- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Wanablogu wa Kenya Waunda Umoja; BAKE

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Kenya, Sheria, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, Wasifu wa Wanablogu

Mnamo tarehe 25 Machi, wanablogu kadhaa wa Kenya walifanya mkutano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi, mkutano uliitishwa na BAKE ( Bloggers Association KEnya). Huo ulikuwa mkutano wa 4 uliotokana na msukumo wa wanablogu wakongwe wa Kenya.

Kumekuwepo na malalamiko mengi, shutuma na hata katika nyakati nyingine, vita vikali vya maneno kurindima kati ya upande wa wanablogu dhidi ya ule wa vyombo vikuu vya habari hasa kuhusiana na matukio ya kugushi habari [1],kitendo ambacho kinakiuka suala la hakimiliki na kutokiri chanzo [2]vitendo vinavyofanywa na vyombo vikuu vya habari [3] na hasa katika taathira ya kublogu katika uzalishaji habari na utangazwaji wake kwa umma na makala mbalimbali nchini Kenya. Mtafaruku huu umeandikwa kiyakinifu zaidi na makala ya kwenye blogu ya Jacque Ndinda aliyoipa kichwa cha habari chaWriteThinking: Plagiarism-masters of copy paste. [4] (yaani Uandishi wa Fikra: ‘Wataalamu wa kugushi kwa mtindo wa kunakili na kubandika).

Wanablogu wa Kenya katika mkutano uliopita wa Barcamp. Chanzo cha picha na: Njeri Wangari


Msingi mkuu wa hoja yake ni jinsi wamiliki wa vyombo vikuu vya habari wanavyodharau suala hili kama wakosefu hasa pale wanapoanikwa hadharani kupitia baruapepe, wakati huohuo hakuna hatua za kinidhamu zinazochukuliwa dhidi ya wahariri. Mara nyingi huishia tu kusema “samahani”, kwa mwanablogu bila kuwepo majadiliano kuhusu fidia au kukiri kwa maandishi.

Jambo hili, miongoni mwa masuala mbalimbali, na vilevile fursa kwa wanablogu yalikuwa baadhi ya mambo yaliyojadiliwa katika mkutano wa Ijumaa hiyo.

Mahudhurio yalikuwa ya kutia moyo ambapo zaidi ya wanablogu 20 walishiriki. Wengi wao walikuwa wanashiriki kwa mara ya kwanza, hasa kwa vile wanablogu waliowahi kushiriki hapo kabla walikuwa na mambo mengine ya kushughulikia.

Makala ya kwenye blogu iliyoandikwa na Kachwanya, [5] ambaye ni mmoja wa wanablogu wanaoblogu sana nchini Kenya, alianika ajenda nzima na vilevile shabaha na malengo ya umoja huo.

Shabaha zetu kimsingi ni:
1.Kubuni na kuhamasisha utoaji habari kupitia mtandao zinazohusu nchi yetu zenye ubora na ubunifu wa hali ya juu
2.Kubuni mkondo wa utafutaji masoko kupitia mtandao unaowezekana kwa ajili ya makampuni ya Kenya
3. Kufurahia kupitia mtandao

Moja ya mambo yaliyotiliwa mkazo sana lilikuwa kuhusu kujenga jamii ambapo wanablogu watasaidiana na kufanya kazi pamoja ili kufikia lengo moja ambalo ni kutoa habari za nchi zilizo mwafaka na zenye kufaa kupitia mtandao.

Katika mjadala uliohusu upatikanaji mapato, kitu ambacho wanablogu wengi, hawakukichukulia kama kichocheo kikubwa katika kiu yao ya kublogu, wengi walikiri kwamba ingawa walikuwa wamejisajili katika makampuni ya kimataifa ya masoko ya mtandaoni, hakukuwa na kitu kikubwa kilichopatikana jambo lililowafanya wengi kujitoa katika huduma. Kwa hiyo, taasisi itabuni, miongoni mwa mambo mengine, jukwaa linalozingatia hali halisi na lililo mwafaka litakalojishughulisha na watangazani kutoka nchini Kenya.
Ilifikiriwa kwamba jambo hili huenda litasaida kufanya wanablogu wajipatie kipato cha ziada pamoja na kwamba sicho kitu wanachokisaka kwa udi na uvumba, lakini bado itawapatia wanablogu kifuta jasho.

Wanjiku, [6] ambaye ni mmoja kati ya wanablogu wakongwe nchini Kenya, alitangaza kwamba ameandikisha anwani za mtandaoni www.bake.co.ke na www.bake.com kwa ajili ya matumizi ya jumuiya ya BAKE .

Baadhi ya shughuli zinazoandaliwa na BAKE ni pamoja na:

Shughuli za
• Maonyesho ya wanablogu kila baada ya miezi mitatu.
• Wanablogu kukutana mara moja kila mwezi kwa saa moja kujifurahisha.
• Mashindano ya blogu kuhusu mada iliyo moto ambapo washindi watapatiwa zawadi kubwa.
• Kuwepo kwa Zawadi kwa blogu kila mwisho wa mwaka.

Wanablogu walioshiriki walitaarifiwa kwamba Collins Mbalo ambaye huendesha blogu inayoitwa ‘A Nairobian’s Perspective’ [7] na ambaye ni mwandishi wa Global Voices [8], atatoa ushauri wake kuhusu masuala ya kisheria hasa kuhusiana na kugushi na ukiukwaji wa hakimiliki, miongoni mwa mambo mengine mengi.

Wengi walikubaliana kwamba jambo hilo lilikuwa vuguvugu la maana na kwamba wakati ulikuwa umefika ili wanablogu wa Kenya wawe na sauti moja.

Kwa hiyo tuna matumaini kwamba mambo mengi mazuri yapo njiani yanakuja katika siku za usoni. Tayari kulikuwa na mnong'ono kwamba kampuni moja kubwa ilikuwa kwenye majadiliano na BAKE ili kudhamini Expo ya kwanza ya Wanablogu. Tuombe kwamba jambo hili liamshe ari si ya kublogu peke yake lakini hasa katika kufanya mambo yaendane vema na utoaji wa makala zilizo mwafaka.