Zambia: Ban Ki-Moon atoa wito kwa taifa kuheshimu haki za mashoga

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliitembelea Zambia hivi karibuni, akalihutubia bunge, akaweza pia kukutana wanasiasa maarufu kati yao akiwa ni Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Kenneth Kaunda na kutembelea Maporoko ya Viktoria, yaliyoko katika mji wa kusini wa Livingstone, ambayo ni sehemu muhimu kabisa kwa utalii nchini humo. Hakuna katika haya yaliyogonga vichwa vya habari kama mwito wake kwa taifa hili kuheshimu haki za mashoga.

Lusaka Timesliliripoti:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alisema watu wa historia mbalimbali za kiutamaduni wanahitaji kuthaminiwa utu wao na heshima. Bw. Ban aliwatolea mfano watu wafanyao mapenzi ya jinsia moja, wasagaji na mashoga kuwa ni watu ambao haki zao zinahitaji kutambuliwa na kuheshimiwa na watu wote.

The UN Secretary-General Ban Ki-moon speaking in Lusaka, Zambia. Photo courtesy of zambianwatchdog.com.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akizungumza mjini Lusaka, Zambia. Picha ya zambianwatchdog.com

Katika hotuba yake kwa Bunge la Zambia, Bw. Ban alisema:

Sasa mmeingia kwenye agenda ya mabadiliko – mchakato wa kutengeneza jamii mpya ya watu wamoja–yakiongozwa na Katiba ambayo itakuwa msingi wa maendeleo ya Zambia, Katiba ambayo inaweza kusimama na kudumu muda mrefu. Hii inaipa Zambia nafasi ya kuongoza kwa mara nyingine tena kwa kuheshimu haki za binadamu kwa viwango vya juu kabisa na kuwalinda watu wote – pasipo kujali rangi, dini, jinsia, mihemuko ya kimapenzi au ulemavu.

Matamshi hayo yalirejesha upya mjadala wa suala la ushoga  ambalo ndilo lililokaribia kabisa kukifanya chama tawala enzi hizo MMD kumwangamiza kisiasa kiongozi wa upinzani wakati huo, sasa Rais wa nchi Michael Sata, wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi wa mwezi Septemba ambao ulishuhudia akimbwaga rais wa zamani Rupiah Banda.

Wananchi wa Zambia wanaotumiao mtandao katika tovuti mbalimbali za kijamii walionyesha kupinga kauli hiyo ya Bw. Ban, wengi wao wakinukuu tamko linaloitambulisha Zambia kuwa “Taifa la Kikristo”, ambalo linalindwa na katiba ya nchi hiyo.
Akitoa maoni yake baada ya kusoma habari hiyo ya Lusaka Times (iliyonukuliwa hapo juu), Mambala aliandika:

hehehe!!!!! Bw. Ban, tulitegemea kusikia hayo kutoka kwako. Na kwa hakika hiyo ndiyo ilikuwa agenda yako kuu…kuharakisha na kukuza mwanzo wa mashoga na wasagaji. Sikia, Zambia ni taifa huru, hatuhitaji kuelekezwa namna ya kuishi. Tunajua hawa mashoga na wasagaji wamekuwa siku zote sehemu ya jamii yetu. Wanafanya vitendo vyao kwa siri na hiyo haitusumbui. Lakini kama watathubutu kuanza kujitangaza hadharani ili kuendeleza uovu wao, tutawashughulikia bila huruma!!!!

A map showing penalties targeting gays and lesbians in Africa. Image source: ilga.org

Ramani ikionyesha adhabu zilizokusudiwa kwa mashoga na wasagaji nchini AFrika. Chanzo cha picha: ilga.org

Citizen aliandika:

Tafadhali Bw. Katibu Mkuu, sisi kama wa-Zambia tumeridhia kuwa tu Taifa la Kikristo, ni katiba yetu na hiyo inakuwa haki yetu. Kuwa hivyo, maana yake ni kuheshimu watu wote kwa kuwa ni sura ya uumbaji wa Mungu –ikijumuisha wahalifu, mashoga, wasagaji, waongo, makahaba na wanaofanana na hao, wakati huohuo tukihukumu vitendo vyao hivyo vya dhambi, ili wageuke. Mhe. Katibu Mkuu, tunajua unatutaka tufuate mataifa mengine kwa kutokuchukulia ushoga kuwa jinai. Hilo tutalikataa. Kamwe hatutageuza sheria kuvibariki vitendo kama hivyo. Ni wakati sasa kwa mataifa hayo kuiga kwetu kwa sababu hilo ni jambo lenye maana kulifanya.

Moja ya sauti chache zenye mtazamo tofauti na huo, Observer, anaandika:

Mhe Ban anazungumzia haki za MSINGI. Hazungumzii ndoa za mashoga au kitu kama hicho. Hivi mmesoma habari hii kabla ya kuandika maoni? Haki za msingi kama haki ya kupatiwa maji na elimu. Anasema watu hawa wapaswa kuruhusiwa kuishi maisha huru dhidi ya hatari ya kimwili na kufurahia haki hizi za msingi pasipo ubaguzi. Sioni chochote kibaya kwa hilo. Hawa ni watu pia. Makanisa na familia zetu lazima yafanye bidii kuhakikisha kuwa vijana hawajitumbukizi kwenye ushoga na tabia nyingine chafu. Serikali haiwezi kubebeshwa jukumu hilo la kuratibu maisha ya mtu mmojamoja. Ni faida kwa nchi yetu kutembelewa na Mhe Ban.

Kwenye kundi la Zambian Facebook, , siku 90 (Serikali imepatia/imekosea kwa kila baada ya siku 90) , Sidique Abdullah Gondwe Geloo alitofautisha kati ya dhambi na uhalifu::

USHOGA NI DHAMBI, SI UHALIFU. UZINZI NI DHAMBI NA SIO UHALIFU. Je, mwanaume asiyeoa atapelekwa gerezani kwa kufanya mapenzi na mwanamke asiyeolewa? Hapana. Wametenda dhambi lakini hawakutenda kosa la jinai, ni kufanya uamuzi. Je, mashoga waende jela kwa kutoka pamoja?…Ni DHAMBI mbaya tena mbaya sana lakini si uhalifu…Wana haki ya kutokupigwa mawe, kuuawa au kusumbuliwa, lakini wasiwe na haki ya kuoana, kuonyesha mihemuko yao ya kimapenzi hadharani kwa sababu sisi ni NCHI INAYOJIVUNIA CHUKI DHIDI YA VITENDO VYA MAPENZI YA JINSIA MOJA…kwa hiyo mtu anaposema mashoga wana haki zao, hiyo isiwaogopeshe ili mradi wanauficha ushoga wao majumbani kwao

Kwenye Twita, ujumbe mmoja ulimzungmzia Ban Ki-Moon ukisema:

@chikwe1: Ban Ki Moon kama kupinga ushoga #Homosexuality kunanifanya #mshamba basi ni afadhali #Niishi na #Kufanikiwa mshamba kuliko kinyume chake. Kaa mbali na #Zambia

Wakati mjadala kuhusu ushoga ukishika kasi barani Afrika, Liberia na Uganda vimetunga muswada wa kupinga ushoga hivi karibuni ili kuufanya ushoga uhukumiwe kwa adhabu ya kifo. Ushoga umezuiwa kisheria katika nchi 38 za ki-Afrika na unaweza kuhukumiwa kifo nchini Mauritania, Sudan na kasikazini mwa Naijeria.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.