- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Tanzania: Majumuisho ya Habari za Uchaguzi Mkuu wa 2010

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uchaguzi

Mnamo tarehe 31 Oktoba 2010, Watanzania watashiriki katika uchaguzi wa Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar pamoja na Wabunge na Wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Huu ni mjumuisho wa yale yaliyojiri katika blogu mbalimbali kuhusiana na uchaguzi huo.

Tom Rhodes anaripoti kwamba [1] serikali ya Tanzania ilitishia vyombo vya habari kabla ya uchaguzi:

Hata kama vyombo vya habari vya Tanzania vinahisi kwamba viko huru kuripoti kuhusu mkabiliano mkali uliopo kwenye mbio za uchaguzi, hili ni jambo lingine. Kuchapisha habari zinazoikosoa serikali katika kipindi hiki nyeti lilionekana kuwa jambo lenye hatari kubwa hasa baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sethi Kamuhanda, kutembelea ofisi za vyombo mbalimbali vya habari mwezi uliopita, ambapo alitishia kuvifunga vyombo vya habari “vinavyochapisha habari zinazoifanya serikali ionekane katika mwanga mbaya,” televisheni ya taifa iliripoti. Zaidi ya asasi 50 za haki za binadamu na vyombo vya habari vilitoa tamko la pamoja wiki iliyopita, vikidai kwamba serikali imevitishia vyombo vya habari mapema kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika.

Tangu kampeni zilipoanza, Msajili wa Magazeti, shirika linalomilikiwa na serikali ambalo linasimamia utoaji leseni, limekuwa likiandika barua na kuzituma kwenye magazeti mbalimbali, na kuyaonya dhidi ya kuandika habari yoyote inayoonekana kuikosoa serikali, waandishi nchini humu waliiambia CPJ. Magazeti matatu ya kila wiki ya Mwanahalisi, Raia Mwema na Tanzania Daima, tayari yamekwishapokea barua hizo za onyo kwamba hayana budi kukwepa kuandika habari zozote ambazo serikali itaziona kuwa ni za “uchozezi” vinginevyo yanaweza kusimamishwa.

“Aina hii ya vitisho imekuwa jambo la kawaida kusikia kutoka kwa Msajili wa Magazeti, ambaye waziri wa habari humtumia kama chombo cha kuhakikisha waandanishi wanachuja na kujizuia kuandika habari fulani wao wenyewe,” mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, aliniambia.

Gazeti la Kiswahili linaloongoza kwa kuwa na wasomaji wengi, Mwananchi, hivi karibuni lilipokea barua mbili kutoka kwa Msajili huyo zinazotishia kulifunga kwa kuwa liliripoti habari ambazo ziliikosoa serikali, Mhariri Mtendaji, Theophil Makunga, alinieleza.

ZanziBits anasema [2] kwamba kutokuwepo kwa vurugu katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010 huko Zanzibar ni ushahidi kwamba watu wameanza kuipokea na kuielewa demokrasia:

Nyakati za uchaguzi katika miaka iliyopita, kulikuwa na vurugu za kisiasa huko Zanzibar wakati watu walipokuwa wanajiandaa na uchaguzi, lakini si hivyo safari hii. Kampeni yote imekuwayamani na usalama. Hizi ni dalili njema kwa nchi yetu, kwa sababu inaonyesha kwamba watu sasa wameanza kuipokea demokrasia na kwamba wameanza kujishirikisha katika mchakato wa kisiasa.

Kampeni zitakoma rasmi tarehe 30 Oktoba. Mnamo Oktoba 31, Watanzania watapiga kura kumchagua kiongozi wao mpya. Sisi sote tuna matumaini kwamba atakuwa kiongozi aliyechaguliwa kwa haki na atakayeiletea nchi yetu maendeleo. Zaidi ya yote, sote tuna matumaini kwamba uchaguzi utakuwa wenye utulivu kama zilizovyokuwa kampeni.
Mungu aibariki Tanzania na Visiwa vyake.

Labda Hata Mimi anaandika kuhusu [3]uchaguzi wa Tanzania na jumuiya inayokua ya teknolojia:

Hivi sasa kuna nyenzo ya kiteknolojia ya Ushahidi ili kuripoti matukio ya vurugu, fujo na mapigano katika tayari kwa ajili ya uchaguzi uatakaofanyika Jumapili. Unaweza pia kutuma maombi ya kuwa mfasiri wa kujitolea na mthibitishaji kupitia Fomu hii ya Google. Mpaka wiki iliyopita, moja ya kura za maoni kati ya nne inaonyesha kwamba upande wa upinzani unaweza kuwa na nafasi nzuri kushinda. Sitaki kupendelea chama chochote katika uchaguzi lakini ni matumaini yangu tu kwamba uchaguzi utaendeshwa kwa amani. Ni matumaini yangu pia kwamba rafiki zangu nchini Tanzania, Watanzania na Wamarekani vilevile, wote watakuwa salama. (Kama Pernille anavyoeleza, UCHAGUZI ni msukumo wa pamoja kati ya TACCEO, Tanzania; HIVOS, Uholanzi; HakiElimu, Tanzania; Jumuiya kubwa zaidi ya TEKNOHAMA nchini Tanzania – Jamii Forums, Tanzania; TWAWEZA ya Rakesh Rajani, CRECO ya Kenya kwa kushirikiana na USHAHIDI na SODNET za Kenya zote kama washirika wa kimkakati katika teknolojia.


Pernille anatangaza
kuzinduliwa kwa Uchaguzi Tanzania [4]:

UCHAGUZI, TZ ni jukwaa linalotumia tovuti ya USHAHIDI na zana za kiteknolojia za simu za mkononi, na hivyo kuwezesha ushirikiano ambao haukuwahi kuwepo kati ya waangalizi wa uchaguzi na raia katika kusimamia uchaguzi katika muda unaokaribiana na wakati halisi.

Hebu ijaribu – uchaguzi wa Tanzania utakuwa Jumapili hii, na litakuwa jambo la kufurahisha kuona jinsi zana hii inayowika itakavyochagiza upatikanaji taarifa katika tukio hili.

Mwanablogu wa Kenya, Chris, anauliza [5], “Je, kutatokea vurugu nchini Tanzania baada ya uchaguzi?”:

Jumapili hii, majirani wa Kenya, Tanzania, wanaingia katika uchaguzi. Ukweli ni kwamba Watanzania wamekuwa wakifuatilia kwa makini na pengine katika namna ya kuonea gere jinsi Kenya ilivyopitia matukio makubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Watanzania sasa wanajiuliza hivi kwa nini watu wa kawaida nchini humo wasiwe kama wenzao wa Kenya, yaani, wanawatazama kama watu wenye mwamko mkubwa sana katika kudai haki zao kiasi cha kuwa tayari kuzipigania.

Nilishtushwa hivi karibuni nilipowasikia baadhi ya Watanzania wa kawaida katika jiji la Dar es Salaam wakijadili kuhusu uchaguzi wa Jumapili ijayo na wakishauriana kwamba itakuwa vema kuhakikisha watu wanajiwekea akiba ya kutosha ya chakula majumbani, maana walikuwa wakitarajia matukio mabaya.

Anaendelea [5]:

Kwa Wakenya wengi (kama ilivyo kwa baadhi ya watu ambao huwa hawachoki kuchochea chuki za kikabila katika blogu hii) itakuwa vigumu sana kuelewa siasa za Tanzania. Ukabila si kitu chenye nafasi katika nchi hii ambayo ukubwa wake ni karibia ukubwa wa Kenya na Uganda pamoja na ambayo ina makabila yasiyopungua 140 (nchini Kenya ni makabila kiasi cha 40 tu). Wala hakuna historia ya kabila fulani kuwa ndiyo limetawala zaidi kuliko mengine. Mtu pekee ambaye hana budi kupewa sifa zaidi za kufanikisha umoja huu adimu katika nchi za Kiafrika si mwingine bali hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wakati ambapo Tom Mboya na Jomo Kenyatta wa Kenya walijivunia alama za kitaifa zilizo imara kama simba, Nyerere, alimchagua mnyama mkimya, Twiga. Na kuna ushahidi mwingi sana katika maisha ya mtu huyu kwamba aliweza mbali zaidi ya upeo kiasi kwamba pamoja na kwamba tayari yumo kaburini lakini ana nguvu kubwa katika maamuzi ya mambo mengi. Nyerere aliiunganisha nchi kwa kupigania sana lugha ya Kiswahili na kuifuma pamoja katika maisha ya kijamii ya Watanzania.

Jerry Okungu anawashauri Watanzania [6] kutoangukia katika mtego wa vurugu za uchaguzi kama zilizoikumba Kenya:

Magazeti matatu yanayochapishwa jijini Dar es Salaam hayawezi yote kuwa yamefanya kosa, na hasa mojawapo, tena la zamani zaidi na linalomilikiwa na CCM. Yote yanazungumzia kitu kimoja: kwamba kuna hali ya wasiwasi na mashaka inayotawala. Yote yanaelezea hisia kwamba uchaguzi wa nchi ya Bongo huenda ukakumbwa na wizi wa kura ili kukipendelea chama kinachotawala hasa kipindi hiki ambapo kunaonekana kuwa na shauku ya mabadiliko ya utawala katika nchi ya Mwalimu Julius Nyerere.

Dalili kwamba mambo si mazuri zinafanywa kuwa bayana zaidi hasa kupitia matokeo ya siku za karibuni ya kura za maoni zilizoendeshwa na Research and Education in Democracy in Tanzania(REDET), ambacho ni Kituo cha Utafiti kinachomilikiwa na Serikali na kinachopatikana pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Synovate ya Kenya na taftishi nyingine mbalimbali za mtandaoni kupitia Daily News, Uhuru na ThisDay la Bwana Reginald Mengi.

Siku chache kabla ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007, tulikuwa na hali inayofanana na hiyo ambapo matokeo ya tafiti za kura za maoni ziliibua malumbano ya chuki, madai na pingamizi za madai kwamba matokeo yalikuwa yamechakachuliwa vilivyotegemea tu ni nani na ni chama gani kilipendelewa zaidi au kilipuuzwa katika kura za maoni. Ilipotokea kwamba matokeo yalikipa nafasi chama cha PNU, basi vyama vingine na waungaji wao mkono vilipinga vikali na kudai ni matokeo ya kupikwa. Kwa upande mwingine, pale matokeo mengine ya utafiti yalipoonyesha kwamba ODM walikuwa mbele, basi wale nao walipinga vikali wakidai kwamba yalikuwa ya uongo.

Blogu ya VijanaFM inaorodhesha [7] miradi ya kibunifu ya kiteknolojia zinazohusisha utoaji taarifa wa mtu-kwa-mtu kuhusiana na masuala ya uchaguzi:

Wiki chache zilizopita tuliwaambieni kwamba tumeanzisha TZelect, ambalo ni jukwaa lililojikita kutumia Ushahidi ili kukusanya na kujadili ripoti kutoka kwa vijana wa Afrika Mashariki kuhusiana na matukio ya uchaguzi.

Hivi karibuni jukwaa linaloundwa na asasi kadhaa, Uchaguzi Tanzania, liliwasiliana nasi na inaonyesha kwamba inawezekana kuripoti kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno wa simu ya mkononi.

Majukwaa yote mawili, TZelect na Uchaguzi Tanzania, yamelenga uchaguzi huu unaofanyika Jumapili hii ya tarehe 31 Oktoba 2010, na vilevile mchakato wa muda mrefu zaidi wa viongozi walio madarakani kwa njia ya kuchaguliwa.

Hata hivyo, wakati ambapo Uchaguzi Tanzania imeundwa ili kupokea taarifa zinazoingizwa upya kila baada ya saa moja kutoka kwa umma nchini Tanzania, TZelect imeundwa ili kupokea mfululizo majadiliano ya uchambuzi kuhusu matukio ya uchaguzi, hasa yale yanayofanywa na vijana.

Mmarekani aliye nchini Tanzania anaandikakuhusu uzoefu wake baada ya kuhudhuria mkutano wa kisiasa ulioendeshwa na chama kikuu cha upinzani, CHADEMA:

Siku ya Alhamis nilihudhuria mkutano wa CHADEMA (Chama Cha Demokracia na Maendeleo au Party of Democracy and Development) cha Dakta Slaa, ambaye ni mgombea mwenye mvuto zaidi kwa upande wa upinzani Tanzania Bara. Licha ya ukweli kwamba hakufika na kwamba nilielewa tu kiasi cha asilimia 40 ya yale ambayo wagombea mbalimbali walikuwa wakiyaeleza kwa mtindo-wa-mhubiri-wa-KiAfrika kupitia vipaza sauti, kwa kweli lilikuwa jambo la kuvutia sana na la kufundisha mno. Nilijikuta nikipata marafiki wawili ambao ni walimu wa shule za sekondari na tulijadiliana (kwa Kiswahili!) kuhusu uchaguzi, historia ya Tanzania, na majukwaa na ahadi za vyama na wagombea mbalimbali.