- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Malaysia: Je, Uhuru wa Habari Unaelekea Wapi Sasa?

Mada za Habari: Asia Mashariki, Malaysia, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza

Je, ni nchi ipi katika orodha hii ambayo imepotea njia? Tanzania, Uganda, Zambia na Malaysia. Sawa, tuchukulie kwamba mimi ni mwandishi mtukutu ambaye niko kama ninataka kukashifu ufahamu wako wa jumla kuhusu nchi mbalimbali unazozijua. Kwa hiyo, Malaysia ni moja ya nchi zenye uchumi mzuri katika eneo la Kusini Mashariki ya Bara Asia, ina miundo mbinu iliyojengeka zaidi, ina kiwango cha chini cha umaskini, aaaah… unaweza kusema kwamba ina demokrasia zaidi pia. Lakini, ama kwa hakika ni nchi iliyopotea njia, maana Malaysia inaangamia tena chini ya Tanzania, Uganda na Zambia hasa katika kushika nafasi gani kwenye masuala ya uhuru wa vyombo vya habari [1].

Kama matukio ya uhuru wa vyombo vya habari yanavyozidi kujiri nchini Malayasia, kuna masuala 3 yanayojitokeza bayana:

1) Vyama vya siasa vya upinzani vitaongeza upinzani wao kupitia vyombo vya habari vya mtandaoni, baada ya kupewa nafasi finyu katika vyombo vya habari vya magazeti na televisheni.

2) Licha ya kuwepo madai au ushahidi wa kuunga mkono uwepo wa vyombo huru vya habari, bado serikali inaendelea kuwa na mkono wenye nguvu katika udhibiti wa vyombo vya habari hasa kupitia sheria za utoaji habari na upigaji chapa.

3) Uchujaji wa habari hauwezi kuwa na nguvu iwapo mawasiliano ya Intaneti yatabaki bila kuchujwa. Idadi inayokua ya watumiaji wa Intaneti na uandishi ulio huru wa mtandaoni ni mambo yatakayokuwa na athari katika ushawishi wa umma na kuiweka serikali chuni ya shinikizo.

Mapema mwaka huu yalipotoka matokeo ya upimaji uhuru wa vyombo vya habari, wanasiasa wa upinzani [2] walikuwa wa kwanza kutoa maoni yao kupitia tovuti za uenezaji habari za vyama na blogu zao. Ukosoaji wao wa mtandaoni uliongezeka sana hasa baada ya serikali kuchelewesha uamuzi wa kuleta upya majarida ya upinzani [3], na kufungiwa kwa vibonzo vya kejeli za kisiasa; huku mambo yote hayo mawili yakichochea hali ya kutoridhishwa kwa watu na upekenyuzi kupitia vyombo vya habari vya mtandaoni. Raia mmoja, Lai alijibu akisema [4]:

Sababu iliyotolewa na serikali, amini usiamini, ni kwamba ‘yaliyochapishwa yanaweza kuwafundisha watu kukaidi dhidi ya viongozi na sera za serikali'…Vibonzo (katuni) vinaweza kusababisha watu kuasi? Ala, kumbe! Hii ni silaha mpya iliyogunduliwa, au siyo?

Halafu, jambo la kuvutia, licha ya mkakati wa kutumia vyombo vya habari vya mtandaoni kukosoa uchujaji habari, moja ya majimbo yanayo ongozwa na upande wa upinzani liliamua, kwa hakika, kupeleka bungeni muswada wa sheria ya Uhuru wa Habari [5] ili kuweka wazi taarifa kwa manufaa ya umma kwa kila mtu. Anil alisema [6] wakati akimkaripia mwakilishi wa serikali ya jimbo hilo aliyeukataa muswada huo:

Leo ni siku ya kihistoria katika nchi hasa tunapotaka kuwa na jamii ya watu wanaowajibika zaidi …

Kadiri tovuti za vyombo huru vya habari na vile vya kiraia vinavyozidi kuchapisha taarifa zaidi nchini hapa, Gopal Krishnan alitabiri [7]:

Licha ya kuwepo majibu haya ya kimabavu dhidi ya sauti mbadala, kwa hakika, serikali haina budi kuutambua ubatili (bila kutaja matokeo ya kisiasa) wa kuendelea kubana uwepo wa fursa kwa uandishi wa habari na utoaji maoni ulio huru. Mpaka kufika mwaka 2009, zaidi ya asilimia 65 ya nyumba nchini Malaysia tayari zilikuwa zimeunganishwa na mtandao wa Intaneti. Zaidi ya jambo hili, siyo tu kwamba tumeshuhudia kuchipuka wa vyombo vidogovidogo vya habari vya mtandaoni na vyanzo vikishindana katika kuchukua muda tunaotumia mtandaoni, kumekuwa na mfumuko wa uandishi wa habari wa kiraia wa mtandaoni na vyombo vya habari vya kiraia, ambavyo, vyote kwa pamoja kwa kweli vimeunda ukweli mmoja mpya wa kisiasa nchini.

Hatimaye, uhuru wa vyombo vya habari si kitu ambacho serikali au vyama vya upinzani vinaweza kujiamulia, lakini linahusu raia wanaodai kupata ukweli na waandishi wanaotaka kuripoti kuhusu ukweli. Kama Attan alivyosema [8]:

Kama nilivyosema, hata kuwe na nini, sisi waandishi wa habari ndiyo tutakaopoteza – serikali ya Najib inazidi kuyafungia magazeti, Guan Eng (kiongozi wa chama cha DAP) anayapiga marufuku, huku Anwar akituburuza mahakamani.