Uganda: Polisi Wawanyunyizia Waandamanaji Rangi ya Waridi

Polisi wa Uganda wameikabili kampeni inayoendelea kwa mwezi mmoja sasa ya Kutembea Kwenda Kazini kwa kuwanyunyuzia waandamanaji mabomu ya machozi na risasi sa moto. Wakati wa maandamano siku ya Jumanne, walitumia mbinu mpya, ya kuwashambula waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuandamana kuelekea viwanja vya katiba katikati ya jiji la Kampala kwa maji yaliyochanganywa na maji ya rangi ya waridi.

Gazeti la New Vision la Uganda lilituma picha ya viongozi wa upinzani waliokuwa wamemwagiwa rangi hiyo kwa njia ya Twita. Mtumiaji wa yfrog flashdancer11 alituma picha hii:

Baadhi ya wanablogu walinyooshea kidole kejeli ya serikali ya kuwanyunyuzia waandamanaji rangi ya waridi – rangi ambayo mara nyingi huhusishwa na jamii ya mashoga na wasagaji – ikizingatiwa kuwa muswada unaopinga ushoga hivi sasa unapitiwa ndani ya bunge la Uganda. Mwanablogu Afrogay anaandika:

… je hili nalo ni jibu la fumbo kwa kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye, ambaye miezi minne iliyopita aliahidi kuhalalisha ushoga ikiwa atachaguliwa?

(Swali ambalo) Afrogay atamjibu kiongozi wa askari wanaowalowesha wapinzani kwa rangi ya waridi: ahsanteni jamaa lakini rangi ya waridi ni sitiari tu. Hakuna haja ya kuichukulia kama hivyo.

Alama ya #pinkstuff pia ni mada maarufu katika ulimwengu wa Twita wa Uganda:

@Rosejackson3: kwa hiyo ni kinyume cha sheria kutembea kwenda kazini #walk2work nchini U/G bila ya kibali. Ikiwa utapsafiri kwa anga, utazuiwa. Kama ukisimama tu, rangi ya waridi -#pinkstuff

@ishtank: Kwa upande mwingine, fikiria hadithi tutakazowasimulia wajukuu wetu. “kaaka, ulikuwa wapi siku rangi ya waridi #pinkStuff #ilipotawala kwenye #Twita?”

Huku wengi waliona kisa hicho cha “rangi ya waridi” kinachekesha, wengine bado wamekasirishwa na namna ambayo serikali imewatendea waandamanaji. Mwanablogu KellyUganda anaandika:

Kwa nini naiona hali hii kana kwamba ni ya ki-Hitler/ki-Nazi? Ni kana kwamba watu hawana haki ya kuandamana kupinga jambo? Sijui ni kwa jinsi gani Museveni anaweza kujidai kuwa naendesha demokrasi. Bila ya shaka watu hawa wananyunyuziwa rangi ya waridi ili polisi waweze kuwanyanyapaa na kuwahoji na kuwaonea wakati wanajaribu kuvunja moyo wao wa jukumu la kiraia na uhuru wa kujieleza!

Katika makala yenye kichwa “Kugeuka kuwa Waridi,” mwanablogu mwingine, Rhino, analalamikia vitendo vya serikali:

Ninaanza kuichukia sana serikali yangu, inaonesha hofu kubwa sana, mantiki ya kitoto na utashi unaostusha wa kutumia nguvu. Hivyo sivyo ninavyotaka kutoka kwake. Ninaitaka iwe ya haki, na kunitia moyo ili niwe mtu bora zaidi na kunisaidia niweze kujenga mahali pazuri pa kuishi kwa ndugu zangu. Siitaki initishie kifo ikiwa nitatofautiana nayo kimawazo na kiutendaji, ikiwa hiyo ndio jamii inayotaka kuiunda, basi sitaki niwe sehemu yake.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.