Naijeria: Gumzo la Mtandaoni Kuhusu Shirika la Ndege la Dominion

Anga la mtandao nchini Naijeria liliwaka moto hivi karibuni kufuatia kuzinduliwa kwa Shirika jipya la Dominion.. Kwa nini basi kuingia tu kwa jina jipya katika kibiashara ya safari za anga kusababishe majadiliano makali namna hii? Imetokea kuwa shirika hili la ndege si “la kawaida”: linasemekana kumilikiwa na Mtumishi wa injili ya “mafanikio, ” Askofu David Oyedepo:

(David Oyedepo) ni Mwandishi wa vitabu vya Kikristo nchini Naijeria, Mhubiri, mwasisi na Askofu Mkazi wa Kanisa liitwalo “Living Faith Church World Wide” (tafsiri isiyo rasmi: Kanisa la Imani Hai Ulimwenguni) linalojulikana pia kama Winners Chapel (Kanisa la Washindi) na lililoanzisha makanisa yaliyoenea duniani kote yajulikanayo kama Winners Chapel International, yenye makao yake makuu kwenye Jimbo la Ogun , nchini Naijeria. Vile vile (Adeyepo) ni mchungaji kiongozi wa kanisa liitwalo Faith Tabernacle (Kanisa la Imani) linalomiliki jengo kubwa lenye uwezo wa kubeba watu waliokaa wapatao 50,000 kwa mara moja, likidhaniwa kuwa kubwa kuliko makanisa yote duniani kwa mujibu wa kitabu cha Kumbukumbu cha Guinesss. Mtandao wa makanisa ya “Winners Chapel” umeenea katika majiji zaidi 300 katika majimbo yote ya Naijeria, pia katika majiji zaidi ya 63 katika Mataifa ya Afrika, Dubai, Uingereza na Marekani.

Bishop David Oyedepo (Courtsey: yemojanews.com)

Askofu David Oyedepo (Picha kwa hisani ya: yemojanews.com)

Jarida la Forbes linamtaja Oyedepo kama mchungaji tajiri zaidi nchini Naijeria:

Inakadiriwa kuwa ana mali zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 150 (zaidi ya Tsh. Bilioni 240). David Oyedepo ni mhubiri mkwasi zaidi nchini Naijeria…Oyedepo anamiliki ndege binafsi nne na majumba katika majiji ya London na Marekani. Anamiliki pia Kampuni ya Uchapishaji iitwayo Dominion Publishing House, inayochapisha vitabu vyake vyote (ambavyo vimejikita zaidi kwenye mafanikio). Alianzisha na anamiliki Chuo Kikuu cha Covenant, mmoja ya taasisi za elimu ya juu zinazoongoza nchini Naijeria, na shule ya sekondari ya kitajiri ya Faith Academy.

Sahara Reporters linadai kwamba kuanzishwa kwa shirika la ndege la Dominion kumetokana na kupanda kwa gharama za kuendesha ndege binafsi za Oyedepo:

Kupanda kwa gharama za uendeshaji wa ndege nne binafsi kumemlazimu mchungaji huyo wa ki-Naijeria anayependa kuvaa nguo za gharama kubwa, Askofu David Oyedepo, kuanzisha shirika la ndege la kibiashara ambalo litatumia ndege hizo nne ambazo mpaka sasa zinatimika kama sehemu ya usafiri wake binafsi. Mwaka uliopita, zilipopanda gharama za wahudumu, bei ya mafuta na gharama za kutua ndege, Askofu Oyedepo alitaka kuuza ndege mbili. Lakini wanunuzi walipokosekana, aligeukia mpango mbadala: kuanzisha shirika la ndege na kuziingiza ndege zake katika matumizi ya kibiashara.

Miitikio katika majukwaa mengi ya mtandaoni ilitofautiana.

Baadhi ya kejeli na ukosoaji ulioandikwa kwenye mtandao wa twita zilikuwa kama ifuatavyo:

@dangeldiva: Ndio kusema rubani atalazimika kuomba kabla ya kurusha ndege? DominionAir

@nzesylva: Mara tu rubani atakapotoa ishara ya “funga mkanda wako”, itabidi abiria wote wafunge macho yao kwa ajili ya kusifu na kuabudu #DominionAir

@FedUpNigerian: #DominionAirInflightEntertainment (BurudaniNdaniyaNdegezaDominion) Hairuhusiwi kupiga makofi baada ya kutua uwanjani, tunaweza tu kushangilia halleluja! #dominionair

@Ms_Mustapha: Badala ya Majarida ya ndani ya ndege kutakuwa na biblia #dominionair

@sheikhofeffizy: #dominionair…hakuna simu ndani ya ndege na inabeba watakatifu peke yao…

@kj_hova: Dini hazipaswi kutozwa kodi na serikali. Hata hivyo, biashara zake zinazotengeneza faida lazima zihusike na utaratibu wa kodi za makampuni na mapato nk #DominionAir

@BuzorIbusaBoy: Mlilalamika juu ya ndege yake, sasa ana shirika la ndege, hivi hivyo haiwaonyeshi kwamba hajali (mnasema nini)?…bado mnataka kulalamika? #DominionAir

@ChikaUwazie: sasa naona kwa nini wa-Naijeria wanajiua ili wawe baba wachungaji #dominionair

Watumia twita waliomwunga mkono:

@OgbeniBen: Kwa wale wanaokosoa shirika la ndege la #DominionAir “ ♏v̶̲̥̅ Watu (wangu) wanapotea kwa kukosa maarifa” ni hatua nzuri kwetu wanafamilia wa (kanisa la)Winners

@drphilip2010: Ninasikia sauti ya wivu! #DominionAir #BishopOyedepo.

@lutoluh: Kama Oyedepo angeweka fedha zake benki au angezitumia kujengea “hekalu” la kuishi kijijini kwake…hakuna mmoja wenu angepata cha kutia chumvi sasa hivi!#dominionAir

Kathleen Ndongmo i anabainisha “Mambo 7 ya kuzingatia kabla ya kumkosoa Askofu Oyedepo”:

7- Mchungaji wa “asiye na kazi nyingine isipokuwa kuchunga kanisa” haruhusu kufanya biashara? Anatenda “jinai” akifanya biashara? Mwanasiasa asiye na kazi nyingine anaweza kufanya “dili” na bado msione kama kafanya kosa?

6- Chagua kimoja: Mtu anayefanya “dili” za kuiba hazina yako kwa ajili ya biashara yake au mtu anayetumia michango yenu ya hiari kwa ajili ya biashara. Tunaongozwa na hisia?

5- Toza kodi “kanisa” kama serikali itaona inafaa. Hilo halina tatizo kabisa, Wote mnajua, “kanisa” litalipa. Bila tabu.

4- Nimekulia katika kanisa Katoliki. Ambapo shule za “seminari”, hospitali za “misheni” na kadhalika zilikuwa faiada kwa jamii.

3- Inakuwaje kosa pekee la mtu kuanzisha biashara liwe ni kwa sababu eti anaongoza huduma ya Kikristo?

2- Kama mtu aukanaye uwapo wa Mungu anaweza kuanzisha biashara [kama shirika la ndege] inayowatumikia [wateja] kutakuwa na kelele? Je, imani itaharibika?

1. Asiwaju Bola Ahmed Tinubu (anadaiwa) kuanzisha Taifa la Kwanza, na hatusikii kelele. Kwa nini ziwepo kelele Oyedepo anapoanzisha shirika la ndege la Dominion?

Phantom of Jargon anaonyesha mapungufu katika hoja za Ndongmo:

7. “Dili” za kisiasa NI kosa, Ukristo si biashara, SHIRIKA LA NDEGE la Dominion ni KITU KIKUBWA! Kama Bishop Oyedepo anataka kuwa kama Donald Trump, basi aachane na huduma.
6. Kimsingi unataka kumharibia Askofu Oyedepo: “…anatumia michango yenu ya hiari kwa ajili ya biashara” Kama anawakilisha u-Kristo kwa dhati, najua “michango hii ya hiari” siyo mtaji kwa ajili ya ujasiria mali, ni kwa ajili ya kuwasaidia wenye shida na kusaidia uinjilisti.

5. Kathleen Ndongmo- kuna sababu inayoeleza kwa nini makanisa hayalipi kodi, kwamba hayategemewi kuendeshwa kama taasisi zinazotengeneza faida! Yapo makanisa ambayo hayawezi kulipa…bila shaka.

4. Heko kwa makanisa ya kweli ya Kikatoliki lakini vile vilikuwa “vivutio vya umisheni” (lakini) Shirika la ndege la Dominion ni la kibiashara, ninapata tabu kuona namna gani linaweza kuwasaidia moja kwa moja wale wanaohitaji “msaada” katika jamii. Ni kama mtu anayenzisha casino na kudai “Ninajaribu kuwasaidia watu kuwa matajiri”

3. Hoja yako ya ’7′ inapingana na hii…

Hoja ya 1&2 Amkanaye Mungu au mwanasiasa atakuwa anasababisha mgongano na kule kutokuwa kwake na imani

Askofu Oyedepo hajatoa maoni kuhusu umiliki wa Shirika hilo la ndege. Ni kwa sababu hiyo, Jarida la mtandaoni la Contra Culture linadhani kwamba zogo lote hilo kuhusu Shirika hilo la Ndege halina sababu.

Kwa hiyo kuna tetesi mtandoni kwamba Askofu Oyedepo yuko katika mchakato wa kuanzisha kampuni ya ndege iitwayo Shirika la Ndege la Dominion. Ni tetesi kwa sababu hakuna mtu yeyote kutoka kanisa hilo la Winner alitoa majibu yoyote…

1 maoni

  • BAHATI WILSON SEMWALI

    Kwa kweli tunaona tulivyo nyuma kwa kila kitu.tajiri namba moja africa mnigeria,mwanamke tajiri wa pili duniani mnigeria.wanawake wacheza soka,wanaume.wasomi.wakristo,waislam wa nigeria wametuzidi! tunalaana gani hapa tanzania? changamoto,mama rwakatare,mch.katunzi,mch gamanya,askofu kakobe,masheikh kina shekh simba,kipozeo mpo hapo?wenzenu wana ma university,madege,mahospitali.hapa majungu tu.ooh yesu si mungu! amkeni mlio lala.

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.