Ethiopia: Ardhi, Historia na Haki katika Eneo la Gambella

Blogu ya Maendeleo ya Kidunia inayoendeshwa na jarida la Uingereza la The Guardian inaendelea kuandika habari za kugawa ardhi baada ya kuwekwa wazi kwa taarifa kuu za umma zinazohusu mgawanyo wa ardhi mwezi Aprili.

Mojawapo ya nchi zilizoandikwa katika taarifa hiyo ni Ethiopia ambapo wanavijiji katika jimbo la Gambella wanalazimishwa kuhamia kwenye vijiji vilivyoandaliwa na serikali ili kuwapisha “wawekezaji” kutwaa ardhi yao. Gambella ni eneo masikini zaidi nchini Ethiopia.

Mwandishi wa gazeti la The Reporter Ethiopia la nchini humo, linalotoka mara mbili kwa juma, anasema kwamba serikali ya Ethiopia imeanza kutathmini ufanisi wa wawekezaji waliojipatia sehemu kubwa ya ardhi kwa lengo la kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo. Ingawa hiyo inaweza kuchukuliwa kama hatua muhimu kwa wanaharakati wanaopinga unyang’anyi wa ardhi, uamuzi wa serikali ya Ethiopia kutathimini ufanisi wa wawekezaji walionyakua ardhi umevuta macho ya vyombo vikuu vya habari vya kimataifa.

Baadhi ya sura kutoka kwenye kitabu kipya cha Fred Pearce, (Tafsiri isiyo rasmi) ‘Wanyang’anyi ardhi: mapinduzi yaliyofichika ya Afrika’, zinaonyesha kwamba unyang’anyi wa ardhi una madhara kwa mafukara hawa kuliko hata mabadiliko ya tabia nchi. Katika mahojiano, Fred Pearce anaonyesha kwamba watu masikini walikuwa wanahamishwa kutoka kwenye ardhi yao bila kuzingatia haki zao za kihistoria na kiutamaduni.

Target countries of land deals from the Land Matrix Project

Nchi zilizolengwa kwa ugawaji huo wa ardhi kutoka kwenye Mradi wa Land Matrix

Hata hivyo, afisa wa serikali ya Ethiopia anapingana na hoja hii:

Afisa kutoka Wizara ya Kilimo alipuuza ukosoaji huo kwamba ugawaji wa ardhi ‘umeleta athari hasi kwa jamii iliyokuwa ikiishi karibu na mashamba’, akidai kwamba ‘umakini wa pekee umewekwa kuufanya uwekezaji huu usiwe na madhara kwa jamii inayoishi karibu na mashamba hayo na hatua hii itaendelea kwa mtindo ulioimarika’.

Wanaharakati wa masuala ya ardhi wametengeneza hati ya malalamiko ya mtandaoni na wanafanya kampeni kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter. Hati hiyo ya malalamiko inayowalenga wanadiplomasia wa Marekani na Uingereza inasomeka kama ifuatavyo:

Ninaguswa sana na taarifa za uvunjifu wa makusudi unaoendelea wa haki za wenyeji wa kusini magharibi mwa Ethiopia. Mpango wa Serikali wa “kuunda vijiji vipya” unawaondoa kwa nguvu wenyeji wasiopungua 200,000 kutoka kwenye ardhi yao ya asili katika maeneo ya Gambella na kuwahamishia kwenye vijiji vilivyojengwa na serikali. Ingawa serikali imewaahidi kupatikana kwa ajira, elimu, na huduma za afya katika vijiji hivi. Watafiti wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (Human Rights Watch) hawajapata ushahidi au wamepata ushahidi mdogo tu wa kuwapo kwa huduma hizi. Badala yake, watu waliohamishwa wanaishi kwa hofu ya kukumbwa na njaa kwa kuwa sasa hivi hawana mashamba tena, mapori na mito vyote viko mbali nao. Wale waliopaza sauti zao dhidi ya unyanyasaji wa aina hii wameendelea kukamatwa na kuwekwa kizuizini, wanateswa, wanabakwa na vinginevyo kutishwa na vikosi vya kijeshi vya serikali. Wale wanaojaribu kurudi kwenye ardhi zao za asili wanakuta tayari serikali imeshaigawa ardhi hiyo kwa wawekezaji wa kigeni ambao kwa haraka haraka wanasafisha maeneo hayo kwa kuondoa mapori, mashamba yaliyokuwepo na vichaka ili kupata nafasi ya kulima mazao ya kibiashara kama vile ufuta, chai, viungo, mchele, na sukari, ambapo mazao mengi yanakusudiwa kuuzwa nje ya nchi. Matokeo yake mazingira yanaharibiwa na kuathiri hifadhi ya chakula kwa wenyeji.

Kundi la Facebook liitwalo Zuia Unyang’anyi wa ardhi Gambelle, Ethiopia linaandika:

Nafasi kwa ajili ya jamii ya Kimataifa kupaza sauti yake dhidi ya uvunjifu wa haki za binadamu na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na unyang’anyi wa ardhi unaoendelea eneo la Gambella nchini Ethiopia.

Unyang’anyi wa ardhi ni suala tete linalohusu umilikishaji wa maeneo makubwa ya ardhi; ununuzi au kukodisha maeneo makubwa ya ardhi katika nchi zinazoendelea unaofanywa na makampuni ya nyumbani au ya kimataifa, serikali au watu binafsi.

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.