Thailand: Vurugu Zinazotokana na Ujumbe Mfupi wa Maneno wa Waziri Mkuu

Mnamo Disemba 18, 2008, mamilioni ya wateja wa simu za viganjani wa Thailand walipokea ujumbe huu kutoka kwa Waziri Mkuu mpya Abhisit Vejjajiva:

“ผมนายกรัฐมนตรีคนใหม่ ขอเชิญท่านร่วมนำประเทศไทยออกจากวิกฤติ สนใจได้รับการติดต่อจากผมกรุณาส่งรหัสไปรษณีย์ 5 หลักของท่านมาที่เบอร์ 9191 (3 บ.)”

“Mimi, Waziri Mkuu mpya, ninakualika kushiriki kuitoa Thailand kwenye mgogoro. Kama unapenda kuwasiliana na mimi, tafadhali tuma tarakimu zako 5 kwenye namba 9191 (3 Baht)”.

Kama mwenye simu akijibu ujumbe huo, sauti ya Waziri Mkuu Abhisit itatumwa kwa mwenye namba ya simu, ikisema:

“Mimi, Abhisit Vejjajiva, Waziri Mkuu, nimeona kwamba ninyi raia wenzangu mnateseka, na mko kwenye shinikizo kubwa. Kwa hiyo, nitajipanga kuelekeza maarifa na uwezo wangu wote ili kuisaidia nchi. Lakini siwezi kufaulu kama watu wa Thai hawana mshikamano. Kwa hiyo, nawaomba nyote mnipe fursa.”

Ujumbe

Kwa mujibu wa ofisa wa Chama cha Demokrasia, wazo la kutumia ujumbe mfupi wa maneno lilikuwa ni la Abhisit mwenyewe, na lilisimamiwa na Korn Chatikavanij, ambaye ni Waaziri wa Fedha. Inatuhumiwa kwamba Korn aliitisha mkutano na makampuni makubwa matatu ya simu za mkononi ya AIS, DTAC, na True, na kuyataka yatoe ushirikiano katika kutuma ujumbe huo mfupi wa maneno kwa wateja wao. Mkutano huo wa ushirikiano ulifanyika tarehe 16 Disemba, siku moja kabla Abhisit Vejjajiva hajateuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu. Na sababu iliyotolewa ya kuomba tarakimu 5 ni ili kutathmini idadi ya watu ambao wangejibu ujumbe huo. Baadaye wateja hao wangeorodheshwa na kuingizwa kwenye mfumo wa hifadhidata.

Kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa mtu pasipo kupata ridhaa yake ni jambo linalotazamwa kama ukiukwaji wa haki za faragha za wateja, alieleza mtetezi wa haki za walaji Saree Ongsomwang. Yeye alisema kwamba Abhisit hana budi kuendeleza mawasiliano yake na hadhira kupitia televisisheni na njia nyingine za mawasiliano ya ummaili kuepuka kutovunja haki za walaji.

Saree, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati ya Taasisi ya Utetezi wa Walaji katika Mawasiliano ya Simu, aliongeza kwamba sheria inayosimamia mawasiliano ya simu nchini Thailand, kampuni zinazotoa huduma ya simu za mkononi haziruhusiwa kuweka hadharani orodha ya wateja wao pasipo kwanza kupata ridhaa yao. Pale makampuni hayo matatu yalipotuma ujumbe huo wenye utata kwa wateja wao, pasipo kutoza malipo, kwa niaba ya Waziri Mkuu au Chama Cha Demokrasia, jambo hilo lilileta migogoro ya kisheria na kisiasa.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kupiga Vita Ufisadi ya mwaka 1999 (iliyorekebishwa mwaka 2007), watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na mawaziri, , hawaruhusiwi kupokea zawadi au takrima inayoziti Bhat 3,000. Inakadiriwa kwamba utumaji wa ujumbe huo wa Waziri Mkuu unagharimu zaidi ya Baht milioni 10. Kwa maana hiyo, Abhisit anaweza kupelekwa mahakamani kujibu mashitaka ya kuvunja sheria hiyo, ndivyo alivyojenga hoja msemaji wa Chama cha Pheu Thai, Prompong Nopparit, ambapo aliihimiza Tume ya Kudhibiti Rushwa ya Taifa (NACC) kuanzisha uchunguzi wa kesi hiyo.

Endapo Abhisit na Korn watapatikana na hatia, watavuliwa madaraka yao na kupigiwa marufuku kushika nafasi yoyote ya kisiasa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Maoni yaliyotumwa kwenye mtandao wa intaneti yalikuwa tofautitofauti kwa wakati ule. Kwa ujumla, wengi walikubaliana kwamba ukiukwaji wa haki za faradha za walajio pamoja na siri za taarifa binafsi, pamoja na Waziri Mkuu kufanya mambo mengi ili kujijengea sifa binafsi kupitia vyombo vya habari. Lakini wakati huohuo wengi wanafikiri pia kwamba nia yake ilikuwa njema, kwa hiyo hakuna shida, na kwamba apewe nafasi ili kuitumikia nchi.

Baadhi ya maoni kupitia Yahoo! Answers:

Non noN: “Nafikiri ni njia nyepesi ya kukusanya takwimu, maana ilidai kwanza sanduku la barua la mtu. Kwa hiyo, wanaweza kujua ni kutoka wilaya zipi, majimbo gani, ambapo majibu yanarejeshwa na kwa hiyo wanaweza kutathmini hali ya mambo. Binafsi, nafikiri ni jambo jema na ninataka kuona mshikamano kila mahali nchini Thailand.”

Nicky: “Je, nani anapata hiyo Baht 3? Je, naweza kujitoa? Nafasi yangu ya kuhifadhi kumbukumbu karibu imejaa. Ni ya muundo wa kizamani.”

‘A-Mei': “Nafikiri hii inavuka mipaka ya kujitangaza.”

Tanapon: “Ndiyo, inavuka mipaka. Lakini hebu tumpe nafasi, ajithibitishe kwamba yeye anastahili kwa kazi zake. Pengine ni bora hivyo kuliko sisi huku kubaki tunapambana.”

NH: “Nafikiri, kama imefanyiwa kazi vema, matokeo yatakuwa mazuri.”

Mnamo Julai 16, 2010, NACC imeahirisha tena kupitisha uamuzi juu ya kesi hiyo, na haijapanga tarehe nyingine ya kutoa uamuzi wa mwisho.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.