Afrika Kusini: Wanablogu Wajadili Hukumu ya Mkuu wa Zamani wa Jeshi la Polisi

Hakuna shaka kwamba makosa ya jinai ni doa katika mafanikio ya Afrika Kusini tangu kuzaliwa kwa demokrasia mwaka 1994. Ni suala ambalo linawaathiri Waafrika Kusini wote, bila kujali wapi wanaishi na wao ni akina nani. Kwa hiyo, ilitokea kwa kutarajiwa kwamba mashitaka na hatimaye kuhukumiwa kwa Jackie Selebi, former Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Taifa na Rais wa zamani wa Polisi wa Kimataifa (Interpol), kungevutia hisia za wengi.

kama ilivyoripotiwa na Bloomberg:

Jaji Meyer Joffer alibaini kwamba Selebi, Rais wa zamani wa Polisi wa Kimataifa (Interpol), alipokea mamia ya maelfu ya randi kwa ajili ya malipo mbalimbali kati ya mwaka 2000 na 2005 kutoka kwa wafanyabiashara watatu, ikiwa ni pamoja na mtuhumiwa na mauaji Glen Agliotti, malipo ambayo “hayakuleta maana yoyote kama biashara halali kwa mujibu wa sheria” na yalikusudiwa kuwa kama rushwa. Selebi alituhumiwa kuwa na uhusiano na ‘genge’ ambalo linafanya biashara ya kusafirisha watu, madawa na bidhaa za wizi, kwa mujibu wa hati ya mashitaka.

Hukumu ilihitimisha uchunguzi wa karibu miaka mitano ya kikosi ambacho sasa kimevunjwa cha kuapambana na uhalifu nchini Afrika Kusini kinachojulikana kama Scorpions. Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki alishutumiwa na baadhi ya watu kwa kuchelewesha mchakato huo mzima. Ingechukua miaka mingine 2 na mashinikizo mengi ya kisiasa kumfanya Mbeki kujiandaa kumshtaki rasmi afisa wake wa polisi wa ngazi ya juu. Hii iliwafanya wengi wajiulize kwa nini Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Afrika Kusini alikuwa analindwa na rais.

Habari hizo ziliamsha maoni mengi na hata maswali zaidi kutoka kila pembe ya Afrika Kusini. Vyama vya Upinzani vya Afrika Kusini vilipongeza hukumu hiyo kama maendeleo chanya. Chama rasmi cha upinzani, cha Democratic Alliance hata hivyo kilionyesha:

Matokeo ya kesi ya ufisadi ya Jackie Selebi kwa hakika ni maendeleo chanya, kwa sababu yameonyesha kwamba sio wanasiasa wote waandamizi wa chama cha ANC wapo juu ya sheria. Hata hivyo, kesi hiyo kwa kuangalia nyuma lazima isaidie kuonyesha masuala mawili: kwanza, wajibu mkuu uliofanywa na Kurugenzi ya Operesheni Maalumu (Scorpions), ambayo kwa utata kabisa ilisambaratishwa mwaka jana, kwa kuanzisha uchunguzi dhidi ya wanasiasa; pili, tatizo sugu la sera iliyoshindwa ya ANC ya kuwapa kazi au madaraka makada wake.

Baadhi kama Ray Hartley wana mtazamo wenye mashaka:

Hukumu ya Selebi ni, kwa kuitazama juu juu, ushahidi kwamba mfumo wa sheria za uhalifu kwa mara nyingine unaonyesha uimara wake linapokuja suala la uhalifu unaofanywa na wanasiasa waandamizi.
Lakini si rahisi hivyo. Selebi ni mtu aliyepitwa na wakati, mteule wa Thabo Mbeki ambaye hapati tena kinga ya kisiasa inayotolewa na wale waliokalia ofisi nyeti katika serikali na chama cha ANC.

Pierre de Vos pia anatupa mwanga kwenye masuala mengine yanayoibuka kutokana na shitaka hili:

Hukumu lazima iweke alama ya kuuliza dhidi ya vitendo vya rais wa zamani Thabo Mbeki, aliyemteua Selebi, mwanzoni alichukua hatua zilizokuwa na lengo la kumlinda Selebi na akadai kwamba hapakuwa na ushahidi wa makosa kwa upande wa Selebi hata baada ya Mbeki kupewa taarifa fupi na Mkurugenzi wa Taifa wa Mashitaka ya umma (NDPP) kuhusu ushahidi dhidi ya ofisa huyo wa zamani wa polisi.
Kwa nini Mbeki alisisitiza kuwa Selebi asitiwe nguvuni? Kwa nini Mbeki alituomba tuwe na imani naye kwa suala la Selebi na kwa kwa nini alishikilia msimamo – pamoja kuwepo kwa ushahidi mzito na wa wazi aliopewa – kwamba hapakuwa na ushahidi wa kuonesha kwamba Selebi alikuwa mhalifu? Kwa nini alimteua mtu huyu awali ya yote? Je, hii haionyeshi – hata kwa kiwango cha chini kabisa – ukosefu wa busara katika maamuzi kwa upande wa rais wetu wa zamani?

Sarah Britten alitoamaoni yanayofanana na hayo:

Hukumu ya Selebi ni msumari mwingine katika jeneza la uadilifu wa Thabo Mbeki

Iluvsa aliuliza:

Suala zito zaidi linaloikabili nchi hii leo baada ya shitaka la Selebi na hukumu yake kwa mashitaka ya ufisadi ni hili: nani atamfuata huko jela? Linaloleta uzito zaidi ni hili: nani atamfikisha mahakamani mwanasiasa huyo kigogo?

Labda hilo ndilo suala zito zaidi sasa. Demokrasia changa ya Afrika Kusini iko shakani kushindwa ikiwa suala la ufisadi halitashughulikiwa. Mfumo wa sheria wa nchi hii umeonyesha kwamba unaweza kufanya kazi ikiwa pana utashi wa kisiasa. Pierre de Vos kwa mara nyingine tena anasema:

Utashi wa kisiasa ni ufunguo wa kupambana na ufisadi. Kama tutaona kesi za vigogo wa mashirika binafsi na ya umma wakiletwa mahakamani, tutaona kwamba utawala wa Zuma uko makini katika kutokomeza ufisadi. Kama hatutaona, tutajua kwamba (utawala huo) umeoza mpaka kwenye kiini.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.