Misri: Mubarak Afariki Dunia kwa Mara Nyingine

Makala haya ni sehemu ya Habari zetu maalum za Mapinduzi ya Misri 2011.

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak amewahi kufa angalau mara moja kwa kila baada ya majuma machache tangu kuanza kwa mapinduzi ya Misri, yaliyouangusha utawala wake uliodumu kwa miaka 32. Watumiaji wa mtandao wanaitikia tetesi za hivi karibuni kuhusu afya yake.

Lubna F. aliwahakikishia wasomaji wake kwamba hali ya afya ya Mubarak ni habari isiyokoma kujirudia-rudia. Aliandika:

@fatanil: Wapendwa wahamiaji na wageni nchini humu, ninahisi kuwa wengi wenu mmechanganikiwa. Kwa hivyo kwa kufafanua tu, Mubarak amefariki na yu hai bado. Kifo chake hutokea kila baada ya majuma machache, wala msiogope.

Na Jonathan Moremi alitwiti ratiba ya kifo cha Mubarak:

@jonamorem: HABARI ZA HIVI PUNDE: #Mubarak atafariki dunia leo saa 5: 57 asubuhi na kwa mara nyingine saa 10:12 alasiri. Tafadhali onyesha moyo wa huruma. Onyesho linalofuata ni kesho saa 1:48 asubuhi na 9:44 alasiri.

Hata hivyo, Tarehe 19 Juni, habari za kifo cha Mubarak zilionekana kuwa na ukweli.

@HaYatElYaMaNi: Habari mpya: Imethibitika Mubarak amefariki #mubarak

Shirika la habari nchini Misri ‘Shirika la Habari la Mashariki ya Kati’ liliripoti habari hizo [kiungo hakifunguki, na tovuti imeripotiwa ‘kufa’ pamoja na Mubarak], na Ahram Online baadae aliandika , “Hosni Mubarak amethibitika kuaga dunia mara tu baada ya kufikishwa kwenye hospitali ya kijeshi kwenye mtaa wanakoishi matajiri uuitwao Maadi, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Misri, MENA”.
Kwa hali ilivyokuwa, ilionekana sasa ni rasmi, kama anavyotwiti Ekram Ibrahim:

@Ekramibrahim: Ninadhani #Mubarak amefariki ‘rasmi’

Lakini kwa mara nyingine, waandishi wa habari wa ki-Misri na wale wageni waligeuka kuwa wahanga wa tetesi za kifo cha Mubarak. Saa moja baadae, habari zilisema kuwa Mubarak alikuwa bado yu hai, au ‘angefufuka’ tena kama Ms. Entropy alivyotwiti:

@MsEntropy: #Njama za Mubarak zimeanza. Ni kwamba #Mubarak anamwiga Yesu katika jitihada zake za kutafuta kuungwa mkono na Serikali ya kijeshi. Atafufuka!

Moja wapo ya akaunti za twita zilizotengenezwa kwa majina ya Mubarak zilitwiti:

@NotMobarak: Bazzinga! Hujawahi kujifunza? #Mubarak huwa hafi.

Josh Shahryar aliweka vitu vilivyotumika kutengeneza kinywaji cha kumfufua Mubarak:

@JShahryar: Vyanzo vya siri vimeniambia kinywaji kilichotengenezwa kwa makucha ya Gaddafi, meno ya Prince Nayef na mapembe ya Assad ndicho kilichomfufua.

Imran Garda ana nadharia tofauti kuelezea mshituko huo wa moyo unaompata Mubarak.

@ImranGarda: Wamisri siku zote wamekuwa na wasiwasi na ukweli wa habari zinazotaja moyo wa Mubarak. Hawakuwahi kuwa na uhakika kuwa anao.

Pamoja na wale wote waliokuwa wakijiuliza ni mara ngapi Mubarak atandelea kuishi au kufa, Baseem Babry alitwiti:

@Bassem_Sabry: Japo siwezi kuthibitisha haya kwa vyovyote, kuna hadithi maarufu sana inayodai kwamba baba wa Mubarak aliishi miaka 104, na tena inasemekana alifariki dunia kwa ajali ya gari.

Nathan Nemo alionyesha hofu kuhusu idadi ya marekebisho yanayoweza kufanyika kwenye ukurasa wa Wikipedia unaoelezea maisha ya Mubarak. Melissa Rose akapendekeza Mubarak Zombie liwe kama jina la bendi nzuri na BuddhasHag akatwiti:

@BuddhasHag: Siamini katika mapenzi yanayozaliwa kwa kumwona mtu kwa mara ya kwanza tu, ninaamini kifo hutokea kwa mshutuko wa kwanza wa moyo. Lakini kwa mara nyingine Mubarak inabidi anionyeshe vinginevyo.

Si tu Wikipedia, lakini pia hata magazeti yalilazimika kuhariri habari zao za awali kuhusu ‘kifo’ cha Mubarak. NewsDiffs (@newsdiffs), ambaye hutazama matoleo mbalimbali ya makala zinazowekwa zaidi kwenye tovuti za habari, alichapisha ulinganifu kuonyesha namna habari ya jarida la New York Times ilivyohaririwa pale ilipofahamika kwamba Mubarak alikuwa bado hai..

Habari kuhusu maisha au kifo cha rais huyo wa zamani wa Misri si habari pekee ambayo haiwezi kuthibitishwa nchini Misri siku hizi. Kuna mashaka kuhusu nani atakuwa rais ajaye, kufuatia wagombea wote wa urais Ahmed Shafiq na Mohammed Morsi kudai wameshinda duru ya pili ya uchaguzi wa juma lililopita.

@the_blacklisted: Shafik na Morsy wameshinda na kushindwa uchaguzi. Mubarak yu hai na amekufa. Jeshi linatawala na halitawali Misri. Bado name si mwenye furaha.

Mwisho, ikitokea unasoma habari hizi siku chache baadae, na una wasiwasi ikiwa Mubarak yu hai au amefariki sasa, usijali, kuna namna unaweza kutuma maombi kwa ajili hiyo.

Makala haya ni sehemu ya Habari zetu maalum za Mapinduzi ya Misri 2011.

1 maoni

Sitisha majibu

jiunge na Mazungumzo -> Fredrick ruttahanamwa kasusura

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.