Singapore: Maoni ya Waziri Yasababisha Tafrani Mtandaoni

Kufuatia tamko lifuatalo, Waziri wa Nchi mwenye dhamana ya Mazingira na Maji, Grace Fu, aliibua mkanganyiko miongoni mwa raia wa Singapore:

Nilipofanya uamuzi wa kuingia kwenye siasa mwaka 2006, suala la malipo halikuwa kichocheo. Nilitambua wazi kuwa ningepoteza faragha, mimi na familia yangu tungechunguzwa sana, na hata kupoteza muda wangu mwingi. Nilizingatia pia kwamba kazi yangu ya kitaaluma ingeingiliwa. Hata hivyo, nilikuwa na sababu za kuamini kwamba familia isingeathiriwa sana, japokuwa uamuzi huo ulifanya kipato kupungua. Na ndivyo ilivyokuwa kwenye punguzo la kipato la hivi karibuni. Kama kilichobaki kitaendelea kupunguzwa siku za baadaye, basi wale wanaotaka kuwania nafasi ya kisiasa itawapasa kujiuliza mara mbilimbili.

Minister Grace Fu. Image from Wikipedia.

Waziri Grace Fu. Picha imechukuliwa kwenye mtandao wa Wikipedia.

Kufuatia tangazo la hivi karibuni la kupunguza mishahara kwa mawaziri –hatua ambayo wa-Singapore wengi bado wanaamini bado si ya kiwango cha kuridhisha –Maoni ya Mhe. Fu yaliwakasirisha wengi waliofikiri kwamba wale wanaowania utumishi wa umma hawapaswi kufanya hivyo kwa matarajio ya kupata malipo makubwa kupitia fedha za wananchi.

Ilimlazimu Mhe. Fu kujitokeza na kueleza kwamba tamko lake lilieleweka visivyo, jambo ambalo nimekuwa nikiliona likijitokeza kwa wananachama wa chama tawala cha PAP (People’s Action Party) mara nyingi:

Hebu vijana wadogo, watu wasiostaarabika na watu wasiodhibiti hasira zao wakae pembeni. Wanachama wa chama cha People’s Action Party (PAP) ndilo kundi la watu wanaoongoza kwa kutokueleweka duniani. Inaonekana kama vile hawawezi kusema ama kufanya kitu bila kutokueleweka. Kama wakienda kwenye duka la MacDonald kununua chakula cha Big Mac chenye mbogamboga zaidi ila bila rojo ya pilipili bila shaka wangenunua mnofu wa samaki (Fillet o’Fish).

Ufafanuzi wa Mhe. Fu kuhusu tamko lake haujafanikiwa kupooza hasira za wa-Singapore waliokerwa na maneno yake, kwa sababu wengi wanaona kwamba bado analipwa vizuri kupindukia ikilinganishwa na wa-Singapore wa kawaida.

Mollymeek anaandika kwa kejeli kuhusiana na namna Mhe. Fu alivyoeleweka vibaya:

Kwa sababu ya kukosa kwetu uwezo wa kufikiri mtindo wa maisha unaoweza kuhalalishwa kwa mshahara wa dola za marekani milioni moja, ni rahisi kwetu kufikiri kwamba anajali mali zaidi. Ni kosa letu. Huyu mama haangalii mali. Wala hadai mshahara mnono zaidi. Ni ile tu kwamba mtindo wake wa maisha uko juu kupita kiasi kwamba anaweza kukumbana na ugumu wa kulipia anavyovitumia kama angekuwa alipwe mshahara wa kawaida wa Waziri katika nchi zilizoendelea.

Maoni ya Mhe. Fu ndani ya muda mfupi yaligeuka kuwa zogo la mtandaoni, ambapo watu waliiga na kuweka maneno yao wenyewe.

Lee Kin Mun anaandika kuhusu uchaguzi wake wa kuwa “baba wa blogu” ya Singapore yaani Mrbrown:

Nilipofanya uamuzi wa kuwa mrbrown mwaka 1997, malipo hayakuwa sababu ya msingi. Kena limy kopi ya ISD, “kena sue” mpaka “tng kor” ya mawaziri na kusimamishwa kwa safu yangu ya gazeti ndivyo vilikuwa sababu. Kupoteza muda niliokuwa nautumia kwenye kucheza michezo ya kompyuta nayo ilikuwa sababu muhimu kuiangalia. Nilikuwa na sababu ya kufikiri kwamba familia yangu isingekumbana na mabadiliko makubwa ya mtindo wa maisha lakini tuliuza gari na sasa naendesha baiskeli. Ninaogopa kwamba kama hata kilichobaki kitapunguzwa kwa mara nyingine huko mbeleni, nitakula mweleka na baiskeli yangu pia.

Joshua Chiang katika uamuzi wa kujiunga na wavuti ya masuala ya kijamii na kisiasa The Online Citizen:

Joshua Chiang Nilipofanya uamuzi wa kujiunga na wavuti wa The Online Citizen mwaka 2009, mshahara haukuwa sababu ya msingi (kwanza haukuwepo). Kupoteza uhuru hasa hasa ISA, kuchafuliwa mimi binafsi pamoja na familia yangu kulikofanywa na vyombo vikuu vya habari na kupoteza fursa zangu zote kupitia mashitaka ya kuchafuana ndizo hasa zilikuwa sababu. Kupoteza kwa utulivu wa akili yangu lilikuwa suala la kutazama sana. Nilikuwa na sababu ya kuamini kwamba familia yangu ingekuwa na nafasi zaidi ya chumba kimoja pale nyumbani kama ningewekwa ndani. Hasa wakati ule tovuti yetu ilipotangazwa kwenye gazeti la serikali. Kama malipo yaliyobaki yataendelea kuminywa zaidi huko mbeleni, itakuwa vigumu kwa yeyote anayefikiri kujiunga na uandishi/uanaharakati wa kiraia.

Hata Danny the Democracy Bear, alama ya chama mbadala cha siasa, SDP (Singapore Democratic Party) alikuwa na tarafakari ifuatayo:

Nilipofanya uamuzi wa kujiunga na chama cha SDP (Singapore Democratic Party) malipo halikuwa suala la msingi sana. Kukosa usiri, kuchambuliwa na umma mimi binafsi na kupoteza muda kwa mambo binafsi ndiyo hasa yalikuwa masuala ya msingi. Ukweli huo kwamba ningekuwa alama ya majaliwa ya chama kwa sababu nilikuwa mwenyewe tu pale lilikuwa suala la kutazama. Nilikuwa na sababu nzito kuamini kwamba familia yangu isingeathirika sana na kubadilika kwa mtindo wa maisha hata kama chama cha PAP kinapenda siku zote kuwashitaki wanachama wa SDP. Kama malipo yataendelea kuminywa zaidi na wanyama wakazuiwa kujiunga na vyama vya siasa huko mbeleni, itakuwa vigumu kwa jamaa zangu wengine kuunga mkono, wala si tu kuungana na chama cha SDP.

Blogu ya Tumblr iitwayo’Nilifanya uamuzi…‘ imetengenezwa kwa ajili ya kuweka mitazamo mbalimbali kuhusu maoni ya Mhe. Fu.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.