Je, Sifa ya ‘Kisiwa cha Amani’ Tanzania Imeanza Kutoweka?

Tanzania imeshuhudia matukio kadhaa ya kusikitisha tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, yakiwemo kadhaa yaliyosababisha vurugu na vifo. Mwanablogu Dunia Duara ametengeneza orodha (haijakamilika bado) ya matukio yaliyochochewa na migogoro mbalimbali, ambayo kwa siku za karibuni yamesababisha matatizo makubwa nchini Tanzania:

2011 Januari: CHADEMA [chama kikuu cha upinzani] chaongoza maandamano jijini Arusha na kuingia kwenye mgogoro na polisi.
2011 Februari: Milipuko ya mabomu huko Gongo La Mboto
2011 Julai: [machinga] wapambana na polisi jijini Mwanza
2011 Septemba: Meli ya MV Spicelander yazama ikiwa kati ya sinks Zanzibari na Pemba
2011 Desemba: Jiji la Dar es Salaam lakumbwa na gharika
2012 Februari: Polisi yaua watu mjini Songea
2012 Aprili: Masuala ya ardhi yajitokeza katika uchaguzi mdogo Arumeru
2012 Mei: Maandamano mjini Zanzibari yakihusishwa na kikundi cha kidini kinachodai kujitenga kiitwacho UAMSHO
2012 Juni: Madaktari wagoma (ni kama walianza mwezi Februari na kuendelea) na kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari Dk Ulimboka.
2012 Julai: Boti ikiwa njiani kuelekea Zanzibar kutokea Dar es Salaam yazama.
2012 Julai: Vurugu mjini Zanzibar zikihusishwa na UAMSHO, na maombolezo kufuatia vifo vilivyoisababishwa na ajali ya boti.

Police brutality in Tanzania. Photo source: wavuti.com, used with permission.

Ukatili na matumizi nguvu kupita kiasi yanayofanywa na Polisi nchini Tanzania. Picha: wavuti.com, imetumiwa kwa ruhusa.

Hivi karibuni, mnamo Septemba 2, 2012, mwandishi wa habari wa Tanzania Daudi Mwangosi aliawa kwa kile kinachodaiwa kuwa bomu la kutoa machozi katika kijiji cha Nyololo, Mufindi Kusini, Iringa mkoa ulioko Kusini mwa Tanzania. Gazeti la The Citizen lilikuwa kati ya magazeti ya kila siku yaliyoripoti tukio hilo la kusikitisha, likieleza namna polisi walivyotumia bomu la kutoa machozi kukitawanya kikundi cha wafuasi wa CHADEMA (chama cha upinzani):

Bw Mwangosi anakuwa mtu wa pili kuuawa katika migogoro inayolihusisha Jeshi la Polisi na chama cha upinzani katika kipindi kisichozidi wiki mbili. Awali, Agosti 27, kijana muuza magazeti Ally Zona aliuawa mjini Morogoro wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakijiandaa kufanya maandamano.

Picha za tukio hilo la kijiji cha Nyololo zilisambaa kwa kasi sana katika mitandao ya kijamii. Blogu ya Wavuti.com imetengeneza mkusanyiko mzuri (pamoja na picha iliyotumika hapo juu). [Tafadhali, unatahadharishwa kuwa baadhi ya picha zinatisha, zikionyesha mabaki ya mwandishi huyo ambaye alichanwa vipande vipande na bomu hilo la machozi.]

Tukio hili limepewa nafasi kubwa na magazeti mbalimbali, ya Kiswahili na Kiingereza pamoja na yale ya Kimataifa, yote yakiandika maoni mengi. Watumiaji wa mitandao ya kijamii wameonyesha hasira na mshangao kufuatia kile kinachoonekana kuwa mauaji yasiyoleta mantiki yoyote na kwa kweli mauaji yanayoonyesha ukatili. Watu wameonyesha kushangaa vyote viwili, mauaji na ukatili wa polisi.

Daraja blog alikuwa mwepesi kutengeneza orodha sahihi ya ‘vyanzo muhimu’, ikiwa ni pamoja na tamko la Baraza la Habari Tanzania na tamko la Baraza la Habari Duniani, lakini pia Daraja alifanya uchambuzi wa kina -akitaja bayana kwenye kichwa cha habari kwamba ‘mstari umevukwa’.

Kwanza, alianza na muhtasari wa kilichotokea:

Wanatuambia kwamba Mwangosi alikuwa Nyololo pamoja na waandishi wengine kuandika habari za CHADEMA kufungua ofisi kijijini hapo, kinyume na amri ya polisi kuzuia shughuli za kisiasa wakati huo wa zoezi la sensa. Palikuwa na idadi kubwa ya polisi katika kijiji hicho. Mwandishi mwingine, Godfrey Mushi wa gazeti la Nipashe, alikuwa ameshikiliwa na polisi, na ndipo Mwangosi alipokwenda kufahamu imekuwaje. Ndipo kundi la maafisa wa polisi lilipomgeukia Mwangosi, kwa kumpiga vibaya kwa dakika kadhaa.

Taarifa zinasema Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Michael Kamuhanda, alikuwa karibu katika gari lililoegeshwa, na alijulishwa kwamba mtu aliyekuwa anapigwa na polisi alikuwa ni mwandishi. Hata hivyo, hakuchukua hatua yoyote kuzuia ukatili huo, na dakika chache baadae bomu la kutoa machozi lililipuliwa kwa karibu mno kuelekea kwenye sehemu ya tumbo la Mwangosi. Mwangosi alipoteza maisha pale pale, na ofisa mmoja wa polisi alijeruhiwa.

Journalists demonstrate in Dar es Salaam on September 10 against the police violence which caused Daudi Mwangosi's death. Photo by Gaure Mdee, used by permission.

Waandishi wa Habari wakiandamana jijini Dar es Salaam tarehe 10 Septemba kupinga matumizi makubwa ya nguvu yaliyosababisha kifo cha Daudi Mwangosi. Picha ya Gaure Mdee, imetumiwa kwa ruhusa.

Daraja anaendelea:

Hakuna dalili kuwa Daud alikuwa anafanya chochote kisichostahili. Alikuwa pale kama mwandishi, akiwa na haki ya kisheria kuwa pale kuripoti shughuli za CHADEMA na mwitikio wa polisi. Hakuwa pale kama mfuasi wa CHADEMA kwenye mkutano ule, kwa hivyo hakuwa anavunja amri ya polisi kupiga marufuku shughuli zozote za kisiasa wakati wa zoezi la sensa. (Ingawa hata kama mfuasi wa CHADEMA angeuawa namna hii, bado vitendo hivyo vya polisi visingekuwa sahihi.)

Daraja anaibua maswali mazito:

Je, polisi waliohusika na mauaji haya watawjaibishwa? Na je, tukio hili lina madhara gani kwa vyombo vya habari?

Majibu hayapatikani kirahisi.

Wanahabari za Tanzania walionyesha maombolezo yao kwa mwenzao walioandamana jijini Dar es Salaam (na sehemu mbalimbali nchini Tanzania) tarehe 10 Septemba, kupinga matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na polisi hivi karibuni.

Sifa ya Tanzania kama nchi ya amani inaendelea kumomonyoka kwa kasi kufuatia matukio haya ya hivi karibuni.

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.