Mashabiki wa soka kote ulimwenguni walikusanyika kwenye kumbi za baa na migahawa ili kushuhudia mechi ya fainali za Kombe la Dunia usiku wa Jumapili iliyopita. Nchini Uganda usherehekeaji huu ulikatishwa pale milipuko ya mabomu iliposambaratisha maeneo mawili maarufu kwa sherehe za mpaka majogoo jijini Kampala, mji mkuu wa nchi hiyo.
Mpaka sasa vyombo vya habari nchini Uganda vimeripoti vifo zaidi ya 70, huku dazeni kwa dazeni wakiwa wamejeruhiwa vibaya kutokana na milipuko hiyo. Polisi wa Uganda wameeleza kwamba huenda milipuko hiyo imefanywa na kikosi cha wapiganaji wa Ki-Somali cha Al-Shabab. Mmoja wa makamanda wa juu wa kikosi hicho hivi karibuni alitaka Uganda ishambuliwe kwa kuwa imepeleka wanajeshi wake katika kikosi cha kulinda amani nchini Somalia. Kundi hilo limepongeza kutokea kwa milipuko hiyo lakini hakikusema kama kinahusika nayo ama hapana.
Mwanablogu wa Uganda Gay Uganda anaandika:
Uganda imeshambuliwa. Kwa kusema kweli ni ubinadamu ndiyo ulioshambuliwa. Je, nani anaweza kuthubutu kuwa na furaha kufuatia ukatili mkubwa kama huu? Mpaka sasa ni wapiganaji wa Ki-Somali ndiyo wanaofurahia. Wanafurahi kwa sababu wanapambana na vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somali, vikosi hivyo vimewazuria wapiganaji hao kuanzisha dola la Kiislamu lenye kuongozwa na Sharia ya Kiislamu.
….Ninachokiona ni raia wenzangu, binadamu ambao kikubwa walichokuwa wanakifanya ni kutazama mechi ya kandanda ambapo wengi wao wameuawa na wengine kujeruhiwa, wamefanyiwa hivyo kwa fikra na njozi ambazo pengine wala hawakuwahi kuziwazia, yaani vitendo ambavyo wala hawawezi kuvitawala au kuwa na ushawishi navyo.
Ernest Bazanye anatahadharisha kwamba pengine watu wasifanye haraka kuhukumu kwamba nani hasa alitega na kulipua mabomu hayo, bado ni mapema mno:
Ni mapema mno kusema nani anahusika na kwa nini, hata kama kuna minong'ono huko nje ya nchi kwamba kitendo hicho cha kuua watu kwa mabomu kilifanywa na kundi la Al-Shahab, ambalo ni kundi la magaidi huko Somalia. Bila shaka mpaka sasa tumeshakomaa vya kutosha kuelewa kwamba kwa kawaida ukweli hauji haraka hivyo, kwamba bado ni mapema mno.
Trevor Snapp, ambaye ni mpiga picha mtengeneza makala za maoni na anayeishi Kampala, alikwenda Hospitali ya Mulago, mahali ambapo waathirika wengi wa mabomu hayo walipelekwa mara baada ya milipuko. anaandika:
Wanafamilia walimiminika kuelekea sehemu ya mapokezi wakati ambapo madaktari na miili iliyojaa damu walikimbizwa na kutolewa katika chumba cha upasuaji. Katika ukumbi wa kuelekea chumba cha upasuaji kulikuwa na mwili umelala sakafuni, damu zilikuwa zikimiminika kutoka kichwani, ilikuwa vigumu kusema kama alikuwa bado yungali hai au alikwishakufa. Hatua chache kutoka hapo, katika chumba kidogo cha kuhifadhia vifaa vya madaktari, wahudumiaji walipageuza kuwa mahali pa kuhifadhia miili ya watu, kulikwa na miili 6 iliyokuwa imelazwa sakafuni, baadhi ya maiti nguo zikiwa zimechanwachanwa na nguvu ya milipuko. Miili yote ilikuwa ya vijana.
Wanablogu wengi wameshtushwa kwamba milipuko hiyo imetokea Kampala, jiji ambalo linafahamika kwamba ni moja ya majiji makuu yaliyo salama zaidi barani Afrika. Joshua Goldstein, a mwandishi wa zamani wa Global Voices ambaye aliwahi kuishi Kampala, anaelezea maeneo mawili ambapo milipuko ilifanyika:
Klabu ya Mchezo wa Rugbi ya Kampala ni Baa iliyo na eneo kubwa la wazi, iko pembezoni mwa kiwanja, mahali hapa wanapenda sana kuja wanafunzi wa vyuo ambao huja hapo kurandaranda na marafiki zao. Kama Uganda ingekuwa na makundi fulani ya kiitikadi basi hapa ndiyo mahali ambapo wangefika kufanya sherehe zao. Hapo ni mahali ambapo watumiaji hujipatia vinywaji vyao maalumu vya Nile huku wakisindikizwa na muziki wa mbali wa rege pamoja na hip hop. Katika siku za mwisho wa juma ni makundi ya watu wa aina hiyohiyo ambao huja kutazama ragbi,huku kola zao zikiwa zimenyanyuliwa juu ili kujikinga na jua.
….Upande mwingine wa jiji kuna Kijiji Cha Ki-Ethiopia, upande wa chini wa mtaa kuna Ubalozi wa Marekani, hapa ni katikati kabia ya Kabalagala, ambayo inaweza kuitwa ndiyo Las Vegas ya Kampala. Mgahawa, upo upande wa juu wa kiasi cha nusu dazeni au zaidi kidogo ya mighahawa ya Ki-Ethiopia ndani ya kiasi cha mita 500, ipo katikati ya makutano ya Barabara ya Ggaba na ile ya Tank Hill. Nyakati za Mchana waandishi wa habari wa Ki-Ethiopia waliokimbia kwao hupoteza wakati wao kwa kutafuna miraa na kubadilishana habari za matukio ya siku hiyo. Nyakati za usiku, eneo lote huchangamka kwa mwanga wa taa zinazotoka kwenye baa na mitoko ya usiku.
Sleek anaandika:
Kutoa picha kamili kwa tukio hili zima, nitasema kwamba mpaka sasa, Kampala imekuwa moja ya sehemu zile ambazo mtu anaweza kutembea mpaka hata saa 9 usiku kutoka upande mmoja wa mji hadi mwingine. Na kwamba sisi ni aina ile ya watu ambao hulalamikia kuongezeka kwa bei za mafuta, kodi zilizo juu za Lipa Kadiri Unavyopata, gharama za juu ya upigaji simu … kwa ujumla ni gharama zilizo juu ya maisha. Lakini pamoja na hayo bado mtu anamudu kwenda sehemu ya burudani na kulipa walau Shilingi za Uganda 5,000 ili kujipatia bia. Na huwa tunajazana kwenye sehemu hizo mpaka mtu unapata shida kupita ili kujinunulia kinywaji. Na hapo tunazungumzia nyakati zile ambazo watu hujazana wa kiwango cha wastani.
Na kisha mara unasikia milipuko ya mabomu …
2 maoni
Je,mbona al-shabab inaua wasio na hatia?baadaye itatawala miti au maiti?
Vitendo vya ugaidi vinazidi kuongezeka barani Afurika na mamiliyoni ya watu wanapoteza maisha yao kila siku.Wanaafurika wenzangu hamuoni kwamba tumekosa umoja kweli?Wanablogu wenzangu,vitendo vya unyama vya tarehe 11 julai nchini Uganda,vimenivunja moyo sana.Wanamgambo wa AL-shabab wamejigamba kuhusika na ubabe ule,vingozi katika mkutano wa kimataifa baraani afurika,katika mkutano wa kilele wamepinga vikali shamburio hilo,lakini nauliza waafurika,ni lini vita vya wenye kwa wenyewe vitamalizika?Ndugu zangu,dunia inakabiliwa na mabaya mengi miongoni mwa hayo kuna mabadiliko ya hali ya hewa,mbona nguvu zenu zinaishilia katika mapigano?Ni vyema kutumia nguvu hizo kushughurikia mazingira.Al-shabab badirisheni msimamo huwo,na muingie katika mazungumzo baina yenu na serili ya somalia.Waafurika nasi tutafutie amani baara letu.Asanteni.