji mabadiliko.
Anachukulia mfano wa Henrique Capriles, ambaye ni mpinzani wa Chávez, kuwa ni sura ya “kukua kwa upinzani” na ambaye kwa mara ya kwanza anaweza kumpa changamoto ya kweli kweli Rais Hugo Chávez.”
Kwa mradi huu, Eduardo anataka “kutengeneza picha ya uelewa sawia juu ya kile ambacho watu wa Venezuela wanafikiri kuhusu mabadiliko na matuamaini yao kwa nchi yao.
Tembelea mkusanyiko wa picha zake mtandaoni na ujionee na kujisomea zaidi kuhusu ‘sura na sauti’ nyingine nyingi zaidi za Venezuela.
Unaweza pia kuendelea kumfuatilia kazi za Eduardo kupitia mtandao wa Twita (@Eduardoleal80), Facebook, na Tumblr.