Tetemeko la ardhi la ukubwa wa 6.8 lililopiga Jimbo la Kaskazini la Shan nchini Myanmar Alhamis iliyopita, kwa mujibu wa taarifa ya habari iliyorushwa na Televisheni ya Taifa idadi ya vifo imeongezeka na imefikia 74, , na wale waliojeruhiwa idadi yao imefikia watu 100.
Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni kutoka Weekly Eleven, kumekuwepo na matetemeko mengine madogomadogo yaliyofuatia na kuripotiwa mashariki mwa jimbo la Shan na kusababisha hofu miongoni wa wakazi wa maeneo hayo. Mkazi mmoja wa kijiji cha Oak Kyin alisema siku ya tarehe 26 Machi saa 6 mchana:
Usiku uliopita kulikuwa na tetemeko lingine na hata asubuhi ya leo pia. Sithubutu kuendelea kukaa ndani ya nyumba yangu tena. Tunasikia mtetemo zaidi kwenye nyumba yangu kwa sababu yenyewe ndiyo iko chini na imekwenda chini ardhini. Ni vigumu kutabiri nini kitatokea, maana hili ni tukio la kimaumbile la dunia. Nitaacha majaliwa yaamue hatma.
Vilevile, wakaazi walisema kwamba kwa sababu ya tetemeko hilo la ardhi, idadi ya vifo katika vijiji vya Tarchileik, Tarle, Nar Yaung, Mine Lin, Viand Mine Koe vinakadiriwa kuwa zaidi ya mia moja, huku kijiji cha Mine Lin kikiwa kina idadi kuwa zaidi ya waathirika wa tetemeko hilo.
Katika taarifa hiyohiyo ya Weekly Eleven, mfanyakazi wa kutoa misaada alieleza hali ilivyokuwa kule Tarle:
Majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Tarchileik na ile ya Mine Phyat. Vikundi vya watoa misaada kutoka Tarchileik na Kyaing Tong wamepiga kambi kule Tarle. Naweza kusema kwamba hivi sasa hali imetulia kidogo. Kazi ya kujenga upya imeanza. Kambi za ukarabati zimefunguliwa katika vijiji vya Tarle na Nar Yaung.
Mfanyakazi mmoja wa kutoa misaada alikwenda Tarle, eneo lililoathiriwa vibaya zaidi na tetemeko la ardhi alihojiwa na The Irrawaddy:
Niliwasili Tarle majira ya saa 4 asubuhi. Majengo mengi yaliyokuwa ya ghorofa 3 pembezoni mwa barabara hivi sasa yamebaki kuwa ya ghorofa 2 tu, mengi yameanguka. Jumba la Utawa (Monasteri )pia ni kati ya majengo yaliyoanguka. Baadhi ya majengo haya yana zaidi ya umri wa miaka 20, kwa hiyo hali inakuwa mbaya zaidi.
Sio wakazi wa Tarle tu waliolazimika kulala kwenye mahema bali hata wale wa Tarchileik. Nilipowasili Tarle, niliona baadhi ya watu wakiondoa vitu wao wenyewe kutoka kwenye nyumba zao. Wapo waliokuwa wakilia mbele ya nyumba za ndugu zao. Kadhalika niliwaona waliokuwa wakilia kwa ajili ya kuwapoteza ndugu zao. Sikuweza kuwauliza chochote. Naweza kusema tu kwamba baadhi yao walikuwa na bahati kubaki hai.
Serikali bado haijafanya kitu. Wapo waliotumwa kwenda kwenye mahospitali. Lakini mimi sikwenda hospitalini, kwa hiyo sijui nini kinaendelea kule. Ukiniuliza makadirio yangu, naweza kusema watu kiasi cha 60 walipoteza maisha kule Tachileik. Kulikuwa na kati ya watu 20 – 30 waliopoteza maisha kule (Tarle). Naamini waliokufa ni wengi zaidi.
Nilichangia vifaa kadhaa, maji na tambi za kupika haraka. Nilivitoa vyote hivyo kwa maafisa wa makazi. Sijui watavitumiaje vitu hivyo. Wameanzisha sehemu za kujihifadhi za muda. Wale walio na ndugu wamekwenda kuishi nao kwenye nyumba zao.
Kwa sasa, barabara kuu imefungwa kwa muda. Walisema kwamba lengo lilikuwa ni kuifanyia matengenezo.
Mfanyakazi mwingine wa kutoa misaada kutoka Tarchileik alisema:
Tetemeko la ardhi lililotokea mnamo tarehe 24 Machi, saa 2.25 usiku. Saa kadhaa baadae, maofisa kutoka Tarchileik, walinijia na kutaka niende kujitolea kufanya nao kazi. Niliwasili kule Tarle usiku wa manane.
Kwenye barabara kuelekea Tarle, kuna daraja moja kubwa. Tulipofika pale, gari letu lisingeweza kuendelea mbele. Kwa hiyo, ilitulazimu kuvuka daraja kwa miguu na kuendelea kutembea kwa miguu hadi Tarle. Sehemu ya barabara pale kwenye daraja ilikuwa imeporomoka kwa takribani futi 5. Kulikuwa na uharibifu mkubwa. Kwa baadhi ya nyumba mtu uliweza kuona paa tu, nyumba nzima ilikuwa imetitia ardhini.
Nilichofanya pale ilikuwa ni kuwasafirisha majeruhi kwenda hospitali ya Tarchileik. Kuna hospitali kule Tarle, lakini nayo iikuwa imeharibiwa vibaya. Kwa hiyo, mwanzoni ilitulazimu kuwalaza wagonjwa kwenye uwanja mtupu ulio mbele ya jengo la hospitali na kuwapa matibabu pale. Baadaye, walibebwa kwenye machela hadi kwenye magari upande mwingine wa daraja. Umbali wa kutembea hapo ulichukua takribani dakika 15.
Baada ya kufika upande wa pili wa daraja, hatukuweza kuanza safari ya kwenda hospitali mara. Kwani hatukuwa na machela nyingi za kutosha, ilitulazimu kurudisha machela kule hospitali ili tubebe wagonjwa wengine. Pia hakukuwa na magari ya kutosha, kwa hiyo isingewezekana kumsafirisha mgonjwa mmoja peke yake kwenye gari. Kwa hiyo, mgonjwa aliyepelekwa wa kwanza hadi kwenye gari, ilimlazimu kuendelea kusubiri ili wagonjwa wengine waletwe.
Jambo lingine ni kuwa ilitulazimu kusubiri vibali kutoka ngazi mbalimbali kabla hatujaruhusiwa kuondoka na gari kwenda hospitali. Jambo hilo linapoteza kiasi kikubwa tu cha muda. Katika gari niliyiopaswa kuendesha, mgonjwa mmoja alifariki tulipokaribia kufika hospitali ya Tarchileik. Wapo walionusurika katika janga la tetemeko la ardhi, lakini walikufa huku kwa kweli wangeweza kabisa kuokolewa kwa sababu hawakupata matibabu katika muda mwafaka ili kumudu kuvumilia majeraha yao. Kwa kweli jambo hili linanihuzunisha sana.
U Win Swe, ambaye ni rais wa Chama cha Jiolojia cha Myanmar, aliliambia Weekly Eleven:
Miaka ya nyuma, matetemeko ya ardhi makubwa zaidi yaliwahi kutokea katika jimbo la Shan. Lakini sasa ni muda mrefu umepita tangu tetemeko litokee. Matetemeko ya ardhi huwa yana kawaida ya kujirudia katika maeneo ambako tayari yameshatokea. Suala lilikuwa tu ni kwa karibu-karibu kiasi gani. Katika maeneo ulikotokea ufa wa tetemeko la ardhi, daima kuna kawaida ya tetemeko kubwa kufuatiwa na mengine madogomadogo.
Alitahadharisha kwamba kwa sababu miamba iliyo chini ya India inaendelea kusukuma kuelekea bara Asia, basi Myanmar haina budi kuwa kwenye tahadhari siku zote na hasa kwa siku za usoni.