- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Mfumo wa Kipekee wa Kuwapa watoto Majina wa Nchini Myanmar (Burma).

Mada za Habari: Asia Mashariki, Myanmar (Burma), Lugha, Sanaa na Utamaduni, Uandishi wa Habari za Kiraia

Pale mtu wa Burma anaposema kuwa hana jina la ukoo [1], wageni huwa wanashangaa ni kwa nini. Myanmar inaweza kuwa ni miongoni mwa nchi chache duniani ambamo hadi asilimia 90 ya watu wake hawana majina ya ukoo. Watu wa familia moja wanaweza kuwa na majina yasiyofanana kabisa na idadi ya maneno kwa kila jina inaweza kuwa na utofauti mkubwa kabisa.

Mkazi mmoja wa Myanmar anaandika kuhusu utaratibu wao wa kuwapa watoto majina. Anasema:

Sisi wa-Myanmar, ni kama neno tu katika hadithi ziandikwazo kwa Kiingereza. Amini usiamini! Hatuna majina ya ukoo kabisa. Na hakuna nafasi nyingine baada ya sehemu ya jina la kwanza katika fomu yoyote itakayotakiwa kujazwa majina hapa Myanmar.

[2]


Muuza juisi itokanayo na miwa kutoka Myanmar. Picha kutoka ukurasa wa Flirck wa Michael Foley iliyotumika chini ya mpango wa CC wa haki miliki.

Na anaeleza [3] namna ambavyo watu wa Myanmar wanavyojaza fomu zinazohitaji majina yote, yaani jina la kwanza na la ukoo:

Lakini tunapojaza fomu kutoka kwenye mtandao wa intaneti, huwa hatuna njia mbadala zaidi ya kuweka majina ya ukoo kwa kuwa ni lazima kufanya hivyo. Sasa, huwa tunajaza nini? Kwa upande wangu, huwa ninajaza maneno mawili ya kwanza kutoka katika jina langu kama jina la kwanza na neno la mwisho kama jina la ukoo. Unafikiri hakuna mpangilio? Vizuri, labda ungependa kufahamu kuna maneno mangapi kwa kila jina? Kwa busara kabisa, jibu langu ni kuwa “inategemea”. Ndio, inategemea na namna wazazi walivyo wabunifu au inategemea na yule anayempatia mtoto jina.

Twobmad alizitaja [4] changamoto anazokabiliana nazo mtu pale anaposhughulikia majina ya watu wa Myanmar:

Huwa ninachanganyikiwa kabisa pale ninapolazimika kuandika majina yote matatu, yaani jina la kwanza, la kati na la mwisho. Hali hii pia hujitokeza pale ninapokuwa ugenini, yaani mbali na nchini mwangu, marafiki huwa wananiuliza ningependa waniite kwa jina gani. Hakika, wao pia, huwa wanachanganyikiwa. Kwa sababu kama wakiniita kwa jina kwanza jina, sio tu kuwa hawaniiti kama nilvyokuwa naitwa katika familia yangu, lakini pia hata kwa jamii yangu iliyotangulia. Wangeweza kuniita jina langu la kwanza, lakini ningeona kama maajabu kama ningekuwa naitwa kwa jina ambalo sikuwahi kulisikia kamwe.

Ba Kaung aliandika makala katika blogu [5] kuhusiana na namna ya utoaji wa majina kwa watu wa Myanmar ambapo katika maelezo yake, alihusisha pia na imani ya elimu ya nyota:

Miaka michache baadae, baada ya kushuhudia tamaduni mbalimbali duniani kote, niligundua kuwa utamaduni wa watu wa Burma wa kuwapa watoto majina ni wa kipekee kabisa kwani unajumuisha muunganiko wa kipekee wa tabia njema ya mtu huku jina likihusisha pia mahesabu ya elimu ya nyota ya mtu kwa siku ya wiki aliyozaliwa kwa kuzingatia kalenda ya mwaka itokanayo na mwezi wa wa-Barma.

Pia alizungumzia [5] hatma ya lugha ya wa-Myanmar ambayo ni muhimu kwao na ambayo wakati mwingine imekuwa ikiwachanganya wageni, kwa mfano, “U” (inayotamkwa Oo) katika “U Thant [6]“. Kwa kuongezea, watu wenye majina yenye neno moja tu, mara nyingi huwa wanapata ugumu wakati wa kuelezea jina la familia, kama ilivyo kwa neno la kwanza kama “U”, Ma”, “Daw” na kadhalika, ambayo siyo majina yao kiuhalisia:

Kuonesha heshima pia ni jambo muhimu sana katika kutaja majina ya watu wa Myanmar. Mtu anaweza kutambulishwa kwa jina lake kutanguliwa na maneno ya heshima kwa kutegemea na umri wake, aina ya uhusiano na jinsia. Itachukuliwa kuwa ni jambo lisilo la heshima kumuita mtu jina kama ilivyo katika utaratibu wa kawaida wa kuongea.Kutamka majina ya vijana na ya rika, majina yao hutanguliwa na “Ko” ambayo hutumika kutambulisha wanaume, “Ma” hutumika kutambulisha wanawake na ndio utaratibu rasmi.“Maung” inatumika kama namna ya kuwatambulisha wanaume katika mfumo rasmi. Majina ya watu wazima hutanguliwa na “U” or “Oo” ambayo hutumiwa kutambulisha wanaume katika mfumo rasmi. “Daw” hutangulizwa katika majina ya wanawake katika mfumo rasmi.

Kwa kuwa hakuna majina ya kifamilia kwa watu wa Myanmar, wanawake hawana ulazima wa kubadilisha majina yao pindi wanapoolewa. Dharana anaandika [7]:

Mradi wangu wa tatu umekuwa ni kujifunza namna ya kutamka kwa usahihi majina ya wenzangu. Majina ya watu wa Myanmar hutegemea na siku ya wiki mtu aliyozaliwa na huwa hayana kipengele chochote cha majina ya kifamilia. Hii inamaanisha kuwa, wanawake wataendelea kuwa na majina yao hata mara baada ya kuolewa- jambo ambalo wasichana wenzangu wananionea wivu

Kwa upande mwingine, baadhi ya makabila ya Myanmar, wale wenye asili ya India na wakristo wanafuata utaratibu wa kuwa na majina ya kifamilia. Lionslayer anaandika [8] kuwa watu wachache sana wa Myanmar wana majina ya ukoo:

Baadhi ya watu wanapenda kutumia majina ya baba zao kwa kutumia utaratibu wa kuwapa watoto majina kwa mfumo wa Kiingereza Aung San Suu Kyi [9] ni mtoto wa kike wa Aung San [10] na Hayma Nay Win [11] ni mtoto wa kike wa Nay Win [12]. Hata hivyo ni nadra sana kuona utaratibu wa namna hii. Watu wa Burma huwa wanawapa majina watoto wao wachanga kwa kuzingatia unajimu [13] kuliko kuwapa watoto majina kwa kuwa kuna fulani aliwahi kupewa jina hilo. Baadhi ya makabila ya Myanmar kuna majina ya kifamilia. Na baadhi ya Waislamu na Wakristo pia huwapatia watoto majina kwa kuzingatia majina ya baba zao na babu zao.

Alihitimisha kuwa, serikali ya Myanmar inapaswa kuweka utaratibu wa usajili kwa kuweka kumbukumbu za familia kwa kuwa ni vigumu kufuatilia chimbuko la familia ya mtu fulani:

Kuna madhara ya kutokuwa na majina ya familia. Ni vigumu sana kutafuta chimbuko la mtu kwa zaidi ya vizazi vitano. Sio tatizo kubwa sana kama Myanmar itakuwa na ofisi inayoratibu familia za watu wa Myanmar. Ni matumaini yangu kuwa serikali iataweka utaratibu huu pamoja na namna nzuri ya kupata taarifa hizi. Hata hivyo haijalishi kwa kuwa sio sisi tu katika ulimwengu tusio na majina ya kifamilia. Siku za hivi karibuni nilijifunza kuwa kuna baadhi ya makabila ya Asia ambayo pia hayana majina ya kifamilia.