- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Singapore: Wanablogu Waikosoa Ilani ya PAP

Mada za Habari: Asia Mashariki, Singapore, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uchaguzi, Utawala

Chama kinachotawala Singapore, People’s Action Party (PAP), kilitoa ilani yake ya uchaguzi [1] tarehe 17 aprili, 2011, ambayo mara moja ilikosolewa na wanablogu wengi kwa “kutokuwa wazi”. PAP kimekuwa madarakani kwa miongo mitano. Uchaguzi mkuu [2] nchini humo umefanyika tarehe 7 Mei.

Ilani ya Uchaguzi [3] ya PAP inaahidi mustakabali bora kwa kila mwananchi wa Singapore

Hauwezi kuitegemea PAP kuwatendea vyema zaidi Wasingapori wa kila kada ya maisha, na kuendelea kutuunganisha katika wakati mzuri na mbaya. Kwa pamoja, tutaifanya Singapore kuwa jamii ya kusisimua na shirikishi, yenye nafasi za maisha bora kwa kila raia. Tutakuwa jiji la wazee na vijana

Ili kutekeleza visheni hii, tunaomba ridhaa yenu ili:

• Tutengeneze fursa za kujipatia kipato cha juu kwa wote
• Tuboreshe maisha ya Wasingapori wenye kipato cha chini
• Tuwezeshe kila mtoto kufanya vyema zaidi
• Kujenga mji wa kusisimua na kaya zinazovutia
• Tuwasaidie wazee wawe na maisha yaliyochangamka, yenye afya na yenye kujishirikisha
• Kuwashirikisha wasingapori wote katika kutengeneza mustakabali wao

Ifuatayo ni video [4] ya ilani iliyotayarishwa na PAP:

Ilani hiyo iligusia juu ya ahadi ya PAP kuheshimu maoni tofauti katika jamii. Lakini Bw. Brown alilalamika [5] kuwa maoni hayakubaliwi kwenye tovuti ya video hiyo ya PAP.

jadenster [6] aliweka video hii yenye hali halisi kama ilivyo sasa huko Singapore ambayo inatofautiana na ilani ya PAP:

cloudywind [7] pia ana video fupi ambayo inakosoa urithi wa PAP:

Lucky Tan naye hajashawishika [8]na ilani hiyo na anaonya kwamba ufumbuzi uliopendekezwa umeshawahi kufanyika huko nyuma:

Kwa kweli, ufumbuzi unaelezwa katika ilani, ndiyo yale ambayo PAP imekuwa ikiyafanya kwa miongo mingi iliyopita, kwa mfano, kuwapa mafunzo wafanyakazi wa kipato cha chini kutoka kazi moja ya kipato cha chini kwenda nyingine n.k. Pale ambapo ufumbuzi huo huo unatumika, tutapata matokeo yale yale – kupanuka kwa pengo la vipato, ongezeko la gharama za maisha na kuanguka kwa kiwango cha maisha.

Kupitia tovuti ya Wordle [9], alvinology analinganisha ilani ya PAP na ilani iliyotolewa awali na chama cha upinzani cha Wafanyakazi (Workers’ Party au WP). Ilani ya PAP ina kurasa 25 ikilinganishwa na kurasa 63 katika ilani ya WP. Wanablogu pia waling’amua kuwa ilani ya WP ina mapendekezo ya kina katika maeneo 15 ya sera.

Yawning Bread anakosoa [10] chapa ya uongozi wa PAP:

Inaanza kuchoka. Na kile ambacho PAP haijakigundua ni kuwa huu upigaji kinanda kuhusu hatari ya kushindwa kwa hakika kumeiathiri vibaya Singapore. Mbali na kutufanya tuwe jamii yenye kujiamini, yenye ubunifu ambayo iko tayari kujaribu mambo mapya na kunufaika na majaribio hayo, imetufanya tuwe waoga wa kujaribu na wenye mashaka kiasi. Si ajabu kuwa kiwango cha mashininikizo nchini Singapore ni kikubwa

Blogging for Myself anakishutumu PAP kwa‘kutokuwa na ufahamu’ [11] kuhusu hali ilivyo sasa duniani:

Katika neno moja, PAP HAIFAHAMU LOLOTE. Sitegemei nadharia kuu fulani ambayo ni nzuri kiasi cha kuweza kumpa mwanadamu mwanga wa utabiri wa huko mbeleni, lakini hawa hawana mashiko ya mambo yanavyojiendesha hii leo zaidi ya kushikwa butwaa na ninaweza kusema hivi: mustakabali hauna uhakika.

PAP imekuwa ikijidhulumu chenji kwani imekuwa ikiwachagua watu inaowaamini kuliko wale ambao wana uwezo. Unajua mahusiano ya watu, haiwezekani kuwa na kundi kubwa la watu ambalo unaweza kujenga kuaminiana kweli ndani yake.

Molly Meek anachapa nyaraka yenye maelezo [12] ya ilani ya PAP. Pia anaeleza kuwa ilani hiyo ina nia ya kulinda hali (ya uongozi) kama ilivyo [13]:

Lengo kuu la Ilani ya PAP ni kuendeleza hali kama ilivyo, na kuifanya kuwa bora kwa urembo na kwa takwimu lakini kubaki mbaya katika ukweli halisi. Tegemeeni marekebisho madogo lakini msiwategemee kuitafsiri kwa manufaa yoyote dhahiri kwa Wasingapori; msitegemee lolote linalokaribiana na mabadiliko ya kimuundo katika kufikiri. (Na hapana, hakuna mawazo ya kijumla katika PAP.)

Nigel Tan amesikitishwa na kwamba ilani hiyo imesheheni ahadi ambazo haziko bayana [14]:

Nyaraka yenyewe inaoneka kuwa imesheheni mfululizo wa ahadi sizisokuwa bayana, bila ya maelezo ya kinaganaga ya sera husika wala maelezo yanayofafanua kwa jinsi gani sera hizo zitatekelezwa.

Kadri uchaguzi unavyokaribia, raia wa kwenye mtandao wanaombwa watume picha [15] picha za uchaguzi kwenye tovuti ya GE2011 Media.