Zambia: Magari Mapya ya Kifahari ya Mtoto wa Rais Yasababisha Minong’ono

Inaonekana kwamba kuna upungufu wa mambo mapya ya kisiasa yanayoibuliwa kwa wa-Zambia siku hizi. Wakati mtoto wa Rais wa zamani Banda akiendelea kuchunguzwa kwa manunuzi yenye utata kabla ya uchaguzi, mtoto wa rais mpya Mulenga Sata, naye yu katikati ya utata mkubwa kufuatia habari zilizoibuliwa na mkurugenzi mtendaji wa Asasi ya Kiraia iitwayo Committee of Citizens, Gregory Chifire kwamba katika siku za hivi karibuni (Mulenga) alijipatia magari ya bei mbaya yenye thamani ya Kwacha za Zambia zipatazo bilioni 1.8 (sawa na Dola za kimarekani 200,000).

Wa-Zambia wanatathmini habari hizi katika wavuti ya Zambian Watchdog:

Mpimpa anasema:

Kauli mbiu ya kisiasa ya chama cha PF ya fedha zaidi kwenye mifuko yenu ilikuwa kweli tupu. Sisi wengine hatujaziona hizi fedha, bado tunaenda kulala tukiwa tumekula mlo mmoja tu, lakini bado majirani zetu wananunua magari ya kifahari kwa bilioni 1. Mfano wa namna gani Ndugu Rais. Tafadhali tembea kwenye maneno yako mwenyewe kwa kuanzia ndani ya familia yako. Ee Mwenyezi Mungu uturehemu!!!!!!!!!!!!!!!!!

KimZ anaongeza:

Mtoto wa kiume wa Rais Michael Sata (aliyebeba kamera). Picha kwa hisani ya Zambian watchdog.

Mujanwa Mukikopo, kwa nini tunawauliza maswali watoto wa Rais kama tunajua wanao upendeleo wa kujipatia mali wakiwa kama watoto wa Rais aliye madarakani? Au kwa sababu tu hili limefanywa na mtoto wa mtu unayempenda basi inakuwa kawaida? Hivi sasa, watu wanamlaani Liato kwa zile bilioni 2.1 (zilizokuwa zimefukiwa ardhini) na Liato alikuwa waziri kwa muda mrefu. Mulenga ambaye baba yake hata hajamaliza siku tisini tangu aingie ikulu ametumia mpaka sasa K bilioni 1.8. Unaweza kuona kiasi gani atakitumia baba yake akiitawala nchi hii kwa miaka mitano.

Makala hiyo inabainisha kwamba kazi kubwa ya Mulenga ilikuwa ni kuingiza mbwa kwenye soko la Zambia na kwa hivyo Sipho kwa kichekesho analitathmini hili:

naine ndeya muku order ama puppies kuti wa wina!!! [Tafsiri: Hata mimi nitaanza kuingiza mbwa, huenda ninaweza kufanikiwa/kuwa tajiri].

Kwa hali ya kumaanisha anachokisema, Kabanshi analalamika:

Inahuzunisha kuona kwamba kwa sababu tu baba ni rais basi hana haki ya kumiliki gari kama hilo, kama mtu kama mimi ninamiliki (gari la aina ile) na hakuna mtu angeweza kujua kinachoendelea, nadhani wamiliki wa wavuti hii pamoja na watu wanaotoa maoni yao hapa waonyeshe kukomaa katika namna wanavyojadili masuala yenye maslahi ya taifa. Kwa kawaida unajikuta unasoma maoni yanayochefua ambayo hayaleti maana kabisa na kwa sababu tu watu wanayo hadhira basi kila akina Jim na Jack wanadhani wana habari. Huyu mtu anayejiita kiongozi wa AZISE hii ambayo nimeisikia leo kwa mara ya kwanza anaweza tu kuleta habari ambazo huenda alikuwa akijadiliana na rafiki zake kilabuni na ndivyo ilivyo kwamba jarida hili linafikiri kila kitu ni sahihi bila hata kuwa na vyanzo vya kuaminika. Aibu!!!

Black Doyo anamtetea mtoto wa Sata:

Nyie watu muwe na uhakika na mnachokisema! Mulenga ni mhandisi wa ujenzi aliyebobea. Huyu jamaa amesoma.

Watumia mtandao wamekuwa wakizungumzia hatua ambayo haikutegemewa katika siasa za Zambia baada ya rais kuziomba mamlaka za kutekeleza sheria nchini humo kumchunguza mwanae na kumshauri Bw. Chifire aliyeibua tuhuma hizi kupeleka taarifa za kitendo chochote kinachohisiwa kuwa kinyume cha sheria na kinachohusianishwa na familia ya rais kwenda kwa mamlaka za kisheria zinazohusika.

Akijadili hili kwenye wavuti ya Tumfweko.com, Tumbo Tumbo anasema:

Mhe. Sata amefanya kile ambacho mtangulizi wake Rupia Banda asingeweza kamwe kukifanya. Kitendo cha kuruhusu mwanae achunguzwe na mamlaka za kisheria zinazohusika zikishirikiana na Polisi ni cha kuungwa mkono. Chifire lazima awe makini sana, kwa sababu kama baadhi ya blogu zinazowahukumu watu wengine kwenye magazeti pasipo wanaotuhumiwa hao kupewa fursa ya kujibu ama kujitetea. MULANGA Sata ni mwuungwana. Ninaamini Chifire anao ushahidi.

Mhe. Sata lazima vile vile aliambie taifa kuweka wazi kilichotokea kufuatia taarifa aliyoiomba kutoka kwenye Baraza la Mawaziri na idara za upepelezi kuhusiana na Dk. Miti ambaye uteuzi wake ulitenguliwa ndani ya masaa 24 baada ya kuwa ameteuliwa kuwa Balozi wa Zambia kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO), huko Geneva. Mrejesho wa wazi kwa wa-Zambia ni wa muhimu kama ilivyo kwa mwanae, Mulenga. Tunaye rais anayeaminika, asiye na woga ndani ya Mhe. Sata. Hebu Miti na Mulenga wasafishwe na idara hizi za upelelezi!!! Kwa uwazi!!!!

Mulenga, kupitia mwanasheria wake, amempa Gregory Chifire masaa 48 kumtaka radhi vinginevyo atampeleka mahakamani. Chifire anasema hatishiki na anaisubiri polisi wamwite ili aweze kwenda na kuwaambia kile anachokijua.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.