Kenya: Wito wa Mshikamano Baada ya Mashambulizi ya Kigaidi

Siku chache tu kabla ya ufunguzi wa GV2012 mjini nairobi, Kenya ilishuhudia milipuko na utekaji nyara huko Mombasa na katika mji wa Garissa. Mlipuko ulitokea katika ukumbi wa starehe mnano Juni 24 na kuwauwa watu watatu, siku moja baada ya ubalozi wa marekani kuionya mamlaka ya Kenya kuhusu uwezekano wa mashambulizi jijini humo. Umati huo ulikuwa umekusanyika katika baa kutazama robo fainali ya Kombe la Ulaya kati ya Uingereza na Italia.

Beegeale anamnukuu mtu aliyeshuhudia tukio hilo:

 

“Nilikuwa ndio tu nimewasili na nilikuwa nakunywa kinywaji nikisubiri mechi ya mpira ianze, ndipo nikasikia mlipuko, mlipuko mwingine tena, na mwingine. Nililala chini, kisha nikaona gari ikiondoka kwa kasi na miili imetawanyika kila mahali” alisema Muthoni.

Mnamo Julai 1, Huko Garissa nchini Kenya, washambulizi waliokuwa wamefunika nyuso zao, waliwaua watu kumi na saba na kuwajeruhi arobaini na watano kwa risasi na mabomu kwa makanisa mawili. Jiji hili linatumiwa na wanajeshi wa Kenya kama ngome ya oparesheni dhidi ya wanamgambo wa al-Qaida huko u-Somali.

 

 

Katika posti iliyoandaliwa na wanahabari wa Sahara, James Macharia alidondoa

 

Ijapokuwa wa-Kenya wengi ni wakristo, huko Garissa waislamu ndio wengi. Mji huo una jumla ya watu 150,000, soko la kuuzia ngamia, punda, mbuzi na ngombe, na wakazi wake wengi ni wa-Somali.

Mji wa Garissa katika Jimbo la kaskazini mashariki nchini Kenya. Picha imetolwa chini ya Creative Commons (CC BY-SA 3.0) by Wikipedia author Chking2.

 

Francis Njuguna aliandika kwenye CatholicPhilly:

 

Mashambulizi hayo yaliyotokea muda ule ule kwenye kanisa la Our Lady of Consolation na katika kanisa la Protestant Africa Inland Church katika mji wa kaskazini wa Garissa yanakuwa matukio ya hivi karibuni zaidi katika matukio kadhaa tangu wanajeshi wa Kenya walipopelekwa nchini Somalia mwezi Oktoba kuwaangamiza wapiganaji wa al-Shaabab.

 

Katika shambulizi lingine la kinyama katika kambi ya wakimbizi Dadaab, wafanyakazi wanne wa shirika la misaada la kigeni kutoka Canada, Norway, Ufilipino na Pakistani walikamatwa na dereva wao mkenya kuuawa na watu wanaohisiwa kuwa ni al-shabaab. Ushirikiano kati ya jeshi la Somalia na Kenya ulisaidia katika kuwanusuru baada ya siku tatu tangu watekwe nyara.

 

Maandamano na miitikio ya mtandaoni imekuwa ya ghadhabu sana, ikiyalaani mashambulizi hayo, pamoja na kutoa wito wa mshikamano miongoni mwa raia wa mtandaoni na kupanga mikakati ya kuzuia mashambulizi ya baadaye. Makala katika tovuti ya nation.co.ke gazeti kuu la Kenya iliibua maoni tofauti kutoka kwa raia wa mtandaoni.

 

Ahmed Mohamed aliandika:

 

Hii ni siku ya huzuni kwa Kenya. Hawa waoga wanataka kuanzisha vita vya kiraia; wamekwisha angamiza nchi yao kwa njia hii. Tusiwaruhusu wazue chuki baina yetu. Waislamu na wakristo wamekuwa na mahusiano ya karibu kwa karne na wataishi hivyo daima. Kitendo hicho cha kijinga hakitaathiri nchi yetu.

Kwa Michelline Ntara serikali ya kenya isaidie kambi za wakimbizi zilizoko kenya:

 

….Hata hivyo, Kenya yafaa itathmini upya kanuni zake za ukarimu. KDF (Jeshi la Kenya) limesaidia kurejesha amani katika sehemu nyingi ndani ya Somalia. Kambi za wakimbizi katika mpaka wa Kenya na Somalia yafaa ufungwe sasa na hao watu wasaidiwe kurudi nchini kwao. Pengine hawa washambuliaji wanafanya mashambulizi haya ya kijinga kutokea kwenye kambi hizo kisha wanarudi baadaye. Hata vikosi vya usalama vikijaribu iwezekanavyo kuwakamata hawa majambazi, itakuwa vigumu kupigana na adui akiwa katikati yao.

 

Triple A aliandika:

 

Wapenzi taifa la Kenya, ni wakati sasa tuanze kuyaita mashambulizi haya kwa majina yanayostahili… Mashambulizi ya kigaidi. Kwa kuyataja kama mashambulizi ya kanisa yaweza maanisha chochote, ilhali twajua kuna chembechembe za msimamo mkali wa Al-shaabab nyuma ya mashambulio hay. Wakenya wanalipia gharama kubwa kwa miaka mingi ya ujinga wao. Sote tulijua kwamba kulikuwa na chembechembe za misimamo ya kigaidi nchini kwetu lakini tukachagua kukaa kimya.. lakini hatuwezi endelea na mbinu hii dhaifu ya mbuni. Hatua ya kwanza ni kuyaita mashambulizi haya kwa vile yalivyo, na ndivyo yalivyo, Mashambulizi ya kigaidi.

 

Msomaji mwingine Mohamed Abdi aliuliza:

 

Saa nne na dakika ishirini asubuhi? Ilikuwa mchana kabisa. Kuna jambo lisiloeleweka sawia hapa, walikuwa wapi wanausalama, jeshi, polisi na uongozi wake? Itakuwaje washambulizi wawili au watatu kutekeleza shambulizi hili saa nne asubuhi bila kukamatwa wakati inaeleweka Garissa ina maelfu ya walinda usalama? Ingekuwa rahisi kuzingira eneo hilo na kuwakamata waliohusika. Kwa mara nyingine watu wetu wa usalama wamewaangusha wakenya wasio na hatia wanaowalipa kwa jasho la kodi zao. Ni jambo la aibu sana!

 

Mazzaroth Darkman aliandika:

 

NSIS (Idara ya Usalama wa Taifa) ni lazima iwaambie wakenya ni akina nani wanaorusha makombora katika makanisa na mikutano ya kidini, kama ni mambo ya siasa za kenya tunataka kujua. Kama ni Al shaabab jeshi lazima liamke, liwatumie mashushu wake katika kona hizo za giza kuanzia Kismayu mpaka Eastleigh na kusitisha hali hii kirahisi… tusijifanye wapole sana. Hii haikuwa kampeni ya kivita ya kawaida.

AZISE ya ki-Islamu ilijitolea kusaidia kulinda makanisa:

 

Aidha, ni jukumu letu kama waislamu kuhifadhi na kulinda maisha ya wote wasio na hatia, hii ikiwa ni pamoja walioko makanisani. Twawasihi ndugu zetu waeneze ujumbe wetu na kuhimiza upinzani baina yetu wa-Islamu wataowakamata wale wanaodai kuwa waislamu lakini kiukweli ni wafanyakazi tu wa shetani, na ndio wanaoendeleza vitendo hivi.

 

Habari hiyo ilitolewa kwa blogu My Joy Online, nakupokea maoni kutoka kwa John Mensah, aliyesema:

 

Tuzungumzie kuhusu kuishi pamoja kwa utulivu na amani. Yafaa iwe mfano kwa kila mtu. Hata lengo tu lafaa kusifiwa.

 

Hata hivyo, wanaoendeleza vitendo hivi vya kigaidi hawaonekani kutilia maanani miitikio kama hii:

 

Polisi wa kenya mnamo alhamisi iliripotiwa wamemkamata mtu mmoja akiwa na mabomu mawili alipokuwa anajaribu kupenya kuingia kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Kilimo huko Nakuru, dakika chache kabla ya Rais wa Kenya Mwai Kibaki kuwasili kwenye eneo hilo.

 

Kwa sasa, uchunguzi unaendelea na watu themanini na tatu wameshikiliwa kufuatia zoezi la kuwasaka lililozinduliwa baada ya mashambulizi hayo mawili jumapili katika makanisa ya mji wa Garrissa.

3 maoni

Sitisha majibu

jiunge na Mazungumzo -> Adiie9

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.