Guatemala: Waandamanaji Wazawa 7 Wauawa Totonicapán

Makala hii ni sehemu ya makala zetu maalumu kuhusiana haki za wazawa .

Raia wasiopungua 7 wameuawa, takribani watu 32 wamejeruhiwa na 35 walidhuriwa na sumu mnamo tarehe 4, Oktoba, 2012 wakati majeshi ya muungano yalipotumia nguvu kuwatawanya waandamanaji kutoka katika njia panda maarufu inayoeleka Quetzaltenango, jiji la Guatemala City, Huehuetenango na Totonicapán.

Waandamanaji walifunga barabara kupinga ongezeko la bei ya nishati ya umeme katika eneo lao. Pia, wanahitaji majadiliano na serikali ili kujadili pingamizi lao kuhusiana na mabadiliko ya elimu pamoja na ya katiba yaliyopendekezwa na Rais Otto Pérez Molina.

Waandamanaji walikuwa wawakilishi wa jamii za wazawa kutokaTotonicapan, kwa upekee kabisa, wazawa wengi ambao ni asilimia tisini(90%) ni wanajamii kutoka katika nyanda za juu za Guatemala.

Wakati maandamano yakiwa yanafanana katika eneo hilo, idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa si ya kawaida kabisa. Kuna ushahidi kuwa wanachama wa jeshi la Guatemala walibeba bunduki, pamoja na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani hakukukubaliana na taarifa hii akisema kuwa wakulima waliuana wenyewe kwa wenyewe kama Mario Rodríguez anavyoelezea katika makala kwenye blogu yake “ Matamko Yenye Ushawishi binafsi” [es].

Mkoa wa Totonicapán. Picha na Sandra Sebastian kutoka plazapublica.com.gt chini ya Creative Commons Attribution kwa Ruhusa isiyo ya Kibiashara.

Totonicapán ni moja ya maeneo ya nchi yaliyopangiliwa vizuri na ambayo ni nadra sana kuwa na machafuko [es], pamoja na kugubikwa na umasikini uliopitiliza kiasi cha kuwa na watu wenye 82.2% [es] utapia mlo. Wakiwa ni wachapakazi wazuri na jamii ya wanamazingira, watu wa Totonicapán wanajulikana kwa utunzaji wa misitu na vyazo vyao vya maji, kama inavyofafanuliwa katika mtandao wa Masalio ya Kitamaduni (Cultural Survival):

Misitu imekuwa ikihifadhiwa kwa ajili ya vizazi, shukrani kwa juhudi za watu walioishi kwa amani na ulimwengu uwazungukao, hali iliyochangiwa na maarifa ya mababu zao ya umilikaji wa rasilimali pamoja na ushiriki hai wa kila jamii.

Kwa hali hii ya kuthamini na usimamizi, unahitaji jamii iliyo na mshikamano na yenye viongozi wawajibikaji wanaotafuta maslahi ya umma. Totonicapán ni miongoni mwa maeneo machache ambayo mamlaka za wazawa zina nguvu, zilizogawanywa katika majimbo 48 yanayoongozwa na Mameya pamoja na Rais ambaye anafanya kazi kama mpatanishi endapo kutatokea migogoro na pia kama mzungumzaji mkuu endapo kutakuwa na majadiliano ya nje ya wanajamii.

Mwaka 2011, meya wa kwanza katika historia, mwanamke mmoja ambaye ni mwanafunzi wa sheria, María del Carmen Tacam, alichaguliwa kuwa rais wa jimbo la Totonicapán. Katika mahojiano [es], mwanamke huyu alieleza kuwa anafuata maelekezo yaliyofikiwa na mamlaka zote 48 za mamlaka za vijiji.

Taarifa iliyotolewa na Voces Mayas [es], María del Carmen alieleza kuwa, wakati akisihi kuacha kutumia nguvu, jamii za watu wazawa walifunga njia panda ya Cuatro Caminos kufuatia serikali na mashirika kushindwa kusikiliza madai yao ya msingi. Pia alitanabaisha kuwa, hospitali ya mtaa ilizidiwa na wagonjwa kutokana na idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa.

Katika matamko yake, María del Carmen aliwafafanulia [es] waandishi wa habari kuwa, jamii ya watu wa Totonicapán walihitaji mdahalo kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mambo muhimu matatu:

  1. marekebisho ya katiba yaliyopendekezwa na Rais ambayo wananchi hawajakubaliana nayo.
  2. Mabadiliko ya elimu , kama wanavyopinga marekebisho ya vigezo vya mtu kuwa mwalimu katika shule fulani.
  3. kuongezeka kwa gharama za nishati ya umeme kwa kuwa kampuni haikuzingatia malengo iliyojiwekea.

Wanajamii wanataka majadiliano yawe ya wazi na wanasubiri majibu ya serekali ya Pérez Molina. Wakati wa serikali iliyotangulia, majadiliano kati ya serikali na wanajamii yalipatanishwa na Ombudsman kama hati [es] zinavyoonesha, lakini kwa kipindi hiki, alizuiwa kufanya hivyo.

María del Carmen Tacám na ishara ya uongozi. Picha na Sandra Sebastian kutoka plazapublica.com.gt chini ya Creative Commons Attribution Ruhusa isiyo ya Kibiashara.

Kwa kuongezea zaidi, mapema mwezi Machi, 2012, watu tofauti waliweka bayana matakwa yao kuhusiana na ongezeko la haraka la idadi na kazi za kijeshi nchini Guatemala na uwepo wa kile kijulikanacho kama “miradi mikubwa” (“mega projects”) kama vile mgodi wa Goldcorp. Cascadia solidaria anaeleza kuhusiana na kuongezeka kwa matukio mengi ya kijeshi dhidi ya raia:

Mkakati wa kufunga barabara unaotumiwa na wazawa na jumuiya za campesino kama namna ya hamasa za kisiasa na kama namna ya kuhamasisha utatuzi wa changamoto zao unapingwa vikali na taifa pamoja na mkundi yenye ushawishi mkubwa wa kiuchumi haswa haswa kundi la watu wafanyabiashara la CACIF*, ambalo limeshahamasisha kuwashikilia watu kama namna ya kukiuka haki ya watu kuwa na uhuru wa kutembea. Serikali ya Pérez Molina siku za hivi karibuni ilitumia nguvu kuwatawanya makundi ya wanafunzi, walimu na wazazi wanaoandamana kupinga mabadiliko ya elimu yaliyo ya kibaguzi; kama mauaji ya sasa yatathibitishwa kuwa yametokana na matumizi ya nguvu ya kijeshi, itakuwa ni kiashirio cha kwanza cha serikali kandamizi iliyo ya kiuaji dhidi ya raia wanaoandamana chini ya uangalizi waMano Dura. Wakati viongozi wa kijamii wanashinikiza uchunguzi kufuatia mauaji haya, kama uongozi unafuata mkakati ulioanzishwa kufuatia migogoro ya kijamii na maandamano ya Barillas, Huehuetenango, mbinu za kushikilia watu kama vile kuwaweka kizuizini viongozi wa maandamano au serekali kutoa tamko zingeweza kutumika.

Katika tamko rasmi la serikali, Rais ambaye ndiye mwenye mamlaka ya mwisho na aliye amiri jeshi mkuu wa jeshi la Guatemala alitanabaisha kuwa ameshatoa amri ya kufanyika kwa uchunguzi [es] kuhusiana na uonevu na mauaji toka Octoba 4.

Wakati huohuo, wanajamii wanasubiria majadiliano pamoja na majibu ya kero zao.

Makala hii ni sehemu ya makala zetu maalumu kuhusiana na haki za wazawa .

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.