Wakati wananchi wa Ghana wakijiandaa kwa uchaguzi wa Rais na wabunge utakaofanyika tarehe 7 Desemba 2012, jumuiya ya wanablogu ya nchi hiyo iitwayo “BloggingGhana” imeanzisha mradi wa vyombo vya habari vya kiraia ambao unalenga kuwaelimisha wadau namna ya kutumia zana za uandishi wa kiraia kwa ajili ya uangalizi wa uchaguzi na namna ya kuhabarisha yatakayotokea wakati wa uchaguzi.
Jumuiya hiyo ya “GhanaBlogging” ni kikundi cha wanablogu wa ndani na nje ya Ghana wanaoblogu habari za Ghana.
Mwandishi wa habari za matangazo ya redio, mwandishi na mwanablogu Nana Sarpong anaandika kuhusu kuzinduliwa kwa mradi huo:
“Ghana Decides” [Taasiri yake Ghana Yaamua] –Mradi wa Uchaguzi wa Ghana wa 2012 ulioandaliwa na BloGh(Jumuiya Wanablogu wa Ghana) umezinduliwa leo kwenye Hoteli ya Windy, mjini Winneba. Mradi huu ni mpango wa Jumuiya hiyo ya wanablogu unaokusudia kuzielimisha AZISE (Asasi Zisizo za ki-Serikali), Mashirika ya Kiraia, wanafunzi (hususani wapiga kura wapya), makundi ya kisiasa na umma wa wananchi wa Ghana kwa ujumla kuhusu umuhimu na faida ya kutumia zana za uandishi wa kiraia kwenye uchaguzi wa Ghana. Miradi hiyo ina lengo la kuyashirikisha makundi hayo na watu mmoja moja, kuwafunza namna ya kutumia zana hizi pamoja na kuwapa jukwaa linaloaminika kwa ajili ya ufuatiliaji wa uchaguzi wa nchi hiyo.
Nana anaendelea::
Kwa kuwa miradi mingi ya kibunifu inayofanana na “Ghana Decides” kwa kawaida hujikita kwenye makao makuu ya nchi hiyo, timu ya mradi huo ilionelea vyema iuzindue mradi huo nje ya jiji la Accra. Uzinduzi huo uliokuwa na kauli mbiu ya”Kuhamasisha Ushiriki Ulioerevuka wa Vijana Katika Uchaguzi wa 2012” ulihudhuriwa na washiriki kutoka Shule za Sekondari ndani ya mji wa Winneba, umoja wa watu wenye ulemavu wa mji huo, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ualimu, Winneba, AZISE kama Plan Ghana na umma kwa ujumla.
Uzinduzi huo ni mwanzo wa kampeni rasmi ya kutangaza mfululizo wa shughuli za “Ghana Decides” mtandaoni na nje ya mtandao ikiwa ni pamoja na kampeni ya niMejiandikisha inayokusudia kuwahamasisha wapiga kura vijana kujitokeza kwa idadi kubwa, na kujiandikisha aidha na kujipiga picha za video au za mnato zitakakazoonyesha wakishiriki zoezi hilo au baada ya kujiandikisha. Hivi sasa, alama ya #iRegistered inatawala mijadala ya mtandao wa twita.
Video ifuatayo kutoka chaneli ya mtandao wa You Tube ya “Ghana Decides” inaonyesha vipande kadhaa vya zoezi hilo linaloendelea la kuandikisha wapiga kura nchini Ghana.
“Ghana Decides” wanaeleza zaidi kuhusu mpango wa #iregistered:
Miongoni mwa shughuli za “Ghana Decides” ni kampeni ya “#iRegistered” (niMejiandikisha) kuwahimiza wa-Ghana kujiandikisha wakati Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo ikiwa imeanza kuendesha zoezi hilo la kuandikisha wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya alama za vinasaba.
#iRegistered katika hatua nne rahisi;
1.“Ghana Decides” imetoa taarifa kuhusu zoezi la uandikishaji wapiga kwa kutumia alama za vinasaba katika tovuti yake (http://ghanadecides.com). Tovuti ya Serikali ya Ghana (http:///gahan.go.gh) pia inacho kipeperushi cha taarifa kuhusu zoezi hilo la kuandikisha wapiga kura. Kila raia wa Ghana anahimizwa kukisoma, kuhabarishwa na kusambaza taarifa hizi kwa ndugu, jamaa na marafiki katika jumuiya zao.
2. Tuma ujumbe kupitia mtandao wa twitter, facebook au Google+ ukiwaambia rafiki zako na ulimwengu kuhusu zoezi la kuandikishwa na haja ya kujiandikisha kwa kutumia alama za #iRegistered na #GhanaDecides.
Mpango wa “Ghana Decides” uko katika mitandao ya kijamii kama YouTube, Twitter, Flickr na Facebook.
Ushindani mkubwa katika uchaguzi ujao wa Desemba 2012 utakuwa kati ya vyama viwili vikuu ya siasa nchini Ghana, chama tawala cha NDC (National Democratic Congress) na chama kikuu cha upinzani cha NPP (New Patriotic Party).