- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Kocha wa Timu ya Taifa ya Zambia Atunukiwa Ukaazi wa Kudumu

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Zambia, Mahusiano ya Kimataifa, Michezo, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhamiaji na Uhamaji, Vichekesho

Zambia imewahi kuwa na makocha wengi wa kigeni wa timu yake ya taifa. Pengine aliyekuwa maarufu zaidi kati yao ni raia wa Kroatia Ante Buselic [1], ambaye aliifikisha nchi katika fainali za Kombe la Washindi barani Afrika za mwaka 1974, lakini Mfaransa, Herve Renard [2], aliyeiwezesha timu kushinda Kombe la Washindi barani Afrika la 2012 [3] amefutilia mbali umaarufu wa watangulizi wake wengine wote. Ili kutambua mafanikio yake hayo, Serikali ya Zambia hivi karibuni ilimtunuku ukaazi wa kudumu [4].

Akitangaza tunu hiyo ya hali ya uhamiaji wa Renard — utakaomfanya asiwe na haja ya kuomba upya kibali cha ukaazi — Waziri wa Michezo Chishimba Kambwili slisema [5]:

Kama anataka kuwa mkazi wa kudumu, Serikali ya Zambia iko tayari kumpa fursa hiyo, na ndiyo sababu tumeamua kumtunuku kwa ukaazi wa kudumu kama njia ya kuonyesha tunathamani mchango wake katika maendeleo ya soka ya nchi hii.

Herve Renard showing off a scarf in Zambian flag colours.

Herve Renard akionyesha skafu yenye rangi za bendera ya Taifa la Zambia. Picha imetumiwa kwa kibali kutoka tovuti ya UKZambians.

Katika moja ya tovuti za uandishi wa kiraia [6] suala la kumtunuku ukazi wa kudumu kocha ambaye wakati fulani aliitosa Zambia na kwenda zake Angola, kunaonekana kuwa na mrengo wa kisiasa zaidi. Suala la uraia wa nchi mbili bado lina mzozo kwa sababu Wazambia wengi wanaoishi nje ya nchi wanataka suala hilo liingizwe kwenye katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa, lakini hali ya Renard ya sasa kuhusu uraia wake ni kama vile imetia dosari mchakato huo.

Huku ikiwa bayana kabisa kwamba haelewi maana ya ukazi wa kudumu na uraia wa nchi mbili, mtumiaji canadian aliandika [7]:

Hivi, hawa wanasiasa huwa wanatazama vizuri rekodi kabla ya kutoa matamshi yao mbele ya vyombo vya habari? Huku ni kujichanganya hasa kuhusu kile ambacho Sata amekuwa akikisema kuhusu Uraia wa Nchi mbili [8]. Zambia inahitaji kipengele hiki kiingizwe kwa sababu manufaa yanazidi sana kile ambacho watu wasiojua yale wanayoyazungumzia. Ni zaidi sana kuliko kumwajiri kocha wa soka pale linapokuja suala la Wazambia waishio nje ya nchi na kiwango cha uwekezaji watakachokifanya katika nchi.

Msomaji anayejiita harold aliandika [7]:

Upendeleo wa aina hiyo bila kufuata utaratibu unatia mashaka. Renard alikuja hapa kwa kazi moja tu, nayo ni kuwa kocha, sawa sawa na ambavyo watu wengi tu wameshafanya, hebu fikiria ikiwa kila anayekuja Zambia anafanya vizuri sana, je, tutawachukua wote? Alinunuliwa gari lenye thamani ya kwacha milioni 350 [kama dola za Marekani 78,000], huku Zambia ikiwa kwenye lindi la umaskini, je, hivi ndivyo tunavyopaswa kumfanyia mtu mmoja? Tunajua kwamba serikali inamlipia kodi ya nyumba na gharama nyingine nyingi. Mara nyingine nashindwa kuelewa kwa nini tunaendelea kuwahusudu wazungu kuliko Wazambia wenzetu. Kusema ukweli, sisi vijana tumepoteza mwelekeo kabisa kuhusu yale tunayojifunza na kile kinachotokea ambacho ni kinyume cha sehemu yetu ile ya ubongo inayoona mambo kabla.

Msomaji mmoja, Jay Jay, aliibua [7]suala la Padre Mkatoliki aliyefurushwa kutoka nchini [9] Zambia, kwa sababu ya kile kilichoelezwa kwamba hakuwa na vibali vyote vinavyohitajika:

Mnajua nini, sheria ina mambo ya ajabu sana, ya kuja na kukung'ata hasa kwa wanasiasa wanachokatakata kona kama akina Kambwili, tukumbuke kwamba mwezi huuhuu yule padre Mnyarwanda alifurushwa kwa sababu ya kukosa vibali; kama wanashirika Wazambia wenzake na padre huyo kule Chipata wangeomba serikali ya PF [Patriotic Front] kwamba kwa nini wasingeachana na jambo hilo na kumruhusu kuendelea kubaki; je, Kambwili angewajibu vipi swali hilo?

Akimtakia kila la heri Renard, Renard, Ndanji Wayaya aliandika [7]:

Hongera sana HR kwa kazi uliyofanya AFCON. Tafadhali rudia tena rekodi hiyo mwaka 2013. Kwa ruhusa, uraia n.k. umezikonga nyoyo zetu, endelea kuishi hapa Zambia kwa muda mrefu kadiri unavyopenda. Fanya tu ukaaji wako uwe rasmi. Achana na maoni ya watu wengine. Daima binadamu wataendelea kulalamika.

Hata pale tulioshinda AFCON 2012, walilalamika kwamba ilikuwa kwa njia ya penati. Kwamba ilikuwa kama bahati nasibu tu. Walitaka ushindi ndani ya muda wa kawaida.

HR, HR.HR!!!!!!!!

Habari hiyo iliibua ufuatiliaji kupitia Twita.

@ZibaniZambia [10]: Serikali yampa Herve Renard Kibali cha Ukaazi na Gari Jipya. Isome sasa kupitia http://tinyurl.com/8nde5vb [11]

Mtumiaji mwingine alilipoti heshima hiyo:

@modoubeyai [12]: Mfaransa Herve Renard ametunukiwa ukazi wa kudumu nchini Zambia kama heshima ya kutambua mafanikio yake katika Kombe la Washindi Barani Afrika mwaka 2012.

Mtumiaji mmoja alipiga hatua ya mbele zaidi na kumpa Renard jina la katikati la Kizambia:

@DJLBCZambia [13]: Kwa hiyo, tumeambua, mabibi na mabwana, kuwa jina la kati la Herve Renard la Kizambia ni “Madalitso” [Baraka]