Tanzania: Zinavyosema Blogu na Twita Katika Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania

Desemba 9, 2011, ni siku maalumu kwa Watanzania wakati Tanganyika, ambayo ni sehemu ya Muungano wa Tanzania ikitimiza miaka 50 ya uhuru. Katika mtandao, wanablogu na watumiaji wa twita wanasherehekea na kutafakari kwa kina mustakabali wa Tanzania.
The Dar es Salaam blogger's Circle iliwaomba wanablogu kuadhimisha tukio hili kwa kutuma makala kwa ajili ya siku ya Desemba 9:

Kanuni ni rahisi:
Andika makala ya blogu inayohusiana na mada kuu.
Iwekee alama kwenye twita #DarBlogCircle na ##Tanzania50.
Itume pia hapa: http://www.facebook.com/DarBlogCircle

Misterny anaweka vipande vya nukuu zilizochukuliwa kutoka kwenye barua iliyoandikwa na Mwalimu Nyerere kwa mawaziri wake na wakuu wa chama mwaka 1964:

Nembo rasmi ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania. Chanzo cha Picha: serikali ya Tanzania


Je, wanapenda (wananchi wa kawaida) kweli kupigiwa kelele za kuondoka barabarani kwa sababu rais, waziri au mkuu wa mkoa anaendeshwa mchana? (…) Je, wanajisikia fahari na uzalendo kila wakati wanapotakiwa kuacha walichokuwa wanafanya na kusimama wima kwa sababu tu mkubwa mteule mpya ambaye huenda hata hawajawahi kumwona hapo kabla anapigiwa wimbo wa taifa? (…) Utu hauhitaji ubinafsi kuuondoa: na ubinafsi wa namna zake zote ni mbaya. Hata kama ilikuwa imehakikishwa kwamba watu wanaufurahia –kitu ambacho sikiamini sana –bado ubinafsi ungeendelea kuwa mbaya; na ingeendelea kuwa wajibu wetu kuumaliza na kuwaambia watu kwamba kile walichojifunza kukifurahia ni kibaya (…)

Baada ya kubainisha mambo machache ambayo Tanzania ingeweza kufanya vizuri zaidi, David Mugo aliyeishi Tanzania kwa miezi 18, alimalizia makala yake kwa kusema:

Kwa kuhitimisha, bado ninadhani Tanzania ingali moja ya nchi nzuri za Kiafrika nilizowahi kuzizuru. Watu wake ni wema sana. Heri ya siku ya Uhuru, tafakarini uhuru gani mlionao, unamaanisha nini kwenu, kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Ninawapa changamoto vijana kuyatazama mambo zaidi ya macho ya watawala wetu wanaozeeka. Hongera sana. Idumu Tanzania na watu wake.

Mwanaharakati wa Kitanzania na mwanablogu, Ashura, anashangaa, “Tuko wapi katika umri wa miaka 50?”:

Katika Azimio la Arusha la mwaka 1967 la Mwalimu Nyerere alisema “Uhuru maana yake ni Kujitegemea. Uhuru hauwezi kuwa wa kweli kama taifa linategemea fadhila na mikopo kutoka kwa taifa jingine kwa ajili ya maendeleo yake…” Hebu na tujiulize leo je Tanganyika haitegemei fadhila na mikopo kwa ajili ya maendeleo? Jibu ni ndiyo ndio maana sehemu kubwa ya ardhi inauzwa kwa makampuni ya kigeni ikiwaacha watanzania bila ardhi wala fidia. Serikali yetu inafikiri maendeleo yataletwa na wageni kwa kuwaacha wa-Tanzania, kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere hatuwezi kutegemea makampuni ya kigeni na kufanya tunavyojisikia! Ni miaka 50 tangu Tanganyika ilipopata uhuru wake Desemba 9, 1961 na nchi ni kama inarudi kinyume nyume na imedumaa kabisa. Mwaka 1967, paundi moja ya Uingereza ilibadilishwa kwa Tsh. 16.6 leo paundi hiyo hiyo ina thamani ya Tsh. 2650 na zaidi! Hili lina maana mbaya kiuchumi.

Katika kusherehekea miaka 50 ya uhuru, The Wayward Press anaandika:

Mwalimu Nyerere akisherehekea uhuru. Picha imewekwa kwenye ukurasa wa Facebook uitwao Tanzania-Have-Your-Say.


Hivi sasa, nchi yetu imejikuta kwenye wakati wa mpito na usiotabirika kabisa. Siasa zetu zinakosa mwelekeo na muono mpana wa kiitikadi kututegemeza kuelekea mbele. Watawala wetu wanaonekana kukata tama kadri siku zinavyoendelea. Ufahamu wetu wa kihistoria uko katika vipande vipande na umejikita kwenye maono tenge yanayotilia mkazo yaliyopita. Utambulisho wetu wa kiutamaduni umeparaganyika, ukiiga zaidi ule wa kigeni kuliko namna yoyote ya utamaduni wa ndani. Kuwa Mtanzania wa kisasa siku hizi ni kuwa mtu wa usiye na uhakika na vile mustakabali wako ulivyo.

Blogu ya The Creatively Maladjusted inatazama kublogu na vyombo vya habari vya kijamii nchini Tanzania katika miaka 50:

Katika nchi kama Tanzania ambapo habari zinazotawala vyombo vikuu vya habari zinauwezekano wa kufuatiliwa na kudhibitiwa na serikali ama kwa uchache sana haziaminiki (kwa kuwa mwelekeo wake unabadilika badilika), kublogu (na vyombo vya habari vya kijamii kwa ujumla) kunafungua nafasi pana zaidi kwa fursa. “Vyombo vya habari vya kijamii ninaweza kusema vinawapa watanzania sauti yao wenyewe. Hiyo ni fursa yenye nguvu ninayoweza kuifikiria nikiwa wazi” –Elsie wa The Mikocheni Report Blog. Jibu la kawaida (mara nyingi likikusudia kuhitimisha majadiliano zaidi) ninalolisikia katika mijadala kuhusu vyombo vya habari vya kijamii ni kwamba watu wengi hawajaunganishwa na mtandao wa intaneti. Katika maeneo ya vijijini ambapo asilimia 75 ya watu wanaishi, basi kutokuunganishwa bila shaka ni changamoto kubwa (kwa kuhusianisha na mtandao duni wa umeme na huduma ndogo na ghali za mikahawa ya mtandao wa intaneti), lakini hali hii inabadilika kwa kutazama upatikanaji na uhitaji, kwa kujumlisha ongezeko kubwa upatikanaji wa huduma rahisi za intaneti kwenye simu za viganjani na vijana wa kizazi kipya wanavutiwa na uunganishwaji unaopatikana kwenye vyombo vya habari vya kijamii. Mijini ninaweza kusema kwamba idadi kubwa ya watu angalau wamejiunga na Facebook, na kwa kupitia viunga vya Facebook labda wana uwezekano wa kuunganishwa moja kwa moja na blogu/uandishi wa kuraia kuliko watu wanaoishi Magharibi…

Ahmed wa VijanaFM anauliza, “Tanzania kwenye miaka 50 tuna nini cha kuonyesha?”:

Ninadhani kuna changamoto hivi sasa ya kuwalazimisha watu watafakari yaliyofanyika kwa miaka 50. Tunakumbuka nyakati nzuri lakini wakati huo huo tunabaki kukumbushwa zile mbaya. Tuna changamoto nyingi na, kama usemi ulivyo, je watanzania wanajisikia afadhali leo kuliko walivyokuwa miaka kumi iliyopita, achilia mbali miaka 50 iliyopita? Jibu labda ni hapana. Ninafikiri badala ya kukumbuka siku nzuri za kale twapaswa kukujitazama ndani yetu, sote wananchi na watawala na kujihoji namna gani tutaijenga kesho yenye nafuu. Hii ni kwa sababu ninadhani wengi wetu tunawiwa kuhusu namna gani miaka mingine 50 itakavyokuwa.

Karim Hirji, Professor wa takwimu-viumbe wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba, anaujadili mfumo wa elimu nchini Tanzania baada ya miaka 50 ya uhuru:

Wakati wa uhuru, hakuna hata daktari mmoja alifunzwa hapa Tanzania. Sasa, darasa langu la mbinu za utafiti kwenye Chuo Kikuu cha Muhimbili cha Afya na Sayansi za Tiba lina wanafunzi 150. Utata wangu unaakisi hali ilivyo katika kila somo linalofundishwa katika chuo changu na, kwa hakika, katika vyuo vyote vikuu nchini. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa kasi, lakini idadi ya wahadhiri na vifaa vya kufundishia havijaongezeka. Baadhi ya vyuo vikuu bina idara zenye wahadhiri kadri ya 20 hivi, na bado hakuna mwenye Shahada ya Uzamivu…Tumetoka kuhitimisha zoezi la kupitia upya mitaala lililogahrimu Mamilioni ya dola za mikamrekani. Bado, hakuna idara iliyobadili kile inachokifundisha.

Kwenye twita, watumiaji twita wanasherehekea miaka 50 ya Tanzania kwa kutumia alama #Tanzania50:

dgtlUbun2: Ninakumbuka maisha YOTE yaliyopotea KWA UZEMBE kwenye ajali mbaya ya Boti huko Zanzibar na maisha mengi YALIYOPOTEA kwa sababu ya mfumo wa kifisadi. #Tanzania50

@BabatundeJnr: Heri ya siku ya kuzaliwa kwa taifa la Mwafrika Mashuhuri Julius Nyerere #Tanzania50. Ninawatakia watu wote uhuru kutoka kwenye ufisadi na utawala mbovu #Africa

@ChickAboutTown: Heri ya kufikia miaka 50, Tanganyika! #tanzania50

@SalimHatib: Msiwasahau mashujaa walioyatoa maisha yao kutuletea siku hii yenye utukufu. Heri ya siku ya Uhuru #Tanzania50

@dgtlUbun2: Ni Tanzania peke yake ambapo zaidi ya asilimia 80 ya watu wanaishi kwenye umasikini, LAKINI wabunge wanapata ongezeko la asilimia 185 kama posho ya kuhudhuria vikao. Hii ni serikali ya #tanzania yenye miaka 50 inayowajibika.

@SwahiliStreet: Mnisamehe, lakini sherehe za uhuru zilijumuisha onyesho la polisi la namna ya kutuliza maandamano ya wananchi?

@KateBomz: Nimalizie kwa —> #Tanzania katika miaka 50 nini unacho cha kuonyesha? Imeandikwa na @asalim86 http://vijana.fm/2011/12/07/ni-hamsini-ni-hamsini-tanzania-at-50-what-do-we-have-to-show-for-it/ Nimehifadhi andiko bora zaidi hatimaye!

@tweetingchaga: Kuondoka kwa Waingereza kutoka Tanganyika mwaka 1961 kulifanyika kabla ya wakati. Ndio, ninasema #Tanzania50 @atititu @dizainatweets @jmkikwete

@Dunia_Duara: Blogu kuhusu #Tanzania50. Soma na/au jiunge @DarBlogCircle: facebook.com/DarBlogCircle

Tanganyika ilijipatia uhuru wake kutoka Uingereza Desemba 9, 1961, na baade Tanganyika iliungana na Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 2

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.