Zambia: Rais Sata Aituhumu Benki Kuu Kuchapisha Noti Bandia

Wavuti ya Tumfweko ilipotangaza habari hizi kwa mara ya kwanza mwezi Oktoba kuhusiana na Benki Kuu ya Zambia kuamua kutumia mashine mbadala za kuchapisha noti mbali na mzabuni aliyezoeleka De LaRue, ilichukua muda mrefu kwa Benki Kuu kukiri kufanya hivyo.
Hata hivyo, siku chache baadae, Rais Michael Sata aliweka wazi kwamba ni kweli Benki Kuu ya Zambia kwa maelekezo ya kilichokuwa chama cha Upinzani nchini humo MMD, ilichapisha “noti bandia” ambazo inasemekana ziko kwenye mzunguko wa fedha. Hata hivyo, Chama cha MMD kwa kupitia Waziri wake wa zamani wa Fedha Situmbeko Musokotwane, kimekana tuhuma hizo kikisema Benki Kuu inayo uhuru wa kuchapisha noti mpya za ziada bila kuwasiliana na Waziri wa Fedha ama Rais kwa sababu ina mamlaka kamili ya kufanya hivyo.
Mara tu Rais Sata alipoapisha baada ya uchaguzi wa Septemba 20, Gavana wa Benki Kuu Dk. Caleb Fundanga alikuwa mmoja wa watumishi waandamizi wa serikali au mashirika ya umma wa mwanzo kabisa, kama sio wa kwanza, waliokuwa wakihusishwa na chama tawala kilichoangushwa madarakani kuondolewa kutoka kwenye nafasi zao. Katika hali ya kushangaza, nafasi hiyo haikujazwa kwa zaidi ya miezi miwili baadae.
Rais Sata na serikali yake ya chama cha PF wameanika vitendo kadhaa vya kifisadi ambavyo viliendelea katika kipindi cha utawala wa mtangulizi wake, Rupiah Banda kama vile ununuzi wa magari ya bei mbaya aina ya Lexus, kufukuliwa kwa mabilioni ya Kwacha kutoka kwenye shamba la waziri wa zamani na skandali nyinginezo ambazo bado bado hazijadhibitishwa.
Habari za kuibuliwa kwa kashfa hii zimepokelewa kwa miitikio mbalimbali kwa (kuwapo) baadhi ya raia watumiao mtandao kuunga mkono hatua hizo za serikali wakati huo huo wengine wakionyesha kutokubaliana na Rais kwa namna anavyoshughulikia masuala ya kitaifa.
Mchangiaji mmoja, KGB, aliyetoa maoni yake katika jarida la Lusaka Times alipendekeza kwamba Zambia ibadili sarafu yake:

Noti ya Kwacha ya 20,000. Picha kwa hisani ya Zambian Watchdog


Ndugu zangu wananchi, waume kwa wake, kama maafisa wetu wa usalama na sheria kwa pamoja walifukua kwenye shamba la Asiyejiheshimu Austin Liato (K bilioni 2.1 zilizokuwa zimefukiwa kwa kutumia pipa imara) basi Serikali lazima ibadili fedha (sarafu) zake haraka sana kukwepa mfumuko wa bei utakaoshindwa kudhibitika katika nchi yetu. Lazima kutakuwepo fedha nyingi zaidi zilizofukiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Kwa hiyo tusiruhusu wale “wanasiasa” wabinafsi kuuangamiza uchumi wetu kwa kuingiza Kwacha bandia –zilizochapishwa kwa nia zilizojaa uovu –katika uchumi wetu. Tafadhali Rais SATA badilisha noti SASA ili (waliofukua fedha ardhini) wakose pa kuyapeleka hayo mabilioni ya Kwacha bandia. Ndugu Rais tuko nyuma yako.

Mchangiaji mwingine anayejiita Zambia Taifa Lililolaaniwa: Miaka mingine mitano iliyopotea bure, anamshauri Sata kushunghulika na Benki Kuu kimya kimya:

Huyu mtu ni mwongo. Kwa hakika kama kungekwa na noti bandia kwenye mzunguko wa uchumi tungeshaona mfumuko wa bei ukipaa mara tatu. Na alichosema katibu wa Baraza la Mawaziri Joshua Kanganja na Chibiliti kwenye Wizara ya Fedha kinahusianaje na kuchapisha noti? Sata tafadhali elekeza dukuduku lako kwa Benki Kuu ya Zambia (BOZ). Katika umri wako na hicho unachokiita uzoefu hujui hata namna serikali inavyoendeshwa. Sata wewe ni mtu asiyewajibika kabisa. Jambo hili lina uzito mkubwa. Katika tukio lisilo na uwezekano wa kutokea kwamba basi hili tulilosikia ni ukweli, rais mwenye akili angeliiagiza Benki Kuu kimya kimya kuziondoa noti hizo bandia. Ulichokifanya kwa tuhuma hizi zisizoeleweka ni kuleta mashaka yasiyo ya lazima kwa uchumi. Tafadhali wakati mwingine utaapa kwa jamaa wa kabila lako baki kwenye wajibu. Tumechoka na maombi yako yasiyoisha malalamiko…aha!

Lundazi Dweller aliandika:

Inahuzunisha wakati rais anapojishusha kwa kiwango cha porojo za kilabuni. Sasa akiwa rais hakuna haja yoyote ya yeye kuzungumza kirahisi rahisi kama alivyozoea wakati hajawa rais kwa sababu kipindi hicho angetoa maoni yake kwa sababu tu ya uvumi na yanayosemwa kijiweni. Benki Kuu ya Zambia imebadili mashine za kuchapia noti hivi hii inatosha kuzifanya noti ziwe bandia? Je, anaweza kulieleza taifa ni kiasi gani cha ziada cha fedha kilichapishwa? Kwa hakika ninatarajia utaalam kwenye masuala ya urais kuliko hivi anavyofanya huyu.

Kasapato, akimtetea rais Sata, aliandika:

Wale wote wanaopinga kile kinachofanywa na rais wangu wanajifunua jinsi wanavyoonesha chuki binafsi kufuatia ukweli kwamba chama cha PF kilishinda na wamebaki na ghadhabu (Wengi wao ni wale wanaotoka chama ambacho hakitakaa kiitawale Zambia tena (UPND). Kwa taarifa yenu meli ilishavuka bahari wakati huu na mmebaki na kushikana mikono kusiko na nguvu (Hajanza). Jifunzeni kuishi na ukweli kwamba jina la Sata limo kwenye vitabu na hata Mungu alikuwa na mkono wake kwenye uteuzi wake. Ni wazi kwamba noti zilichapishwa na kama mna werevu wa kutosha chunguzeni noti mtaona alama za mashine tofauti ya kuchapia enyi wachache mlio na hasira!

Kwenye twita, mtumiaji mmoja alikuwa ameguswa na kasi ya kutisha ya kuporomoka kwa Kwacha dhidi ya Dola ya Marekani.

@mosesmafwenko: Leo tunabadilisha K5210 kwa Dola moja. Inawezekana ni zile noti bandia! #BOZ #zambia @sandaykc @missbwalya @GNdhlovu

Baada ya wavuti ya Zambian Watchdog kuweka hotuba ya Naibu Gavana wa Banki Kuu ya Zambia, Bwalya Ng’andu, katika semina ya usambazaji wa fedha ambako aliweka mambo wazi kwamba moja ya makampuni yanayosemekana kuchapisha fedha isivyo halali yalianza kazi hiyo tangu wakati wa kipindi cha utawala wa marehemu Levy Mwanawasa, mwanachama mmoja wa kikundi cha Facebook kinachoitwa Issues Concerning Us alikuwa na haya ya kusema [maoni haya kwa sasa yameondolewa]:

Kama ilivyo kawaida tumempigia kelele mbwa mwitu. Je, nini tutaishia nacho? Ni kitu kama hiki
Makampuni ya Giesecke na Devrient yalianza kuchapisha noti za Kwacha katika uatwala wa Mwanawasa | Zambian Watchdog
www.zambianwatchdog.com
Makampuni ya Giesecke na Devrient GmbH ya Ujerumani yalianza kuchapisha noti za Kwacha wakati wa utawala wa Levy mwanawasa.

Jibu moja chini ya makala hiyo lililowekwa na Himalambo Swedish Sianyaka, linasomeka:

Kama huu ndio uzoefu ambao Sata alidai kuwa nao ili kuendesha serikali basi anahitaji kuchunguzwa ubongo? Sakata zima linakera kwa mkuu wa nchi kusimama juu ya kichunguu cha mchwa na kuanza kupigia kelele masuala asiyoyaelewa vya kutosha. Mtu anahitaji kumwambia afikiri na kuchambua masuala kabla hajafunua mdomo wake.

Mtumiaji mwingine wa mtandao anayejiita Zambia Iva New kwenye kundi la facebook liitwalo Zambian People Pact hakuwa muungwana sana na matendo ya serikali ya chama cha PF:

Chama cha PF kinaonekana kufanikiwa kwenye kufanyia kazi tetesi –kwanza GBM anogopa kivuli chake mwenyewe, kashfa ya Dhahabu, wakubwa wa NW, Majenerali wastaafu na sasa kushapishwa kwa noti (bandia) au zisizo halali. Hii ni serikali gani, wasitupotezee muda waelekeze nguvu zao kwenye siku ya mwisho inayokaribia sana katika siku 90 walizojipa za kukomesha biashara ya “kachepa”. Hatutapotezewa mwelekeo kwa kuelekezwa kwenye masuala yanayochefua. Iwavyo, hii inaonekana ni mbinu ya “kaponya” wanaokuchomolea ukiwa unaangalia kwingine. Mara moja wameshakupekua na mifuko ya suruali. Tuwe makini sana wananchi wenzangu macho yetu yawe kwenye mpira ama sivyo mifuko yetu itapekuliwa. “Ba japonya kwena” (hawa wahuni)!

Chita Matt Nonde alijibu maoni hayo kwenye Zambia Iva New kwa kutumia swali:

Hivi [wewe] unataka kusema tuliishi peponi katika miaka 20 iliyopita ya utawala wa MMD?

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.