Uganda: Kuvunja Utamaduni wa Ukimya Kuhusu Haki za Afya.

Huduma za afya zinapaswa kutolewa bure nchini Uganda. Hata hivyo, kumekuwa na upungufu wa nuda nrefu wa dawa na wahudumu wa afya katika vituo vya afya vya taifa.

Video iliyoandaliwa na Results for Development (Matokeo kwa Maendeleo), shirika la kimataifa lisilo la kibiashara ambalo lina malengo ya kutafuta suluhisho la matatizo sugu yanayokwamisha maendeleo, iliwekwa kwenye mtandao wa intaneti siku za hivi karibuni ili kuwahamasisha watu wa Uganda kuvunja ukimya wao na kupigania haki ya afya zao.

Akitambulisha video hii, Oscar Abello anaandika kuwa:

Uganda imeshapiga hatua kubwa katika miaka kadhaa iliyopita kwa kujenga majengo kwa ajili ya mifumo ya kusambaza dawa kwa jamii- vituo vya kuhifadhia na kusambazia dawa- lakini huduma za afya bado si za kuridhisha. Vituo vingi vya afya vinaendeshwa bila ya kuwa na dawa kati ya miezi 2 hadi 3 tokea dawa zipelekwe, wakati katika majengo ya serikali ya kuhifadhia dawa kuna hifadhi kubwa.
Matizo ya mfumo wa usambazaji wa dawa sio jambo jipya kwa watu masikini nchini Uganda, wengi wao wakiwa vijijini, lakini kuna namna chache sana za kutoa taarifa hizo kwa wataalamu wa afya walio katika nafasi ya kufanya jambo kuhusiana na changamoto hizo.

Katika video hii, Denis Kibira, mshauri wa afya wa HEPS Uganda, shirika la wanufaika wa afya linalosaidia kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu nchini Uganda anasema:

nataka kuona nchi ambayo watu hawafi kwa kuwa wameshindwa kupata huduma wanayostahili.

Mwaka 2006, mawaziri watatu walipoteza nyadhifa zao baada ya kuripotiwa kuwa walihusishwa na ufujaji wa fedha katika idara ya afya. Mashitaka yao bado yanasikilizwa mahakamani.
Patients on the floor of Mulago Hospital, the National Referral Hospital. Photo courtesy of williamkituuka.blogspot.com
Wagonjwa wakiwa wamekaa chini katika hospitali ya rufaa ya Taifa ya Mulaago. Picha kwa hisani ya williamkituuka.blogspot.com

Rosette Mutambi, mwanzilishi na mkurugenzi wa HEPS Uganda, katika video hii anasema kuwa huduma ya afya nchini Uganda inapaswa kuwa bure, lakini hali haiko hivyo kwa sasa. Anaongeza kuwa, vituo vya afya vinafanya kazi kupita uwezo wake ikiwa na maana kuwa hata wafanyakazi wa sekta ya afya nao wanafanya kazi kupita uwezo wao.
Pia, Uganda ina tatizo sugu la kukatika kwa umeme ambalo linaathiri sana vituo vya afya ambavyo havina majenereta ya kutoa nishati hiyo pindi umeme unapokatika hasa kwa kuwa kuna dawa zinazohitaji kuhifadhiwa katika majokofu.

Kwa mujibu wa Moses Kamabare, msimamizi mkuu wa Bohari ya Dawa ya Taifa, shirika linalohusika na kuhifadhi na kusambaza dawa katika vituo vya afya, huwa wanasambaza dawa mara moja katika wilaya zote kila baada ya miezi miwili. Lakini mfanyakazi wa kituo kimoja cha afya anasema kuwa vituo vya afya kwa kweli huwa vinapokea dawa mara moja kila baada ya miezi mitatu.

Bohari za dawa za Uganda mara zote huwa zimejaa, lakini katika vituo vya afya hakuna dawa. Baadhi ya watu wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 10 kufuata vituo hivi vya afya ili kujipatia huduma za dawa na kuambulia patupu. Hali hii inawakatisha watu tamaa na kuwafedhehesha kiasi cha kuamua kutorudi tena katika vituo hivi kwa ajili ya matibabu.

Kuna mambo mengi yanayopaswa kutimizwa ili kuimaridha huduma za afya nchini Uganda, ambayo ni: usambazaji wa dawa wa haraka na wa mara kwa mara, sekta ya afya kutengewa fedha za zaidi, vituo vingi zaidi vya afya, mishahara ya kutosha ya wafanyakazi katika sekta ya afya, pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi vya kutosha katika vituo vya afya.
Pia kuna changamoto ya upungufu wa madaktari, baadhi yao wakituhumiwa kuiba dawa kinyemela kwa ajili ya kliniki zao binafsi.

Lakini swali kubwa la kujiuliza ni kuwa; Je, video hii hatimaye itawahamasisha watu wa Uganda kuvunja ukimya?

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.