Salamu kutoka Kenya!
Karibuni katika matangazo ya sauti ya moja kwa moja (Podikasti) kutoka katika mkutano wa Sauti za Kimataifa. Je, mwelekeo wa vyombo vya habari vya kiraia kwa siku zijazo ni upi? Kupitia toleo hili na yatakayofuatia mtaweza kuwasikia wahariri, waandishi, waanzilishi wenza na hata washiriki wengine wa Mkutano huo kutoka mjini Nairobi wakijadili mustakabali wa namna tunavyofanya kazi kwa pamoja mtandaoni.
Mkutano huu hufanyika kila baada ya miaka miwili na huwa kuna mada nyingi katika ajenda, labda hata nyingi kuweza kuenea katika podikasti moja lakini kwa hakika kuna mengi ya kutafakari.
Kwa kuanzia, hebu turudi nyuma, kwa siku za kitambo na tuangazie asili ya Sauti ya Dunia. Mwanzilishi mwenzaEthan Zuckerman anaelezea namna Sauti za Dunia zilivyozaliwa, kile ambacho hufanyika katika mikutano hii, na kile anachofikiri kuwa mustakabali wa Jumuiya hii.
Mkutano wa Sauti za Dunia ni mahali pa kupatanika na kufahamu mengi zaidi kuhusu wahariri, waandishi na wachangiaji wengine waliosafiri kutoka kila kona ya dunia. Kila mtu alikuwa na msisimuko wa pekee, lakini mmoja wapo wa washiriki waliokuwa na furaha alikuwa Elaine Díaz anayetoka Havana, Cuba. Hapa anaeleza kidogo zaidi kuhusu raia wa mtandaoni wa nchi yake ya Cuba.
Kwa kweli mkusanyiko huu usingekuwa na maana hasa ya Sauti za Dunia bila ya kuwa na watu wenye sauti maridadi kutoka kote duniani. Andrea Arzaba ni mwandishi wa habari nchini Mexico ambaye alikusanya utafiti mdogo kuhusu tukio hili, kwa kuanzia na fikra zake mwenyewe.
Daudi Were ni mwanablogu wa Kenya anayeandika katika blogu ya Mentalacrobatics. Yeye ndiye aliyekuwa anaongoza ratiba katika mkutano huu wa umma uliohudhuriwa na watu 300. Alieleza kuhusu uhusiano wake na Jumuiya ya Sauti za Dunia na jinsi teknolojia ya Kenya inavyozidi kuwa ya ubunifu, hasa katika sekta ya vifaa vya mkononi kama simu.
Athari ya Vyombo vya habari vya kiraia
Kwa kupitia Sauti za Dunia, watu wengi ambao mara nyingi hupuuzwa na habari zao kutokupewa nafasi katika vyombo vikuu vya habari wanawweza kupata nafasi na hivyo maoni na habari zao kupewa kipaumbele.
Leila Nashawati Rego ni mwanaharakati wa haki za binadamu mwenye asili ya Uhispania na Syria. Ni muhadhiri wa stadi za mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Carlos III, na pia anaandikia magazeti kadhaa yenye kuheshimika. Tulijadili kuhusu kukua kwa uandishi wa mtandaoni na matokeo ya kutanuka kwa uandishi huo.
Muda mrefu, lakini sio mwisho
Habari zenye mchanganyiko wa huzuni na furaha zilitoka kwenye mkutano huu vile vile. Sami Ben Gharbia kutoka Tunisia alitueleza kuwa anajiuzulu nafasi ya Mkurugenzi wa Utetezi wa Sauti za Dunia, ama Global Voices Advocacy. Kama ilivyotarajiwa aliwaeleza washirika yale aliyokuwa ametimiza na yale anayotaka kufanya katika siku za usoni.
Kama ilivyo desturi, nawashukuru wachangiaji, wazalishaji na watunga nyimbo waliosaidia kufanya warsha ifaulu. Unaweza kuangalia mihutasari mingine katika twita kupitia alama ishara ya #GV2012 na pia kwa kuangalia kurusa maalumu za Mkutano.
Podikasti ya Sauti za Dunia. Dunia inaongea, natumaini umekuwa ukisikiza.
Shukrani kwa watunga nyimbo
Katika podikasti hii unaweza kusikiliza nyimbo nyingi nzuri zilizochini ya Haki miliki ya Creative Commons. Shukrani kwa Mark Cotton kwa ubunifu wake na pia shukrani kwa sauti murua ajabu katika maonyesho ya moja kwa moja mkutanoni na pia zilizorekodiwa tayari ambazo zimetusaidia kutayarisha podikasti hii.