Tanzania: Kufungiwa ‘Mwanahalisi’, uhuru wa habari mashakani?

Ulimwengu wa habari Tanzania umepokea kwa mshtuko mkubwa kufungiwa kwa gazeti la kila wiki ‘MwanaHalisi‘. Taarifa ya Serikali iliyochapishwa kwenye blogu ya Wavuti ilieleza kwa ufupi kwamba

Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258 lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar es Salaam tarehe 27 Julai, 2012.

Toleo la gazeti la MwanaHalisi lenye habari iliyosababisha kufungiwa kwa jarida hilo. Picha ya kundi la mtandao wa Facebook liitwalo Mabadiliko Forums.

Taarifa hiyo iliongeza:

Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.

Kupitia taarifa yake hiyo, Serikali inatoa sababu ya kulifungia gazeti hilo kuwa ni ‘kuandika habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini’.

Profesa Joseph Mbele anayemiliki blogu inayoitwa hapa kwetu, aliandika maoni yake kuhusu habari hiyo ya kufungiwa gazeti la MwanaHalisi, anasema:

Serikali ingekuwa na busara, ingetafakari sana masula haya ya Dr Ulimboka kama yalivyoripotiwa na MwanaHalisi. Kulizuia gazeti hili, nahisi kutaimarisha dhana iliyozagaa katika jamii kwamba serikali inahusika katika shambulio dhidi ya Dr Ulimboka. Inawezekana serikali haihusiki, lakini vitendo hivi vinaweza kuwa vya hasara kwa serikali yenyewe.

Anahitimisha kwa kuandika:

Nimalizie kwa kusema kwamba naudhika na vitendo vya kuhujumu haki yangu ya kusoma ninachotaka kusoma. Ni mtu mzima na nina akili zangu. Naweza kuchambua chochote ninachosoma. Serikali inapozuia gazeti au kupiga marufuku kitabu naona inawatukana wananchi, kwamba hawana akili ya kusoma na kuchambua mambo.

Geophrey Mlewa anauliza kupitia ukurasa wake wa Facebook:

Tunaenda wapi na ubabe kama huu? Wanadai sheria ilikiukwa, kweli wangeandika habari za kusifia serikali wangelifungia pia???

Tumaini Anthony anaandika maoni kwenye ukurasa wa Facebook wa Geophrey hapo juu akisema

…mawe yataongea!Amen

MwanaFacebook Hilda M. Mbangati anaandika kwenye sehemu ya maoni ya ukurasa huo:

Duuh hii ndo Serikali bwana! CCM hoyee…

Simon Mkina alifanyiwa tag kwenye Facebook ambapo kuna picha ya gazeti la MwanaHalisi na maoni chini yakisema

R.I.P MwanaHalisi, sasa tusome udaku

Kwenye ukurasa wake wa Facebook, Ismail Mbuyu anaandika maoni haya:

Kama kuna kitu kimeniuma ni kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi. Nategemea kwamba Rais Kikwete atalifungulia. Why? Lin reveal weaknesses za wateule wake. Kubenea atapataje innermost details while he isn't at the source? Let the journal continue giving us the facts. It is upon the President 2 check his house not Kubenea.

…Nategemea kwamba Rais Kikwete atalifungulia. Kwa nini? Linaweka wazi udhaifu wa wateule wake. Kubenea atapataje taarifa za ndani namna hii wakati hayuko kwenye chanzo chenye cha habari? Acheni jarida liendelee kutupa ukweli wa mambo ulivyo. Ni juu ya Rais kutazama upya nyumba yake na sio Kubenea.

Katika kiungo hiki kuna maelezo kuhusu Saed Kubenea, Mhariri Mtendaji wa gazeti la MwanaHalisi. Taarifa ya kufungiwa kwa gazeti hili ilitangazwa na mtandao wa JamiiForums hapa, ambapo taarifa hiyo iliambatana na maoni haya:

Wajameni serikali hii inataka kutufunga mdomo tuendelee kuwa gizani tusijue madudu yao.

Na mtoa maoni anayejiita Ndahani aliandika:

Haaahaa! Ile dozi ya Kubenea ilikuwa kubwa kuliko. maana amewaweka jamaa uchi bila kutegemea.

JF Senior Expert Member Osokoni anahoji:

Mbona Radio Imani inayohubiri chuki za kidini kila siku haifungiwi?? Kuna double standards kwenye media??

Kwa upande wa Ritz, yeye anasema:

Safi sana gazeti la udaku na majungu na kufitinisha watu hata hivyo serikali imechelewa mno kulifungia.

Na hii haikuwa mara ya kwanza kwa gazeti hili kufungiwa. Liliwahi kufungiwa kwa miezi mitatu mwaka 2008.

Historia ya kufungiwa magazeti Tanzania imeanza siku nyingi soma hapa katika blogu ya Kulikoni Ughaibuni ya Chahali, kuna makala inayohoji kuhusu Uhuru wa Habari wa Tanzania: Tatizo ni Dola, Uoga au Kujikomba?

Maswali bado ni mengi kuhusu uhuru wa habari nchini Tanzania. Je, hali itakuwaje kwa vyombo vingine vya habari? Na John Mnyika naye anasema nini kuhusu suala hili la uhuru wa vyombo vya habari? Hebu tusubiri na tuone.

2 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.