Mvua kubwa imesababisha mafuriko makubwa katika maeneo mengi ya Vitongoji vya jiji la Manila na mikoa ya jirani katika Kisiwa cha Luzon nchini Ufilipino. Eneo la katikati ya Manila, ambalo ndipo penye shughuli nyingi zaidi za mjini katika nchi hiyo hasa kwa kuwa linaundwa na miji 17 pamoja na manispaa mbalimbali, limeathiriwa vibaya. Tayari serikali imesitisha shughuli za shule, kazi katika ofisi za uma na hata zile za binafsi.
Picha zilizo hapa chini, zinazotoka hasa kwenye kurasa za Facebook na Twita, zinaonyesha kiwango cha mafuriko katika maeneo ya jiji na huenda hali itakuwa mbaya zaidi kwa sababu bado mvua inaendelea kunyesha hadi tunapoandika makala haya.
Serikali imetoa orodha ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko katika Vitongoji vya jiji la Manila. Orodha nyingine inaonyesha barabara ambazo bado zina mafuriko mengi. Mashirika ya habari pia yamekusanya orodha za vituo vya uokoaji na shughuli za uokoaji katika maeneo ya jiji.
Watumiaji wa mtandao wa Twita wanatumia alama ashiria #rescueph na #prayforthephilippines kufuatilia hali hiyo. Hapa chini kuna twiti ya kuwakumbusha waandishi wa habariambao wanaoripoti maafa yanayojitokeza:
@katray: Marafiki wa vyombo vya habari, tunathamini kazi mnayofanya. Ningetamani waandishi wa habari wawe wasioathiriwa na maji, lakini sivyo ilivyo, ninawatakia heri na salama. Jitunzeni Marafiki ;)
Carl Ramota anaonyesha kufedheheshwa na kuchelewa kwa serikali kuchukua hatua, hasa Rais:
Mpendwa serikali ya Aquino, ilikupasa kufanya mkutano na vyombo vya habari jana usiku au mapema leo asubuhi. Hatutaki kukuona wewe umevaa vazi la kuzuia mvua au koti katika chumba cha mkutano, ukizungumza juu ya mambo ambayo sisi tayari tunayajua au sasa yanaendelea. Panda vyombo vya majini na uzungukie ili kukagua maeneo yote yaliyoathiriwa na mafuriko. Nenda katika vituo vya uokoaji na saidia kusambaza misaada. Fanya kitu! Sio kukaa tu huko na kuzungumza! Vichwa havina budi kufanya kazi.
Carlo Ople anabainisha wajibu wa vyombo vya habari vya kisasa katika kueneza taarifa kuhusu mafuriko:
Haraka kama mafuriko yalivyoenea watu walianza kuchukua picha na kuziweka kwenye mitandao ya Facebook na Twita. Mtandao mmoja ulianza kushirikiana na mtandao mwingine, na kubadilishana huku kwa taarifa kuliendelea hadi picha hizo zikaenea sana. Kupitia picha hizo ilikuwa rahisi kuona jinsi hali halisi ilivyokuwa mbaya.
1 maoni