Irani: Huenda Mwanablogu Aliyefungwa, Hossein Derakhshan (”Hoder”), Akakabiliwa na Hukumu ya Kifo

Chanzo cha kuaminika kimeifahamisha Global Voices kwamba mwendesha mashtaka huko Tehran analenga kuhakikisha kwamba mwanablogu aliyefungwa Hossein Derakhshan (anayefahamika pia kama “Hoder”) anapewa adhabu ya kifo. Jaji anayesimamia kesi hiyo, anayeitwa Salavati, bado hajatoa uamuzi katika kesi hiyo. Derakshan anashitakiwa kwa “kushirikiana na dola adui, kupiga propaganda dhidi ya utawala wa Kiislamu, kudhihaki utakatifu wa kidini, na kuandaa propaganda kwa ajili ya vikundi vinavyopinga mapinduzi.” Alikamatwa miezi 22 iliyopita, na kesi yake ilianza kusikilizwa mwezi Juni mwaka huu wa 2010.

The Sababu zilizosababisha kukamatwa kwa Hoder mara ya kwanza mara tu aliporejea nchini Irani akitokea Kanada mwaka 2008 bado hazifahamiki, lakini wengi walihisi kwamba safari mbili (zilizotangazwa sana kupitia vyombo vya habari) alizofanya kwenda Israeli huenda zikawa ndiyo sababu.

Derakhshan ana pasi ya Kanada, lakini Irani bado haitambui uraia wa nchi mbili, na kutembelea Israeli ni jambo ambalo linaichukiza sana na serikali ya nchi hiyo.

Jambo linalochanganya zaidi ni kwamba Hoder alipata umaarufu duniani kote kama mwanablogu anayeongoza huko Irani na mwanaharakati wa uhuru wa kujieleza (aliwahi hata kublogu kwa ajili ya Global Voices kati ya mwaka 2004 na 2005). Baadaye alibadili mbinu na kuandika habari zinazosifu sera za Rais Mahmoud Ahmedinejad hususan kwa msimamo wake dhidi ya serikali ya Marekani, silaha za nyuklia, Israeli, na hata kutovumilia upinzani wa umma unaofanywa na wanaharakati wa haki za binadamu.

Mwezi Aprili mwaka 2009, Rais wa Irani, Ahmedinejad, aliandika barua akitaka kesi ya Hossein Derakshan ishughulikiwe haraka na kwa kuzingatia sheria. Serikali ya Kanada bado haijatoa msimamo wake hadharani kuhusu kesi ya Derakhshan. Mara baada ya kukamatwa kwake mwaka 2008, wanaharakati wa uhuru wa kujieleza wa mtandaoni walianzisha blogu ya Kudai Hoder Aachiewe Huru.

Kupitia Twita, Sanam Dolatshahi alituma twitakuhusu habari za uwezekano wa kuwepo na adhabu ya kifo, vilevile kuna tovuti moja ya Uajemi inayojulikana kama Kamtarin ambayo nayo imetaja uwezekano huo, ikizingatiwa kwamba licha ya minong'ono iliyokuwepo hapo kabla kwamba Derakshan alikamatwa kwa “ujasusi” nchini Israeli , lakini ni wazi kwamba hii si moja kati ya makosa ambayo kwayo mwendesha mashtaka anataka itolewe adhabu ya kifo.

Katika blogu iliyoanzishwa na familia ya Derakshan, Edalat Baraye Hossein Derakhshan(ikiwa na maana ya Haki kwa ajili ya Hossein Derakshan) bado hakuna taarifa mpya zinazohusiana na taarifa hii. Makala ya mwisho kuchapishwa kwenye blogu hiyo ni ile ya tarehe 15 Agosti, na ambayo ilieleza kwamba kesi ya Hossein ilimalizika wiki kadha za nyuma [Fa]:

Bado tunasubiri hukumu. Hajapata hata likizo ya wiki moja kutoka gerezani kuja nyumbani … Hii ni Ramadhani ya pili ambayo hajakuwa nyumbani … Alitueleza kwamba ubora wa chakula kule gerezani umeongezeka kidogo tangu Ramadhani iliyopita … Mama yake ana wasiwasi sana … Inasemekana kwamba katika mwezi huu Mungu hujibu dua kwa urahisi zaidi … Tafadhali msimsahau Hossein wetu.

Mwanablogu wa Irani anayejulikana kama Z8tun alihitimisha [fa]hali halisi ya mambo yapata miaka miwili iliyopita:

“Raia wengine wa Irani wamewahi kukamatwa kwa kuingia nchini Israeli, lakini waliachiwa saa chache baada ya mahojiano. Wapo wanaodhani kwamba Derakshan, ambaye katika miaka ya karibuni alitokea kuwa mwungaji mkono wa serikali ya Rais Ahmedinejad, alikamatwa kwa sababu aliwakashifu viongozi wa kidini nchini humu. Yeye mwenyewe ameeleza kupitia vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, licha ya kuwepo kwa ushahidi mwingi wa wanablogu waliotupwa gerezani, kwamba hakuna anayekwenda jela nchini Irani kwa sababu ya yale wanayochapisha kwenye blogu zao.”

Katika miaka ya karibuni, Jamhuri hii ya Kiislamu imetumia nguvu kuvunjilia mbali ulimwengu wa blogu, na wapo wanablogu kadha kwenye magereza ya Irani akiwemo mwanaharakati wa haki za binadamu Shiva Nazar Ahari. Mnamo tarehe 18 Machi mwaka 2009, Omid Reza Mir Sayafi alikuwa mwanablogu wa kwanza kuuwawa katika mazingira ya kutatanisha katika gereza nchini Irani.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.