- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Zambia: Kiongozi wa Upinzani Awa wa Kwanza Kulihutubia Bunge la Facebook

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Zambia, Siasa, Teknolojia, Uandishi wa Habari za Kiraia

Rais waChama cha upinzani [1] cha NAREP (National Restoration Party) Elias Chipimo Jr [2]. amekuwa mwanasiasa wa kwanza katika nchi hiyo “kulihutubia” bunge la Facebook nchini Zambia [3] linaloaminika kuwa na wanachama 1,318 baada ya kuruhusiwa na “Spika” kutuma ujumbe wake wa mwisho wa mwaka.

Mhe Spika [4] aliweka ujumbe ufuatao kabla hajaweka hotuba nzima ya Chipimo:

TANGAZO MUHIMU

Waheshimiwa wajumbe. Naomba tumkaribishe Mhe. Elias Chipimo, Rais wa (chama cha) NAREP ili aweze kulihutubia bunge hili rasmi kwa kutoa salaam za mwisho wa mwaka kutoka chama cha NAREP. Kama kawaida, bunge litaendelea kwa kuijadili hotuba yake.

Mara tu tutakapowapata Rais wa UPND, Mhe. HaKainde Hichilema, na Rais wa chama cha Republican, Mhe Michael C. Sata, tutawaruhusu na wao walihutubie bunge.
Rais Chipimo, ni heshima kubwa kuwa nawe Bungeni. Sasa unaweza kulihutubia Bunge hili tukufu.

Sehemu ya posti ya [5] Chipimo inasomeka hivi:

 

[6]

Rais wa chama cha NAREP (National Restoration Party Elias Chipimo. Haki miliki ya Picha ni ukurasa wa Facebook wa Elias Chipimo.

Salaam za mwisho wa mwaka kutoka chama cha NAREP.

Tukitafakari zaidi ya mwaka 2011: Kile ambacho serikali ya PF inaweza kuanza kufanya katika siku 90 zijazo wakiwa madarakani. Zambia inakabiliwa na changamoto nyingi kuanzia huduma mbovu za afya, miundo mbinu iliyotelekezwa siku nyingi na kwa kweli isiyofaaa, kutokupatikana kwa elimu yenye ubora na uchumi ambao bado hauwezi kuwapatia wananchi walio wengi mahitaji ya kimaendeleo pamoja na kuimarika kwake katika miaka michache iliyopita. Kupambana na matatizo haya hapana shaka tunatakiwa kuwa na malengo ya muda mrefu, nguvu na dira. Kwa hivyo kuna, masuala matatu makubwa yanayohitaji hatua zilizo bayana, zinazohitaji kujitoa na za haraka. 1) ukosefu wa ajira; 2) ufisadi; na 3) madaraka makubwa ya rais na wakubwa wa serikalini. Ingawa vita dhidi ya ufisadi imepewa nguvu na serikali ya PF, yamekuwepo malalamiko ya kushindwa kupata kanuni ya kukabili kila kimoja katika masuala haya kwa namna iliyo endelevu […] Kwa jinsi nyakati hizi katika ulimwengu wote zinavyoonyesha, mwaka 2011 umekuwa wa Majira ya Kuchipua ya Urabuni –hali hiyo ya uelewa wa kidemokrasia ambao umeonekana kuanzia ghafla katika mitaa ya mji wa Tunis na kuweza kusambaa kama virusi kwenda Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati. Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, na kwa hakika Zambia, haikuachwa bila madhara kufuatia matukio haya. Hata kama wazo hili linaweza kuonekana kuwa mbali sana, madai yaliyochochea mapinduzi ya kidemokrasia nchini Tunisia, Misri, Yemen na Libya yalikuwa yanafanana sana na yale yaliyosababisha ushindi wa mkubwa wa chama cha Patriotic Front (PF) tarehe 23 Septemba. Ni wazi, baada ya miaka 20 madarakani, lazima kuna jambo lilikwenda vibaya ndani ya chama cha MMD (Movement for Multiparty Democracy –chama ambacho kiliung’oa utawala wa UNIP uliodumu kwa miaka 27.

Baadhi ya “Wabunge” katika kuijadili “hotuba” hiyo, waliipongeza hatua ya kuwashirikisha wanasiasa katika bunge hilo la kufikirika. Mbunge mmoja, Rodger Chali [7]alimsifu mwanasiasa wa upinzani kwa kuwa na uelewa mkubwa wa vyombo vipya vya habari:

Ndugu Mhe Spika, naomba nimshukuru Mhe Chipimo kwa kuwasilisha hotuba yake na kwa kuwa mmoja wa viongozi wanaoelewa nguvu ya vyombo hivi vipya vya habari. Naomba kuwasilisha hata hivyo kwamba, Zambia haina tatizo la ukosefu wa Marais wenye akili, bali mfumo unaoyawezesha majimbo na wilaya kujiendeleza bila kulazimika kuitegemea Lusaka. Ningependa kwa hiyo kumpa changamoto Mhe Chipimo kuongoza madai ya kuikomboa Zambia kutoka katika udhibiti wa Lusaka. Hii ni ajenda pekee ambayo italeta fanaka. Kama anaweza kutekeleza suala hili moja kabla ya mwaka 2016, ninaweza kumwamini awe rais. Ndugu Spika, nisingependa kusikia kwamba mheshimiwa huyu atalitekeleza hili pale tu atakapochaguliwa kuwa rais.

Kasololo Chisenga alisema:

Mhe Spika kwa kweli mgombea wa urais Mhe Elias Chipimo ameibua hoja muhimu ambazo zinastahili kabisa kujadiliwa bungeni. Nimevutiwa hasa na pendekezo lake kuhusu kukua kwa bayoanuai na kuja na wazo la “uchumi mpya” nchini Zambia. Hili kwa kweli limejaa ubunifu na ndicho hasa kinachotegemewa kutoka kwa viongozi vijana kama yeye. Ni matumaini yangu kwamba mawazo kama haya yanaweza kuchukuliwa kwa uzito unaostahili kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.

Katika suala hilo hilo la bayoanuai, Nicholas Mutalama aliongeza:

Mhe Spika, utafiti wa nishati ya bayoanuai hivi sasa umeshika kasi huko kwenye nchi za Magharibi na wakulima (wa huko) wako kwenye harakati za kutumia mbinu hii kupitia mipango inayofadhiliwa na serikali na watu binafsi. Kwa nini inatuchukuwa muda mrefu kurukia kwenye fursa endelevu kama… hizi ili tusonge mbele. Mheshimiwa, tawala zilizopita pamoja na utawala huu uliopo madarakani zimeelekeza mipango yake ambayo kimsingi haiwezi kuzalisha kitu chochote cha maana…! Hili tunaweza kulifanya au labda ni labda tu, tunasubiri mwekezaji mwingine au mfadhili aje kutuokoa wakati suala lilikuwa ni uwajibikaji ulio makini wa kifedha na kubeba wajibu wetu ambao ungeweza kutupatia fedha nyingi zinazohitajika kwa ajili ya hatua za mwanzo za uwekezaji.

Zambian People's Parliament (ZAPP) [3] ni bunge la mtandaoni lilianzishwa mara tu baada ya uchaguzi wa Septemba 20 uliokifanya chama cha upinzani, PF (Patriotic Front) kuking’oa [8] chama tawala cha MMD ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 20. Kikundi hiki cha Facebook kilianzishwa kwa nguvu ya kikundi kingine cha cha Facebook kiitwachoZambian Peoples Pact [9] ambacho kilifanya kampeni kukipinga chama tawala kilichoangushwa. Yafuatayo ni maelezo yanayokitambulisha kikundi hicho:

Bunge la Watu wa Zambia [3] (ZAPP) ni maigizo ya Bunge la Zambia linaloundwa na makundi mbalimbali ya raia ambao kwa minajili ya kujenga hujadili, huchambua, kubishana, kufuatilia na kukubaliana katika masuala ambayo yanahusu utawala wa kidemokrasia. Kimahususi, ZAPP ni mahali ambapo raia huchangia sauti zao kwa ajili ya utawala wa kidemokrasia wa Zambia na maendeleo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Umuhimu wa mijadala hii ya mtandaoni itakuwa kuwawezesha raia kuchangia mawazo katika sera na maamuzi ya bunge na serikali kwa ujumla na kutengeneza jukwaa kwa mijadala ya masuala ya msingi inayoendeshwa na raia wenye uelewa wa masuala ya kisiasa, watawala katika jamii na wataalam na hivyo kuliwezesha kundi kufinyanga wazo linaloweza kutumika katika ufikiwaji wa maamuzi ya serikali.

Tamko la Lengo

Lengo la ZAPP ni kuwahusisha raia, watawala walio bungeni na serikalini, kwenye sekta za umma na zile binafsi katika kutengeneza muelekeo wa sera kwa pamoja na kuhakikisha maamuzi yanayofanywa katika ngazi zote yanaakisi matakwa ya watu wa Zambia kuongozwa kwa mujibu wa kanuni za kidemokrasia.
Tamko la Dira
Maono ya ZAPP ni kuongoza jukwaa la wa-Zambia wa kawaida na wale wenye nafasi katika uongozi ambao hujieleza kwa uhuru na kusikiwa katika serikali ya kidemokrasia ya Zambia na kukuza shughuli za kijamii na kiuchumi katika taifa.