Brazil: Uchaguzi Safi kwa Mtindo wa “Jifanyie Mwenyewe”

[Makala hii ilichapishwa kwanza kwenye blogu ya Ushahidi's. Ushahidi ni zana huria ya kupanga taarifa ambayo iliendelezwa huko nchini Kenya wakati wa machafuko ya mwaka 2008 na imekuwa ikitumika kwa ajili ya ukusanyaji taarifa moja kwa moja kutoka kwa raia.]

Watoto wa shule wanaambiwa na waalimu wao waimbe majina ya wagombea uchaguzi. Watumishi wa serikali wanafukuzwa kazi kwa kutowapigia kampeni viongozi wao wa kisiasa. Mabati ya kuezekea yananunua kura. Taarifa binafsi za wapiga kura zinauzwa wazi wazi kwa wapiga kampeni. Vitisho vya kuuwawa vinatumwa kwa wale wanaopinga vitendo vichafu vya uchaguzi.

Karibu kwenye upande usiovutia wa kampeni za uchaguzi nchini Brazil.

Hizo ni baadhi tu ya taarifa zinazotoka katika mradi wa Eleitor 2010, mradi wa “vyanzo vya habari vya kiraia” ambao una lengo la kuratibu taarifa za raia zinazoripoti ukiukwaji wa mchakato wa uchaguzi nchini Brazil.

Katika demokrasia kubwa zaidi huko kusini mwa bara la Amerika – katika nchi yenye wapiga kura zaidi ya milioni 120 – mwaka huu, wapiga kura watakwenda kwenye uchaguzi kumchagua kiongozi atakeyemrithi mmoja wa marais maarufu zaidi katika historia (Luiz Inácio “Lula” da Silva) na pia watawapigia kura magavana, ambao wanajaza sehemu kubwa ya bunge la Kongresi.

Tovuti ya Eleitor2010

Kila nchi ina utamaduni wake wa kipekee wa kisiasa pamoja na kawaida zake. Hata demokrasia ndogo (ya ki-ishara) huwa taratibu zake katika mchakato wa uchaguzi, namna upigaji kura unavyoendeshwa, na uhakikishaji kuwa serikali inaratibu mchakato wa uchaguzi.

Brazil ilikuwa ni moja kati ya nchi za kidemokrasia za kwanza kutumia mashine za umeme za kupigia kura. Kadhalika upigaji kura ni sharti la lazima kwa kila mwananchi. Lakini pande nyingine za mchakato wa uchaguzi ni za kipekee, pamoja na jitihada za kudhibiti kampeni za kwenye mtandao wa intaneti, ununuaji kura na kile kinachoitwa “showmícios” (au matamasha ya kampeni).

Brazil ina sheria zilizo wazi na timilifu ambazo zinadhibiti uchaguzi klakini tatizo lipo kwenye utekelezaji wa sheria hizo.

Kuna utamaduni hai wa wanasiasa wa kupindisha sharia, huku wakidumisha nafasi zao za upendeleo kama wafadhili wa wapiga kura nchini Brazil. Jambo hili linatokea katika historia ya ukoloni huko nyuma pamoja na ukosefu wa usawa usiokwisha, ambao kwao maslahi ya viongozi yanaendelea kujidumisha

Wazo lililo nyuma ya mradi wa Eleitor 2010, ambao ni mradi wa kujitolea, usiofungamana na chama chochote na uanoendeshwa na timu ya kwenye mtandao isiyo na ufadhili wowote wa kifedha, ni kuwashirikisha wapiga kura zaidi ya siku siku ya uchaguzi. Kwa mujibu wa waanzilishi, Paula Goes na Diego Casaes – ambo walikutana kwenye Twita na ambao hivi sasa wanashirikiana kwenye mradi wa Global Voices Online, mradi huo una nia ya kukuza uraia hai na wenye jicho la uchunguzi, uraia ambao unachabanga baadhi ya mazoea yasiyo ya kidemokrasia na yasiyoeleweka kama ilivyoelezwa hapo juu.

Mradi wa Eleitor 2010 unatumia programu huria ya Ushahidi, jukwaa la kwenye mtandao ambalo liliangaliwa kwa karibu na watu wengi kutokana na ufanisi wake katika upangaji wa taarifa katika ramani baada ya tetemeko la ardhi huko nchini Haiti, ambao ulifanikishwa na jumbe fupi za simu za mkononi (SMS) kutokea katika maeneo ya tukio.

Mpaka sasa jukwaa la Ushahidi bado halijafikia upeo wake kama jukwaa la ufuatiliaji uchaguzi, wanasema Goes na Casaes. Huku takriban 25% ya nchi inatumia mtandao kila siku, na moja ya nchi zenye watumiaji wa simu za mkononi wengi zaidi katika Amerika ya Latini, wanatumaini kwamba Brazil itakuwa ndiyo sehemu ambapo (ushahidi) itafikia upeo wake mwaka huu. Majuma manne kabla ya uchaguzi, Eletoir 2010 tayari ina taarifa 239+, kutoka kila jimbo nchini humo, na kutoka katika maeneo pweke ya mbali.

Hata hivyo, ni mapambano magumu kueneza ujumbe kuhusu jukwaa hili, katika nchi ambayo vyombo vya utangazaji na magazeti bado vina nguvu sana, na bado vimo mikononi mwa vigogo wachache ambao wana nia ya ketetea maslahi yao.

Pamoja na hayo, timu ya mawasiliano ya eleitor 2010 imeweza kuvivutia vyombo vya habari, na ushirikiano na miradi mingine ya uwazi kwenye mtandao umekuwa ni wa muhimu. Hivi karibuni Google iliuchapisha mradi wa Eleitor 2010 katika ukurasa wake unaoandika habari za uchaguzi wa Brazil.

Goes na Casaes wanatumaini kuwa kutokana na kapeni yao ya kuelimisha umma – kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo Orkut yenye watumiaji zaidi ya milioni 40, ubia na mtandao wa wenye migahawa ya intaneti, Asasi zisizo za kiserikali, na vyama vya wananchi – mradi wa Eleitor 2010 utafanikiwa na kubadilisha namna ambavyo maelfu ya wapiga kura hujihusisha na mchakato wa uchaguzi.

Kwa kupitia jukwaa hilo, simulizi kadhaa za kuburudisha zimeshaanza kujitokeza, muda mrefu kabla ya uchaguzi wa Oktoba 3.

Wapiga kura walimkamata mtu mmoja kwenye mji fulani mdogo akiuza akaunti za Twita zenye wafuasi zaidi ya 40,000 Kitendo hiki ni kinyume cha sheria ya uchaguzi nchini brazil. Alipokabiliwa, mtu huyo alitoa ushahidi uanomtia hatiani zaidi, na kasha yake alitishia kuishtaki Eleitor 2010. Ushahidi huo, zikiwemo picha za kiperuzi na maandishi ya maongezi, vilipelekwa kwa mahakama ya uchaguzi.

Taarifa nyingine ya kuchekesha inatoka Sao Paulo, ambako waalimu katika shule moja, kinyume cha sheria waliwahamasisha watoto waimbe kwa ajili ya wagombea wawili, mmoja kwa ajili ya kiti cha Umeya na mwingine kwa ajili ya kiti cha Urais, lakini kitendo hicho kiliwaridia bila mafanikio pale ambapo watoto walipoanza kuimba “Lula!” “Lula!” Video hiyo ilisambaa sana na imeshaangaliwa mara zaidi ya 70,000.

Video nyingine ambayo iliwashangaza watu ilikuwa ni ile ya mwanablogu Ricardo Gama wa basi la VW linalomilikiwa na Ukumbi wa jiji lilipotumiwa kwa ajili ya kampeni mjini Rio De Janeiro. Mwanablogu huyo alipiga kele akisema “je mnabeba propaganda za kampeni ndani ya gari la ukumbi wa Jiji? Hili ni kosa katika uchaguzi! Nimepiga filamu. Nitawashitaki.”

Kutokea kaskazini mwa Brazil, katika jimbo la Maranhao, Eleitor 2010 ilipata habari kuwa mtandao wa makanisa ya kiinjilisti ulikuwa unataka “kuuza” kura 3000 kwa ajili ya kusaidiwa baada ya uchaguzi. Katika jimbo la Sao Paulo, Askofu mmoja aliwasihi waumini wasimuunge mkono mrithi aliyeteuliwa na Rais Lula, Dilma Roussef.

Mifano hii inaonyesha jinsi gani jukwaa hili pamoja na zana shirikishi za kwenye mtandao zitakavyoweza kutumiwa katika miaka ijayo.Bila kujali kama (zana hii) itasambaa haraka “kama virusi” na kujulikana sana, Eleitor 2010 pamoja na zana nyingine za uwazi vimeshakuwa nguvu ya mabadiliko katika mwaka huu wa uchaguzi.

1 maoni

  • Makala nzuri sana. Inaakisi vizuri yale yanayotokea hivi sasa nchini Tanzania – kampeni za kisiasa za kuwania kiti cha urais, nafasi za ubunge na zile za udiwani. Tunahitaji harakati za mtandaoni zaidi ili kuhakikisha kwamba haki na amani vinalindwa katika kipindi cha kampeni, wakati wa upigaji kura na baada ya kupiga kura. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.