Wanablogu wa Karibeani wanaomboleza kifo cha mmoja wa waasisi wa muziki wa soca katika kanda hiyo – Alphonsus Cassell, anayejulikana zaidi kama “Arrow” – na ambaye kibao chake kikali, Hot, Hot, Hot kinapewa sifa ya kuutambulisha mtindo wa soca kwa kadamnasi ya dunia.
Taarifa za habari zinathibitisha kuwa muimbaji huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani kwa muda; rambirambi za wanablogu zimekuwa na mguso pia zinaelezea masikitiko binafsi.
Mwanablogu One Tribe, Many Voices anatambua kuwa muziki wa mwanamuziki huyo ulikuwa ni muziki uliosindikiza maisha ya watu wengi wa Karibeani , na ametuma kiungo kwa wasomaji ili waweze kusikiliza:
Kwa wengi ambao hawaujui muziki wa Calypso, jina la Arrow linaweza kuwa halijulikani lakini kwa wale miongoni mwetu ambao wameucheza na kushereheka kuanzia Brooklyn mpaka Port of Spain si hivyo.
Arrow alileta vionjo vya aina yake kwa Kaiso (jina jingine la Calypso), vilikuwa ni vionjo vya kisiwa cha Montserrat. Arrow alijiweka yeye pamoja Montserrat katika ramani ya muziki mnamo mwaka 1982 kwa kibao chake kikali: ‘Hot, Hot, Hot’.
Ninakumbuka jinsi nilivyolowana jasho wakati wa tamasha la Carnival nchini Trinidad wakati Arrow alipoimba ‘Bills’, ‘Soca Rhumba’ na ‘Rub Up’. Upigaji wake wa muziki wa soca ulikuwa tofauti kidogo, ulikuwa na hisia za merengue na ulikuwa na mahadhi yanayovuka mipaka na kuijumuisha Karibeani yote. Mrindimo wake ulikuwa mzito na ulinikumbusha Karibeani iliyotawaliwa na Wafaransa pamoja na ile iliyotawaliwa na Wahispania. Matarumbeta yalitawala sana, yalishambulia bila kukwepeka.
Blogu ya The Caribbean Camera inaorodhesha mafanikio ya Arrow katika muziki, lakini pia inachungulia upande mwingine wa mtu huyu:
Arrow alianza kuchanganya muziki wa Calypso na mitindo mingine kama vile R&B, Zouk na salsa na mnamo mwaka 1982 alishirikiana na muandaaji muziki Leston Paul pamoja na bendi yake ya Multi National Force na kurekodi santuri ya ‘Hot Hot Hot.’
Jina la wimbo wa santuri hiyo ukawa ndio kibao chake kikali cha kwanza cha ki-Karibeani na kibao cha soca kilichouzwa zaidi ya vyote. Kiliasiliwa kuwa wimbo wa Kombe la Dunia la FIFA mwaka 1986 huko nchini Mexico, na baadaye ukapigwa tena na David Johansen (huku akitumia jina na nafsi bandia ya Buster Poindexter), Menudo, pamoja na Blabla & Kanchan.
Kadhalika Arrow alijiimarisha kama mfanyabiashara huko Montserrat, alimiliki duka la Arrow’s Manshop pale Plymouth. Wakati duka hilo lilipoharibiwa na mlipuko wa volkeno ya vilima vya Soufriere, akahamia Salem. Aliandaa tamasha la calypso la Harambee kisiwani humo mnamo mwaka 1996, ili kukabili uharibifu uliasababishwa na volkeno.
Arrow aliendelea kuwa mwanamuziki anayetafutwa sana huko Karibeani na hivi karibuni kabisa alitumbuiza katika ufunguzi wa Kombe la Dunia la mchezo wa Kriketi la mwaka 2007 pamoja na Shaggy, Byron Lee na Kevin Lyttle.
Na mwisho, kutoka visiwa vya St. Vincent na grenadines, Abeni anasema:
Alizaliwa katika kisiwa kidogo cha Montserrat, na kipaji cha Alphonsus ‘Arrow’ Cassell hakikuwa kidogo. Alitupatia vibao kama vile ‘Pirates’, ‘Long Time’ pamoja na kibao cha kutisha ‘Hot Hot Hot’. Ambacho kilifanikiwa zaidi kufuatia utengenezwaji wake mpya uliofanywa na Poindexter mwaka 1987. Miaka kadhaa baadaye, Kevin Lyttle anayetokea huko St Vincents naye alifurahia mafanikio ambayo hayakutarajiwa na kibao chake cha ‘Turn me on’. kwa hiyo, nadhani ni sawa nikisema kwamba Arrow alipalilia njia kwa wasanii wengine wa soca ambao waligundua kuwa muziki wa soca unaweza kuuzika katika masoko mengine yasiyo ya kitamaduni.
Nadhani nilisoma mwishoni mwa juma kwamba alisafirishwa kwa ndege kwenda Antigua kwa ajili ya matibabu. Leo (Tarehe 15 Septemba) nimefahamu kuwa alishindwa na saratani ya ubongo. Rambirambi zangu ziwafikie familia yake na watu wa Montserrat ambao wanaomboleza kifo chake. Na ikiwa italeta ahueni, nasema ataendelea kuwa ‘hot, hot, hot’.
1 maoni