Afghanistan: Mwanafunzi wa Sekondari Agundua Kanuni ya Hisabati

Kama hujazoea kusoma habari za mafanikio ya kielimu katika nchi ya Afganistani, habari hii ni ya kukubadilisha mtazamo wako. Mnamo tarehe 30 Juni, 2012, Kituo cha Sayansi katika mji wa Kabul, kilitangaza kuwa Khalilullah Yaqubi, mwanafunzi wa shule ya sekondari kutoka katika Jimbo la Ghazni, kwa juhudi zake mwenyewe aligundua kanuni ya kimahesabu inayoweza kutumika katika kukokotoa milinganyo ya kwadratiki ya mtajo mmoja ya ukomo wa kipeo cha pili. Khalilullah ni mwanafunzi wa darasa la 11 (sawa na kidato cha tano Afrika Mashariki) katika shule ya sekondari ya Al-Beruni iliyo katika mitaa ya Nawabad nje kidogo ya jiji la Ghazni.

Akiongea kuhusu kanuni hiyo, Khalilullah anasema:

Sijawahi kuiona kanuni hii katika kitabu chochote. Wala sijawahi kutumia chanzo chochote, au kufanya udanganyifu wowote kwa kutumia mtandao wa intaneti. Hizi ni kutokana na jitihada zangu mwenyewe. Kupitia kanuni hii, tunaweza kukokotoa maswali mbalimbali ya milinganyo (sic).

Baadhi ya watumiaji wa Twita wamezipokea habari hizi kama ishara ya maendeleo ya sekta ya elimu nchini Afganistani. Kwa mfano, Mulex alitwiti:

Loo! Habari za kushangaza kutoka Afghanistani. Ni ishara ya maendeleo kwa mfumo wa elimu yao.

Mtumiaji mwingine wa Twita, Jasur Ashurov (‘mkazi asiye mzawa kutoka Asia ya Kati aliandika:

Si rahisi sana kupata habari nzuri kutoka nchini Afghanistani. Ndio maana nimekuwa na furaha sana baada ya kusoma habari hii.

Akifupisha maneno aliyowahi kuandika Jasur Ashurov, mwanasayansi na mshairi wa Kirusi ,Jasur Ashurov aliongeza [ru]:

…и может собственных Ньютонов и быстрых разумом Платонов земля афганская рожать…

…… ardhi ya Afghanistani inaweza kuwazaa Newtoni wake na akina Plato wenye akili….

Mafanikio haya ya mwanafunzi huyu yameonekana pamoja na hali ngumu inayoikabili sekta ya elimu katika jimbo la Ghazni. Wanachama wa ikkundi cha kigaidi cha Kitalebani wameshafunga shule nyingi katika jimbo hilo. Hata hivyo, siku za hivi karibuni, takribani wakazi 400 wa kutoka moja ya wilaya za jimbo hili walitofautiana na kundi lililojitenga na kufanikiwa kufungua tena shule 81 kati ya shule 83 katika eneo hilo.

Kwa ujumla, kumekuwa na maboresho katika sekta ya elimu nchini Afghanistan tangu mwaka 2001,Talebani ilipoondolewa madarakani. Zaidi ya shule 5,000 zimeshajengwa (pdf) nchi nzima tangu mwaka 2003. hata hivyo, shule nyingi bado zinakosa zana za kisasa za kufundishia na kukabiliana na upungufu mkubwa wa walimu walio na sifa stahiki. Kwa upande mwingine, shule nyingi za wasichana siku za hivi karibuni zilishambuliwa na watu waliojitenga wanaopinga elimu kwa wanawake nchini Afganistani.

Katika gazeti la Outlook Afghanistan, Dilawar Sherzai anaelezea mfumo wa elimu wa Afghanistani kama ifuatavyo:

Nchi yetu ya Afghanistani ni miongoni mwa nchi ambazo sekta ya elimu haijapewa msisitizo stahiki. Moja ya sababu kubwa imekuwa ni mwendelezo wa kutokuwa na utulivu wa kisiasa, jambo linaloizidi uwezo jamii. Vita na migogoro -ya kitaifa, ya kikanda na hata kimataifa- ambayo imekuwa ikiitumia ardhi ya Afghanistani kama kiwanja cha vita imesababisha maendeleo kudorora kwa kiasi kikubwa katika nyaja za kijamii na za kielimu. Kuanzia mapinduzi ya Kisovieti ya mwaka 1979, mtu anaweza kuhesabu maelfu ya mapigano na usumbufu uliozuia kuanzishwa kwa mfumo wa elimu wa kuridhisha. Matatizo, ambayo ni ya kiasili zaidi, yamekuwa ndio yanayozingatiwa sana na watu kuliko mfumo wa elimu.

Pamoja na changamoto zote hizi, watu wengi wa Afghanistan wamefanikiwa kupata elimu, na wakati mwingine wakijisomesha wenyewe. Mwaka 2011, mkazi mwingine wa Ghazni aliye na kipaji, bila hata ya kupata mafunzo yoyote au vifaa maalum, alipaisha ndege aliyoiunda kwa kutumia mabaki ya mkokoteni wa matairi mawili unaokokotwa na binadamu na pia kwa kutumia mabaki ya gari aina ya Toyota iliyokuwepo katika bustani yake.

Alexander Sodiqov pia alitoa mchango wake katika kuandaa makala hii.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.