Somalia: Migawanyiko Mikubwa Kuhusu Katiba Mpya

Somalia haijawahi kuwa na serikali kuu inayotawala nchi nzima tangu kuanguka kwa Muhammad Siad Barre mwaka 1991. Serikali ya shirikisho ya mpito (TFG) ndiyo serikali ya Jamhuri ya Somalia inayotambulika kimataifa.

Baada ya majadiliano ya kisiasa nchini Ethiopia, viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa vya Somalia walikubaliana kuchukua hatua za kisiasa ili kumaliza kipindi cha mpito na kumchagua Raisi mpya. Miongoni mwa hatua zilizobainishwa katika ratiba changanuzi ni kuandaa muswada wa katiba mpya.

Kamati ya Ufundi ya Mapitio ya katiba mpya ilishiriki katika kikao cha siku nne mfululizo katika jiji la Nairobi:

Picha ya Kijeshi ya Meja Jenerali Mohamed Siad Barre, Rais wa Somalia aliyetawala kwa muda mrefu kuliko wengine. Chanzo: maktaba ya Congress (Kwa matumizi ya umma)

Kikao cha siku 4 mfululizo kilichojumuisha waweka saini wa makubaliano, kimekwishahitimishwa mjini Nairobi. Kazi hii ni ya ufuatiliaji wa yaliyotekelezwa katika kikao cha waweka saini cha hivi karibuni kilichofanyikia mjini Addis Ababa ambapo mambo mengi ya kikatiba yalikubaliwa na baadhi ya mapendekezo -yaliyoandaliwa na Tume Huru ya Katiba ya Serikali ya Shirikisho- yamerekebishwa baada ya makubaliano ya kisiasa ya amani baina ya waweka saini wa mpango huo wa amani wa kumaliza kipindi cha mpito, yaliyofanyika Mogadishu mwezi wa 9 mwaka jana. Mamlaka ya kiufundi ya Kamati ya Mapitio, kwa mujibu wa tamko rasmi la Addis Ababa ni kukamilisha mchakato wa katiba.

Waziri wa Mambo ya Katiba ambaye ndiye aliyeitisha mkutano aliwaeleza washiriki pamoja na vyombo vya habari kuwa “hatua ya kuelekea mwisho wa kipindi cha mpito zinaendelea kuwapo kukaribia sana siku hadi siku, na tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuipatia Somalia katiba inayoistahili na itakayowatumikia watu wa Somalia

Washiriki wa kamati ya ufundi ya mapitio wakiwa mjini Nairobi. Picha kwa idhini ya: http://horn.so/

Mahad Abdalle Awad, Naibu Waziri wa Mipango na Ushirikiano wa Kimataifa wa Somalia ana matumaini makubwa kwamba nchi hiyo katika muda mfupi ujao itapata katiba mpya:

Waoga wanatumia mbinu za vitisho ili kushawishi maoni ya wengi yawe ni ya kuzuia mabadiliko na mchakato huu kwa kusambaza taarifa ambazo si sahihi kuhusu uundwaji wa katiba na kikao cha bunge la katiba kilivyopangwa. Wale wasiotaka kuamini, na wenyewe wasiwasi kwa asili baina yetu, wamekuwa na tabia ya kuonesha mashaka na mafaninikio ya wengine na ambao si warahisi kupokea mabadiliko. Nukuu maarufu ya Dale Carnegie inafafanua kwa usahihi kasumba ya wote wenye tabia za kupinga pale alipoandika “mjinga yeyote anaweza kukosoa, kushutumu na kulalamika, na wajinga wengi ndivyo wafanyavyo.”

Walalamikaji mara nyingi wanasambaza uongo kupinga kila kitu ambacho wengine wanakifanya. Kuhusu suala hili la Bunge la Katiba, wanasema kuwa katiba inaweza kuidhinishwa kwa kukubaliwa na wengi kupitia kura ya maoni tu bila kujali ukweli wa kihistoria ulio wazi kuwa Jamhuri ya Somalia yenyewe ilipatikana kwa katiba ya mwaka 1960, iliyoidhinishwa na bunge la katiba lililokuwa na wajumbe 110 tu, tena kwa mchakato uliochukua siku 29, ambapo mchakato wa kupata maoni ya wananchi ulifanyika tarehe 21 Julai, 1961, zaidi ya mwaka mmoja baadae..

Hata hivyo, Mohamed Ali Hassan, Mwenyekiti wa Baraza la Amani la Somalia-Marekani na Manuela Melandri, mwanafunzi anayesomea shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London, waliweka bayana kuwa wasomali wengi wanauangalia muswada wa katiba kwa mashaka makubwa:

Matumaini makubwa kwa jamii ya kimataifa hayaeleweki kwa wa-Somali wenyewe, ambao badala yake wanaiangalia rasimu hiyo kwa mashaka makubwa wakiiona kama iliyoandaliwa na wageni, yenye makosa na kimsingi isiyo ya kidemokrasia.

Kuielewa hali hii, lazima mtu aanze kwa kuhoji masuala ya msingi. Kitu gani hakiendi sawa katika mchakato wa katiba mpya ya Somalia na kwa nini ukamilishaji wa katiba hii umekuwa ukikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wasomali walioelimika, watu maarufu wa dini, wale wasio katika mrengo wowote wa dini, Mawaziri Wakuu waliotangulia wa Somalia, wanawake, wasomi na hata jumuiya za wa-Somali waishio nje ya nchi?

Kwanza, kuna mambo yanayohusiana na maudhui ya Katiba na utekelezekaji wa mapendekezo yake.

Lililo kubwa kabisa, ni swali la hali ya kuwa shirikisho ambalo linabaki kuwa jambo linaloleta mpasuko mkubwa kabisa. Maoni yanaweza kuwa ya kuunga mkono na ya kupinga mpango wa Somalia kuwa na muundo wa shirikisho.

Rais wa Somalia, Sharif Sheikh akiwa Addis Ababa, Ethiopia, wakati wa mkutano wa 12 wa nchi huru za Afrika uliofanyaka Feb. 2, 2009. Chanzo: Serekali ya shirikisho ya Marekani (Kwa matumizi ya Umma)


Lakini m-Somali mmoja alikuwa na hoja kuwa katiba mpya inaweza kuboreshwa mbeleni. Wa-Somali hawana muda wa kuisubiri kupata Katiba isiyo na makosa yoyote:

Tupende tusipende, tunapoona taswira ya watu wa Somalia ulimwenguni kote, na tukifananisha na hali yetu (angalau, wenzetu waishio nje ya nchi kwa amani), je ni kweli tunahisi kuwa hao kaka na dada zetu wanahitaji katiba inayoweza kuwasaidia hivi sasa kwa kuwa wanahanganika kujinasua na hali mbovu? Lifikirie hili: maxay ku gaaraan mustaqbalka?

Unapaswa kufahamu kuwa, sikuandika makala hizo za habari zilizotajwa hapo juu, mimi sio miongoni mwa kundi linalojadili katiba mpya na sipo hapa kwa nia ya kuhalalisha ikiwa katiba mpya ni nzuri, mbaya au ni mbovu. Ninachotaka kuwakumbusha ni kuwa: wale walio kakika uhitaji wanaweza wasiwe na muda wa kusubiri katiba mpya isiyo na makosa na yenye mvuto; wanahitaji katiba itakayoweza kuwasaidia kupita katika mazingira waliyonayo hivi sasa; Tena lililo muhimu zaidi, siko hapa kupinga wazo la yeyote yule -ninatoa maoni yangu tu kama ambavyo na mwingine yeyote angeweza kufanya. Pamoja na hayo, suluhisho bora zaidi ninaloliona, angalau kwa maoni yangu, hebu tuanze kujadili jinsi ya kuiboresha katiba mpya kwa ajili ya wakati ujao.

Mohamud Uluso anauchukulia rasmu ya katiba kama “kazi inayoharakishwa, toleo la hivi karibuni zaidi likipatikana katika lugha ya kisomali pekee wakati rasimu nyingine za zamani au zile batili zikiwa zinazagaa katika mtandao wa intaneti”:

Inaonekana kuwa mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa unaoonekana kuwa ni wa busara kwa Somalia si chochote bali ni sehemu ya mkakati wa ulaghai ili kuiweka Somalia na wa-Somali katika matatizo. Badala ya kuwakomboa wasomali halisi, wanaohitaji na wanaoendelea kuishi nchini mwao na kuendelea kuiendeleza nchi yao wenyewe na jamii zao ndani ya Somalia, rasimu hii ya katiba inaonekana kuwa ilani ya kuwakumbatia wageni na pia kuwakandamiza milele wazawa wa Somalia.

Wasomali wengi pamoja na wasomi wao wanaonesha mashaka yao kuwa ni wakati muafaka wa kujihusisha katika mchakato wa kuunda katiba mpya katika kipindi cha migongano ya kiraia na matatizo ndani ya Somalia na ushangae ni kwa nini mamilioni ya dola yameshatumiwa na waongozaji watokanao na kile kinachojulikana kama jamii ya kimataifa ya kuiunda tena katiba, wakati katiba iliyopo ya Somalia ingaliweza kurekebishwa tu kama sababu yoyote halisi ingeweza kutolewa na tena kwa kufuata taratibu na pia kwa mfumo wa uwakilishi-inayotoa taswira ya kweli na utayari wa watu wa Somalia.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kilichopo ndani ya serikali ya mpito ya shirikisho (FGM) kwa sasa imeruhusiwa na katiba mpya ya Somalia iliyopendekezwa, ambayo itawasilishwa kwa utekelezaji kwa baadhi ya “viongozi wa jadi” waliochanguliwa. Ni utaratibu wa aina yake ambao umoja wa mataifa na washirika wake wanataka mambo yawe kwa kadiri ya wanavyotaka, au kwa kadiri ya wakubwa wao wanavyotaka iwe..

Abduallhi Jamaa anachanganua hoja mbalimbali kuhusu mswada huu wa katiba unaoonekana mtandaoni, katika redio zinazotangaza kwa lugha za ki-Somali na katika mikutano vijiji na hata migahawani:

Wachambuzi wanasema kuwa mswada wa sheria uliopendekezwa unaonekana kama hatua muhimu sana, lakini ambayo inaweza kuigawa zaidi Somalia katika maeneo mawili yanayojitegemea au yenye aina fulani ya kujitegemea, na hata kufikia kuwa na majimbo madogo madogo.
—-

“Kuna mkanganyiko wa wazi kabisa. Hakukuwa na elimu yoyote ya uraia ya kufafanua suala la muswada wa katiba pamoja na dhima ya sheria zilizopendekezwa na hii inamaanisha kuwa watu wengi hawana uhakika na yaliyomo (katika mswada wa katiba), wengi zaidi hawajawahi hata kuusikia mchakato wenyewe” yeye [Hassan Sheikh, kiongozi wa Chama cha Amani na Maendeleo, PPD) alilieleza shirika la Habari ya Somalia.

Miongoni mwa mambo yanayojadiliwa ni pendekezo la mfumo wa serikali, mkanganyiko wa masualaa ya mali asili na ushawishi wa kidini. Baadhi ya wadau wanasema kuwa lugha iliyotumika katika mswada haieleweki, jambo linaloweza kuleta tafsiri tofauti na ile iliyokusudiwa.

—-

“Suala hapa sio kutokuelewana kuhusu maudhui yaliyomo. Suala hapa linahusiana na kukosekana kwa uwakilishi wa walio wengi. Sitamani kuwa sehemu ya bunge la katiba ambalo haliwakilishi dira na malengo ya Somalia”, alisema kiongozi wa jadi, Mohamed Hersi..

Mradi wa ‘Google Ideas’ ulitengeneza mpango wa majaribio kwa kushirikiana na idhaa ya Somalia, Idaara ya Afrika ya Sauti ya Marekani (VOA) kuwasaidia wa-Somali kuandikisha maoni yao kwa njia rahisi kwa kubofya mara kadhaa tu. Pamoja na mambo mengine, takwimu za maoni zinaonyesha kwamba, wa-Somali wanahitaji Somalia itakayozingatia misingi ya “Sharia” za kiislamu kwa makosa ya madai na jinai, serikali kuu iliyo imara na (wa-Somali) wamegawanyika juu ya hatua za kuwajumuisha wanawake katika muundo wa serikali.

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.