Zambia: Rais Awakera Raia Waishio Nje

Rais wa Zambia, Michael Sata amewakasirisha raia wa Zambia waishio nje ya nchi hiyo kwa kuwakejeli alipokuwa katika ziara ya siku tatu katika nchi jirani ya Botswana na pia kwa kufifisha matumaini yao ya kuingiza suala la uraia wa nchi mbili, linalogonga mijadala mingi, katika katiba mpya ya nchi hiyo inayoendelea kuandikwa.

Rais Sata, anayejulikana kwa kuzungumza kwa jazba na kutokuzingatia protokali, aliripotiwa na tovuti ya habari za kiraia,Zambian Watchdog, kuwa na fursa ya kuzungumza na kupokea maswali kutoka kwa wa-Zambia waishio nchini Botswana, ambapo anadaiwa kusema kwamba Rupia Banda, (Rais wa zamani wa nchi hiyo, ambaye alimshinda katika uchaguzi wa mwaka 2011) alitaka kuiingiza hoja hiyo ya uraia wa nchi mbili katika katiba kwa sababu tu alitokea eneo la Gwanda nchini Zimbambwe.

A changed Sata

Rais Sata, kabla na baada ya kuingia madarakani. Picha kwa hisani ya: Kikundi cha Facebook kiitwacho Zambian People's Parliament

Sehemu ya kipindi cha maswali na majibu kilikuwa hivi:

Swali – hoja ya Uraia wa nchi mbili imefikia wapi?

Sata: Umetokea mji gani? Monze [mojawapo ya miji ya Zambia]? Unataka ufahamike kama mkaazi wa Monze na Namwala [mojawapo ya miji nchini Zambia]? Kwa sababu RB [Rupiah Banda] alikuwa anatoka Gwanda nchini Zaimbabwe ndio maana alitaka Uraia wa nchi mbili.

Swali: ni vigumu kwa sisi tunaoishi nje ya nchi kupata ardhi kule nyumbani, Serikali inalishughulikiaje suala hili?

Sata: Unashughulika na nini hapa Botswana?

Jibu: Ninafundisha!
Sata: Rudi Zambia kafundishe ndugu zako kisha utapata ardhi

Swali: Mhe Rais, hukuwahi kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu wilaya za Ithezhi tezhi na Chiryndu [wilaya hizi mbili zinahamishwa kutoka Jimbo la Kusini kwenda Majimbo ya Kati na Lusaka]

Sata: Ulipata ushauri wa nani kabla hujaja Botswana?

Majumuisho-Rais Sata

Nyote mlioko hapa na maswali yenu yasiyo na msingi mmenisikitisha sana na kwa kweli nimefadhaishwa, hivi hamna aibu? Mliikimbia nchi yenu Zambia mkidhani tusingewapata na sasa leo nimewapata. Mmekuwa wakimbizi nchini humu (Botswana) mkinyonywa na serikali ya Botswana. Mliondoka Zambia kuja kufanya kazi hapa kwa sababu tu ya Kwacha moja ya ziada?

Kuhusu suala la walimu na madaktari wanaofanya kazi Botswana ambapo wengi walikimbilia hapa kwenye miaka ya 1980 mwishoni mpaka miaka ya 2000 mwanzoni, Rais Sata alisema:

Mnajishughulisha sana kuwaelimisha wa-Tswana huku mkiwaacha ndugu zenu wenyewe nchini Zambia wakikosa elimu na mnajisikia fahari? Nyote mlisomeshwa na wazazi wenu ambao hata hawakumaliza darasa la saba na walijitahidi kuwasomesha na mkawakimbia?

Madaktari

Ndugu zenu wanakufa nchini Zambia na nyie mnahangaika kuokoa maisha ya wa-Tswana?

Wahasibu

Botswana ina maduka matano pekee na eti mnajiita wahasibu wakati migodi ya Dhahabu inapohitaji ushauri wa kitaalamu inawaita wa-Afrika Kusini na sio nyie wa-Zambia, bado mnafanya nini hapa?

Majibu hayo ya Rais Sata pamoja na tamko la awali alilokuwa amelitoa kwenye dhifa nyingine katika ziara yake hiyo ya Botswana, ilitofautina na ile ya waziri wake wa Mambo ya Kigeni Given Lubinda ambaye aliwaambia wa-Zambia wafanyao kazi zao nchini humo kwamba sera ya Serikali ya chama cha PF haikuwa kuwarudisha nchini Zambia wananchi wake waishio nje ya nchi.

Akiitikia maoni hayo ya Sata, John, msomaji wa tovuti ya Zambian Watchdog, alisema:

Hotuba ya rais ilikuwa ya kibinafsi sana, yenye kuongozwa na hisia na isiyoonyesha weledi. Inatia aibu kwa Afrika kwa sababu madaraka yanazidi kukabidhiwa mikononi mwa watu wawezao kuwazidi wenzao kwa kupiga kelele kupitia sanduku la kura; badala ya viongozi wenye sera zinazoeleweka juu ya namna ya kuzitawala na kuendesha nchi zao. Hivi kiwango cha elimu ya MHESHIMIWA ni kipi?

Imani kwamba watu wenye elimu (au hata wasiosoma) wanapaswa kuishi katika nchi walizozaliwa imepitwa na wakati. Hiyo ilikuwa miaka ya 1970 wakati ambapo Afrika ililalamikia sana suala la “wataalamu kukimbilia nje”. Je, Rais anatambua kitu kiitwacho “masurufu yanayotumwa na wananchi waishio nje ya nchi” au basi “kufaidika na wataalamu wa nchi nyingine”? Anajua kwamba pesa wanazotuma raia waishio nje ya nchi hivi sasa zinaelekezwa katika kujenga barabara, viwanja vya ndege, miji ya kiteknolojia nchini Naijeria, Kenya na sasa Jamhuri ya Sudani Kusini?

Nkoya Nationalist, mmoja wapo wa wachache waliokubaliana na Rais Sata:

Rais yu sahihi, Zambia ina idadi ndogo ya watu ambao kati yao ni asilimia ndogo sana wana utaalamu katika tasnia na fani mbalimbali. Kati ya hawa wataalamu, karibu robo tatu wako nje ya nchi wakitumikia mataifa mengine.

Nani ataliendeleza taifa kama wataalamu wetu wote wako nje wakifanya kazi kwa ajili ya mataifa mengine?

Kwa nini kila mtu alalamikie kiwango hafifu cha utendaji wa mawaziri na maafisa wa serikali wakati nyie wataalamu hampatikani mfikiriwe kwa nafasi na majukumu hayo hayo?

Hivi mnajua kwamba Zambia huenda ingeweza kuwa moja ya nchi bora zaidi duniani kama wataalamu wetu wangeipenda zaidi nchi yao kwa kurudi nyumbani na kuchangia katika harakati za kuiendeleza?

Msomaji ajiitaye An anguished Peace Maker (Mpatanishi mwenye hasira) aliandika:

Wale wenye mashaka na habari hii wafikiri mara mbili. Hivi mnamaanisha kabisa kwamba hamumfahamu Rais wetu? Rais wetu anahitaji kudhibitiwa anachosema saa zote na siku zote kwa sababu vinginevyo ataendelea kutukera. Mheshimiwa anahitaji mwongozo makini kwa chochote. Nguvu anazoonekana kuwa nazo lazima zielekezwe kwenye mambo yanayoweza kuleta faida na kwa kadri inavyowezekana jaribuni kutokumweka kwenye mazingira kama hayo na kama inalazimu basi fanyeni hivyo mbali na kamera kumsaidia mpaka sasa, nadhani kinga ni bora kuliko tiba! Tayari tupo kwenye tatizo na hakuna sababu ya kumtetea zaidi ya kumsaidia! Hatima ya haya yote haitakuwa aibu yake yeye mwenyewe pekee bali ya kila m-Zambia bila kujali Chama chake.

Tuna kazi ya kufanya!! (Hali hii) inakuwa mithili ya mwiba mwilini mwangu, nikikumbuka alichosema Mt. Paulo. Tunachoweza kufanya ni kidogo sana lakini tuilee hivyo hivyo (hali hii) mpaka mwaka 2016 ambapo, kwa heshima zote, lazima tupange mbinu muafaka ya yeye kuondoka. Hatuwezi kuendelea namna hii. Ni zimwi lenye maumivu na lenye kuogofya!

Kwenye kikundi cha Facebook, siku 90 (Serikali yasitahili pongezi/yakosolewa baada ya siku 90), Maria Kapambwe Kasolo, alitoa sababu kwa nini wa-Zambia waliondoka nchini humo kwa makundi makubwa:

Mnajua kwa nini wataalamu wanakimbilia Botswana – maslahi bora! Ninawajua watu kadha waliofanikiwa wao wenyewe na familia zao hali kadhalika. Kama wangebaki nyumbani wasingepiga hatua zozote za maana. Serikali ya Zambia yapaswa kuboresha mazingira ya kazi na watu hawataenda kutafuta mahali pengine kama nyumbani watapata maslahi bora. Baadhi yenu mnasema Rais alikuwa sahihi kwa majibu ya namna ile –- Mimi nasema rais anahitaji kutumia njia za kidiplomasia kwa mazingira yoyote –lazima aulize kwa nini waliondoka nchini na sio kuwafokea – haikuwa sahihi kabisa!

Akimjibu Maria Kapambwe Kasolo, Arnold Chinyemba aliandika:

Anafikiri kila m-Zambia ni mchuuzi. Kwa hiyo kwake kuruhusu “wamachinga” ni kuwawezesha wa-Zambia. EE MWENYEZI MUNGU ISAIDIE NCHI HII.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.