Kambodia: Je, Viwango vya Maadili Miongoni Mwa Watawa Vinaporomoka?

Kwa kuwa dini ya Kibuda ni dini ya dola kwa mujibuwa Katiba ya nchi ya Kambodia, hasa kwa kuzingatia kwamba karibu raia wote wa Kambodia ni Wabuda, matukio yaliyoripotiwa hivi karibuni kuhusu kuporomoka kwa maadili nchini humo miongoni mwa watawa ni jambo la kutilia maanani.

Watawa wameripotiwa kushiriki katika matukio kadhaa yaliyohusisha utumiaji nguvu au utovu wa nidhamu ikiwemo kushiriki tendo la ngono au kutazama picha na video za ngono. Kuna kisakilichomhusisha mtawa kiongozi aliyeripotiwa kulewa na kisha kumpiga mwanakleri (mtawa) mwingine huku mwanakleri huyo akishindwa kulipigia jambo hilo ripoti kwa sababu za kiusalama,hasa kwa kuwa mtawa kiongozi huyo anafahamika vema kwamba yeye ni kama mtawa mfalme katika jimbo linalohusika. Hivi karibuni , kuna mtawa aliyekamatwa akichukua picha za video za wanawake waliokuwa uchi ambao walikuwa wamekwenda kwenye monasteri ili kujichotea maji yanayoaminika kuwa ya baraka, ambapo inaaminika kwamba maji yanayotolewa na mtawa huyo huwaondolea watu bahati mbaya na kuwafutia mambo yote mabaya. Upelelezi uliosababisha kukamatwa kwa mtawa huyo ulitokana na kusambazwa kwa picha hiyo ya utupu ya video kwa watu wengi hasa kupitia zana za bluetooth za kwenye simu za mkononi. Jambo hili nalo kwa upande mwingine liliibua swali kubwa kuhusu muundombinu wa teknolojia ya kisasa na maendeleo yake nchini Kambodia ambapo sasa hivi watu wanaweza kujipatia picha za utupu kwa urahisi zaidi. Hata hivyo, kama ilivyopendekezwa na Chan Nim, masuala ya namna hii yanaachwa kwa mtu mwenyewe na dhamiri yake hasa kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia hizi zinazoibuka.

Kwa upande mwingine, wapo watawa wengi tu ambao wanaelewa nafasi ya teknolojia katika kuhamasisha mafundisho ya kidini. Wakati ambapo hivi sasa ni jambo la kawaida kuona blogu nyingi zinazoanzishwa na vijana wanaojadili masuala ya kijamii, ya kiteknolojia au ya kibinafsi, sasa kuna hata pia blogu zenye kubeba ujumbe wa Imani ya Buda kama vile Bodhikaram, Saloeurm, Khmerbuddhism. AMafundisho ya kina ya falsafa ya Ki-Buda hivi sasa yanapatikana kwenye mtandao wa Intaneti katika muundo wa maoni mafupimafupi, kamusi, podikasti, na hata vitabu kamili ivilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na Khmer. Zaidi ya hilo, kuna idadi kubwa tu ya watawa ambao wanatumia Intaneti kwa wingi zaidi ili kujaribu kuwafikia watu wengi zaidi. Kwa mfano, Mtukufu Saloeurm Savath, amekuwa akifanya juhudi kubwa kueneza mafundisho ya KiBuda kupitia ukurasa wa face-book ambao sasa umekuwa kama uwanja muruwa unaomwezesha yeye na wafuasi wake kuwasiliana naye kwa urahisi na hasa pale wanapohitaji maelezo zaidi kuhusu Kanuni za KiBuda au masuala mengine.

MaPagoda na watawa ni sehemu muhimu ya urithi wa kiutamaduni na elimu ya Wakambodia. Wanaendelea kutoa mchango mkubwa kwa jamii nzima. Ni matumaini kwamba masuala ya maadili ya watawa yatazingatiwa zaidi ili kuwahimiza watu kujiimarisha zaidi katika imani yao na kuamini kwao imani ya KiBuda. Imani hiyo imechangia sana katika upatanisho wa kitaifa na amani ya kisaikolojia, hasa katika suala la watu walionusurika kufa mikononi mwa Utawala wa Khmer Rouge. Watu hawa waliendelea kufuata mafundisho ya KiBuda na hasa katika kujirekebisha mwenendo wao ili kufutilia mbali shauku yao ya kulipiza kisasi na kutawala hasira zao na badala yake kuwa na matumaini na mtazamo wa kutafuta amani zaidi.

Picha kutoka kwenye ukurasa wa flickr wa Adam Jones, Ph.D.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.