Naijeria Yapiga Kura 2011: Maoni kutoka kwenye Uchaguzi

Makala hii ni sehemu ya habari maalum za Uchaguzi wa Naijeria 2011.

Wanaijeria walipiga kura jana katika uchaguzi wa tatu wa rais tangu taifa hilo lilipoingia kwenye utawala wa kiraia mwaka 1999. Mpaka sasa, uchaguzi huo umeelezwa na wengi kuwa ulikuwa wa mafanikio, huku kukiwa na taarifa za ghasia za hapa na pale na hitilafu za upigaji kura. Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa watu wengi walijitokeza, foleni zenye kufuata utaratibu, na wapiga kura kusubiri hadi uchaguzi utakapomalizika ili kuhakikisha kwamba kura zao zimehesabiwa.

Kama nchi yenye watu wengi zaidi Afrika na muuzaji wa mafuta mkubwa kimataifa, Naijeria inamulikwa kwa ukaribu wakati wa uchaguzi. Chaguzi zilizopita mwaka 2003 na 2007 zilitiwa dosari na uchakachuaji pamoja na ghasia; na matokeo yake, matumaini makubwa yamewekwa kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Parliamentary election results are tallied in Oyo State

Rais aliye madarakani Goodluck Johnathan, makamu wa rais wa zamani ambaye alichukua madaraka baada ya kifo cha aliyemtangulia mwaka jana, anachukuliwa kama mgombea anayeongoza; mshindani wake wa karibu anategemewa kuwa Mohammadu Buhari, ambaye kwa muda mfupi aliongoza nchi hiyo mnamo miaka ya 1980. Washindani wengine ni aliyekuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia rushwa Nuhu Ribadu na Gavana wa Jimbo la Kano Ibrahim Shekarau, kadhalika wagombea wengine 16 kutoka katika vyama vidogo vidogo.

Matokeo rasmi yanatarajiwa siku ya Jumatatu. Kwa habari zaidi, angaliaukurasa maalum wa GV kuhusu Uchaguzi wa Naijeria.

Taarifa kutoka kwenye Uchaguzi

Bella Naija, Chiedu Ifeozo aliandika alivyobadili mawazo yake kuhusu upigaji kura nchini Naijeria. Alisema kwamba japokuwa amepiga kura katika “kila uchaguzi uliofanyika wakati alipokuwa akiishi Uingereza,” alikuwa “haoni sababu” ya kufanya hivyo nyumbani Naijeria kwa sababu ya dhana iliyoenea kwamba ‘kura za Wanaijeria hazina maana’ na kwamba ‘washindi tayari wamekwisha amuliwa.’ Lakini, kama Wanaijeria wengi vijana, Ifeozo alibadili mawazo yake na kwenda kwenda kupiga kura katika msimu huu wa uchaguzi.

Bila kujali mashaka yaliyopo, kumekuwa na mwamko mpya kati ya watu wa kizazi changu juu ya uchaguzi wa 2011. Vikundi mbalimbali vya vijana vimejitokeza ili kuonyesha kwamba kupiga kura siyo tu ‘ni jambo la kisasa’ bali pia vimeendelea na kuonyesha kwa ukaribu ni akina nani wanaogombea ofisi mbalimbali kwa kuendesha chaguzi za kwenye mtandao, kwa kuandaa midahalo, na hata kutengeneza programu-tumizi za intaneti na simu za viganjani kwa ajili ya ufuatiliaji rahisi wa uchaguzi kwa kutumia ripoti za kiraia. Kwa kupitia michakato hiyo, wagombea wamekuwa zaidi ya majina na picha kwenye mabango ya kampeni. (Vikundi hivyo vya vijana) vimekuwa madalali wa mabadiliko ambayo nchi yangu inayahitaji.

Na baada ya hapo alitoa uzoefu wake mmoja baada ya mwingine katika siku hiyo ya kupiga kura:

Saa 7.04 mchana: Ilipofika zamu yangu, moyo wangu ulikuwa unadunda kwa kasi kidogo, siwezi kudanganya. Tulielimishwa jinsi ya kushiriki kwenye mchakato ili kwamba kura zetu zihasibiwe, na sikutaka kufanya makosa, bila ya shaka kwenye bhatua za mwisho. Nilimkabidhi ofisa kadi yangu ya usajili, naye akamkabidhi ofisa mwingine wakati akilitafuta jina langu kwenye orodha. Alipolipata, aliweka wino kwenye kidole gumba changu cha kulia na kunielekeza kwa ofisa wa awali wa kike wa NYSC, ambaye alichomoa kadi mbili tofauti za kupigia kura akazikunja na kupiga muhuri kwenye taarifa fulani nyuma ya kadi hizo. Kisha aliandika mambo kadhaa kabla ya kunikabidhi tena na kunielekeza kwenye chumba cha kupigia kura, kichumba cheupe kilichosimikwa chenye ubao kila upande ili kuzuia mtu yeyote asinione wakati nafanya chaguo langu. Nilielekea kwenye masunduku ya kura, moja kwa ajili ya bunge la seneti, na jingine kwa ajili ya baraza la wawakilishi, nikachomeka karatasi zangu kwenye upenyo na nikawa nimemaliza. Nilipiga kura kwa mara ya kwanza, na kwa kweli jambo la kwanza kupita mawazoni mwangu lilikuwa, “halikuwa jambo baya, au siyo”.

alihitimisha:

Saa 11.15 jioni: Niliona matokeo ya kituo changu cha kupigia kura kwenye intaneti. Midomo ikatanuka na kuwa tabasamu… “huu ni mwanzo wa siku mpya kwa nchi yangu.”

Mfanyakazi wa kituo cha kupigia kura Naijeria. Picha kwa hisani ya @feathersproject

Katika makala yenye kichwa“Vita ya aina nyingine,” Salisu Suleiman aliandika kuhusu jinsi gani msimu wa uchaguzi ulivyoingilia mtiririko wa maisha ya kila siku:

Shule zote zilifungwa. Hapakuwa na aina yoyote ya ufundishaji au kujifunza iliofanyika wakati wote. Na ilipogundulika kuwa shule binafsi ambayo watoto wa rais wanasoma haikufungwa, kilio cha umma kiliilazimu ifungwe pia. Baada ya wiki mbili za mwanzo, ziada iliombwa na ikatolewa. Mpaka sasa ni mwezi mzima, shule zote za msingi na sekondari nchini zimefungwa. Hata katika taasisi za elimu ya juu, hakuna matukio yaliyoendelea.

Katika kipindi hicho cha mwezi mmoja, kila Mnaijeria mwenye umri wa miaka 18 na zaidi aliandikishwa ili aweke jina lake na lalama zake za vidole kwenye vituo mbalimbali. Serikali ilisema kuwa hilo ni jukumu la kiraia. Wahubiri waliwahubiria vikali raia juu ya umuhimu wa kutekeleza jukumu hili lililowekwa wakshi wa kiungu. Vyama vilitumia kila ujanja unaojulikana na usiojulikana ili kuwafikisha watu vituoni. Vikundi vya jumuiya za kiraia vilihakikisha kwamba havikuachwa nyuma na vilipaza sauti juu ya umuhimu wa wananchi kushiriki katika zoezi hili. Sikukuu za kitaifa ziliamriwa katika majimbo kadhaa ili kuhakikisha kwamba taarifa za kila mwananchi ambaye ana uwezo wa kupiga kura zinaorodheshwa. Vifaa vya kisasa vya kidijitali, vyenye thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani Milioni 500 viliagizwa. Na mwisho wa mwezi wa matukio ya haraka haraka, pamoja na kuahirishwa kwa wiki moja, zaidi ya Wanaijeria milioni 73 walishiriki kwa hiari katika zoezi hili adili.

Imnakoya alieleza matumaini yenye tahadhari ambayo wengi kwenye ulimewengu wa blogu wameyaonyesha:

Watu walikuja kupiga kura, na wakasubiri kura zihesabiwe, bila ya kubugudhiwa na wahuni wenye bunduki, kama ilivyokuwa mwaka 2007. Hivi ndivyo inavyoonekana kuwa katika majimbo mengi ya Kusini-magharibi mwa nchi. Haya ni mabadiliko makubwa (ikilinganishwa) na uchaguzi uliopita.

Akiandika kwenyeNigeriansTalk, Kunle Durojaiye anakubali:

Mtu hawezi kupinga kuwa kuna hali ya wimbi la mabadiliko. Watu walipiga kura, na kusubiri ili washuhudie kuhesabiwa na kupangwa kwa kura; vituo vya habari vilirusha matangazo ya moja kwa moja ya uchaguzi wakati unaendelea, na muhimu zaidi, vijana walielekeza zoezi zima kwa mafuriko ya taarifa zilizopatikana kwa njia ya twita, facebook na ujumbe wa blackberry. Bila ya kumung'unya maneno, mabadiliko ni lazima, lakini kila mtu anajiuliza ikiwa uwanja upo tayari kikweli.

Uchaguzi wa Wabunge wa Naijeria ulifanyika Jumamosi iliyopita, Aprili 9. Uchaguzi wa rais ulifanyika jana, Aprili 16. Uchaguzi wa magavana wa majimbo umepangwa kufanyika Aprili 26.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.