Sudani ya Kusini itaendesha kura ya maoni ili kuamua ikiwa iendelee kubaki kuwa sehemu ya Sudani ama la ifikapo tarehe 9 Januari 2011. Uwezekano ni mkubwa kuwa nchi hiyo kubwa zaidi katika bara la Afrika itagawanyika kuwa nchi mbili. Ufuatao ni mkusanyo wa makala za blogu kuhusu kura hiyo ya maoni.
Wa-Sudani Kusini 116,000 wameondoka kutoka Sudani ya Kaskazini tangu mwezi Oktoba mwaka jana, Maggie Fick anataarifu:
Wasudani ya Kusini 116,000 (na hesabu inaongezeka) wameondoka Sudani kaskazini tangu mwezi Oktoba mwaka jana. Ikiwa limesalia juma moja tu kabla kura hiyo ya maoni huko Sudani ya kusini kuanza, watu wanawasili kwa wingi katika miji mikuu ya Jimbo la kusini kwa kasi ambayo ni wazi inaongezeka kwa haraka.
Kwa nini Wa-Sudani ya Kusini wanakwenda kusini kwa idadi kubwa?:
Je ni kwa nini wakaazi wa kusini wanaendelea kumiminika kusini kwa idadi kubwa pamoja na kutokuwepo kwa uhakika wa mustakabali wao huko nyumbani? Kwa sababu wana sababu za kuhofia kama kweli haki zao zitaheshimiwa huko Sudani kaskazini kufuatia kura hiyo ya maoni.
Magdi El Gizouli anachambua hotuba ya Rais Omar Bashir kwa taifa wakati wa sherehe za kumbumbuku ya miaka 55 ya uhuru wanchi hiyo. Anasema, “Kuruhusu watu wa Kusini kuchagua mustakabali wake kwa mtazamo wa Bashir inamaanisha “mstari wa mwisho katika kitabu cha kupona kwa taifa”:
Kutoka kwenye jukwaa hili Bashir alizungumzia masuala matatu muhimu ya kipindi hiki, kujitenga kwa Kusini, mgogoro katika Darfur, madai ya upinzani ya kutizamwa upya muundo wa kisiasa huko Khartoum kufuatia kujitoa kwa Sudani ya Kusini. Kuhusu Kusini Bashir alitoa uchaguzi kati ya kujitoa kwa amani na umoja unaowezekana kwa vita kama mbinu ya kiwerevu na kidemokrasia dhidi ya mpasuko ulioshindikana katika uasili wake wa jumla. Kuruhusu Kusini kuchagua mustakabali wake katika fikra za Bashir kunamaanisha “mstari wa mwisho katika kitabu cha kupona kwa taifa”, kwa kuwa amani, ambayo ni shabaha kubwa ya utawala wake, kwa hakika ni sehemu ya kweli na muhimu ya uhuru wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Yobu Annet, eneo lenye utata la Abyei linaweza kukabiliwa na upungufu mkubwa wa bidhaa ikiwa sehemu ya Kusini itajitenga kwa kuwa bidhaa nyingi huja kutokea Kaskazini:
Jamii ya wafanyabiashara katika eneo la Abyei inaguswa sana – wengi wanadhani kujitenga kutaleta kuanguka kwa uchumi katika eneo hilo. “Kama Abyei itakuwa sehemu ya Kusini basi biashara ya mpakani inaweza kuathiriwa sana”, alisema Chol Mayen, mfanyabiashara. “Kama itatokea kwamba mpaka utafungwa kabisa, tunaweza bado kwenda Afrika Mashariki kufuata bidhaa.”
Kura ya maoni inasababisha hofu kubwa kwa wafanyabiashara wa nje huko Juba:
Kwa Birungi Mary, mfanyabiashara wa Kiganda anayeuza mboga katika soko la Juba, kura ya maoni inasababisha hofu. “Tunajiandaa kuondoka, na kisha kurudi baada ya kura ya maoni kama hakutakuwa na machafuko.”
Mary ni mmoja wa maelfu ya wafanyabiashara wa Juba, wengi wao kutoka nchi za jirani ambao wanashauku ya kujua kile ambacho kura ya maoni itakileta. Haku tayari wanateseka kwa mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, wengi wanahofu kwamba vurugu zinazohusiana na kura ya maoni zinaweza kuvuruga kabisa biashara na bidhaa za thamani zinaweza kuharibiwa.
Kwenye masoko ya Konyokonyo na Jebel huko Juba, wafanyabiashara wengi wakigeni walisema wanaenda nyumbani kwa sikukuu ya Krismas, na kisha watangoja mpaka zoezi la kura ya maoni limalizike ndipo warudi.
South Sudan Info imetengeneza mkusanyiko wa vichwa vya habari vya Sudani mwaka 2010:
Ndani ya siku 9, Wasudani Kusini wataelekea katika upigaji kura katika kura ya maoni ya kujiamulia kama waunde au wasiunde nchi mpya huru zaidi katika Afrika.. Mwaka uliopita ulikuwa ni mwaka wa alama, ya kuwa mwaka wa mwisho katika kipindi cha miaka sita ya makubaliano ya mpito ya amani kinachowaelekeza kwenye tarehe muhimu kabisa ya kura ya maoni ya Januari 9, 2011.
Mishaps na Mayhaps anaona kwamba kura isiyo na sababu nyingine yoyote isipokuwa kutengana si jambo ambalo wapigakura wengi wa Sudani ya Kusini watalivumilia:
Moja ya dalili nyingi mbaya zinazojitokeza huko Sudani ya Kusini wakati tunapoikaribia kura ya maoni, ni kuanza kuwa bayana kwamba kura ambayo haina lengo lolote lile isipokuwa kutengana si jambo ambalo Wasudani Kusini wengi watalivumilia. Bila ya shaka, pamekuwepo na miongo minne ya vita vilivyosababisha vifo vya mamilioni, lakini mchakato huu unaonwa na wengi ndani ya Sudani ya Kusini kama hatua ya mwisho katika njia ya kujitenga, badala ya fursa ya kujipambanua kwa kweli kama taifa.
Tazama viwasilishi vya picha vya Maggie Fick vya “Muda wa mwisho” kuelekea kwenye kura ya maoni ya Sudani ya Kusini:
Idadi tu ya mabango yanayohusiana na kura ya maoni katika makao makuu ya kusini inazidi kustahili kutizamwa. Mabango ya hivi karibuni kutoka kwenye Tume ya Kura ya maoni ya Sudani ya Kusini yanawasihi wapigakura kujitokeza tarehe 9 Januari. Mengi ya mabango haya makubwa kwa madogo hata hivyo, yanabeba ujumbe mmoja ulio bayana: kujitenga kunakuja. Alama hizi, zilizochorwa na muungano wa makundi ya jumuiya za kiraia, zina bendera ya Sudani ya Kusini na kiganja kimoja cha mkono kilichonyanyuliwa, ambayo ni alama inayoonekana kwenye makaratasi ya kura hiyo ya maoni.
Kwa wale wanaoamini katika maombi, ungana na Scott na Meg Rambo:
Je unataka kuungana nasi katika kuomba:
* kwa ajili ya amani kati ya Kaskazini na Kusini, lakini pia kati ya makundi mbalimbali ya kikabila.
* kwa ajili ya makubaliano ya amani katika maeneo yenye vurugu; mipaka yao na makazi yao
* kwa ajili ya mchakato sawia wenye amani na haki wa kura hiyo ya maoni.
* kwamba kanisa katika Sudani liendelee kuwa shuhuda na mtendakazi wa upatanishi
* kwa ajili ya upatanishi; kati ya Kaskazini na Kusini, kati ya serikali na waasi, kati ya makabila, na muhimu zaidi kati ya watu wa Sudani na Mwenyezi Mungu.