Zambia Yapanga Bei ya Mahindi kwa Mara Nyingine, Yaikasirisha Benki ya Dunia

Makala haya ni sehemu ya habari zetu maalumu za Mahusiano na Usalama wa kimataifa

A giant Nshima pot

Sufuria kubwa la kupikia ugali wa Nshima, nchini Zambia 2008. Picha ya mwanablogu Mark Hemsworth (imetumiwa kwa ruhusa)

Nshima, aina ya ugali unaopikwa kwa unga wa mahindi, umewahi kuwa sababu ya migogoro ya kifamilia na kusababisha ghasia kadhaa zinazohusiana na chakula nchini Zambia katika nyakati tofauti. Hii ndiyo sababu serikali zilizowahi kutawala nchi ya Zambia zimekuwa zikiweka mkazo mkubwa kwenye kulima, kuvuna, kununua na kuuza mahindi kwa walaji.

Uzalishaji wa mahindi ni shughuli nyeti katika maeneo yanazalisha dhahabu kama Copperbelt pamoja na maeneo mengine muhimu kama mji mkuu, Lusaka, ambako idadi kubwa ya watu wanategemea sana mahindi. Kwa sehemu kubwa, mahindi yanaongoza mustakabali wa kisiasa katika nchi hii.

Mwezi Mei, Benki ya Dunia iitaka serikali ya Zambiakutokuingilia upangaji wa bei ya unga wa mahindi unaouzwa na wakulima kwa shirika la hifadhi ya chakula la nchi hiyo na wadau wengine katika sekta ya uchumi wa kilimo. Pamoja na mwito huo, Waziri wa Kilimo alitangaza kwamba mwaka huu, bei ya unga wa mahindi itakuwa K65,000 (sawa na takribani Tsh. 20,000) kwa gunia la kilo 50.

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Zambia, Malawi na Zimbabwe, Bw. Kundhavi Kadiresan aliukosoa uamuzi huo na kudai kwamba wakulima masikini wa Zambia wananyonywa kwa sababu baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wananunua mahindi kutoka kwa wakulima hao kwa ajili ya kuliuzia Shirika linaloendeshwa na serikali liitwalo Hifadhi ya Chakula kwa bei ya juu. Kadiresan pia alionyesha kwamba Benki ya Dunia inaguswa na ukweli kwamba si tu kuwa sera ya kilimo ya serikali inashindwa kuhakikisha uendelevu wa ukuaji wa sekta ya uchumi, lakini pia serikali haichukui hatua za kutosha kutengeneza ajira pamoja na kupunguza umasikini

Kadiseran angeweza kusamehewa. Sekta ya kilimo nchini Zambia inategemea sana mahindi, ukiachilia mbali mazao mengine na mifugo. Sehemu kubwa ya mahindi inalimwa na wakulima wadogo ambao wanakabiliwa na hali ya ukame wa mara kwa mara hata nyakati za majira ya mvua, ugavi wa mbolea usioaminika na wenye gharama kubwa, na matatizo ya usafiri kati ya mashamba yao na yaliko masoko ya mahindi.

Mwaka 1986, wa_Zambia wanaoishi kwenye majimbo ya Copperbelt na Lusaka waligoma kwa sababu bei ya mahindi ilikuwa imeongezeka mara dufu wakati kipato walichokuwa wanakipata kilibaki vile kilivyokuwa. Miaka minne baadae, ghasia zilizohusiana na bei ya mahindi ziliongezeka kiasi cha kusababisha jeshi kuingilia kati.

Akitangaza habari hizo za bei mpya ya unga mahindi, waziri wa kilimo na mifugo Emmanuel Chandaalisema:

Tumechukua uamuzi ili kulinda usalama wa chakula katika nchi na pia kuhakikisha kwamba wakulima wadogo hawakatishwi tamaa kuzalisha mazao katika miaka ijayo…kuhakikisha mahindi yanayolimwa Zambia yanakuwa na ushindani vya kutosha katika soko la kimataifa. Serikali itahakikisha gharama za uzalishaji zinapungua kupitia, pamoja na mikakati mingine, mafunzo ya huduma za ugavi wa kilimo na usafiri kwa ajili ya wafanyakazi wa mafunzo hayo kwa mtazamo wa kuongeza uzalishaji miongoni mwa wakulima wadogo.

Chenda pia aliweka wazi kwamba serikali ilikuwa inachukua hatua za kutayarisha mipango wa muda mrefu ywa kujenga maghala ili kuondoa tatizo la kupotea kwa chakula kingi chini ya Shirika la Hifadhi ya Chakula. Siku chache kabla ya tamko hilo la waziri, shirika la hifadhi ya chakula liliharibu kiasi kikubwa cha mahindi yaliyoharibika katika wilaya kadhaa za nchi hiyo.

Chenda alisema:

Ningependa kulijulisha taifa kwamba uharibifu wa vyakula kwenye shirika letu la hifadhi ya chakula kwa sehemu kubwa unatokana na vifaa duni vya kuhifadhia…Ili kukabiliana na changamoto hii, Serikali imeanza kutekeleza mipango ya kujenga vifaa vya kudumu vya kuhifadhia.

ISN logoMakala haya ni sehemu ya tafsiri ya ki-Hispania, ki-Arabu na ki-Faransa ambazo zilitolewa na Mtandao wa Usalama wa Kimataifa (ISN) kama sehemu ya ushirikiano wa kutafuta sauti za raia wa kawaida katika masuala ya mahusiano na usalama wa mataifa duniani. Tembelea blogu ya ISN ili kuona habari nyingine zinazofanana na hii.
Picha inayoonekana ya mahindi yanayolimwa Zambia imewekwa na Choconancy1 kwenye mtandao wa Flickr (CC BY-NC-SA 2.0).

2 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.