- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Afrika ya Kusini: Dakika 67 za Mabadikio – Siku ya Mandela

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Afrika Kusini, Mwitikio wa Kihisani, Uandishi wa Habari za Kiraia

[1]

Nelson Mandela Chanzo:www.ambassadors.net

Watu wengi wanafahamu kwamba Nelson Mandela katika maisha yake alitumikia kifungo cha miaka 27 jela kule katika Kisiwa cha Robben [2]nchini Afrika ya Kusini. Kitu ambacho watu wengi hawajui ni kwamba Madiba (kama ambavyo wengi wanapenda kumwita huko Afrika ya Kusini) alitumia miaka 67 ya maisha yake katika kupiga vita ubaguzi wa rangi na umaskini. Jumapili hii Julai 18 2010, Rais huyu wa Zamani atatimiza miaka 92. Kwa miaka 16 iliyopita, raia wa Afrika ya Kusini wamekuwa wakisherehekea siku kuu hii ya kuzaliwa Madiba kwa shauku na hamasa motomoto. Mnamo mwaka 2002, Nelson Mandela mwenyewe alitumia siku hii kuzindua kampeni yake ya ulimwengu mzima kuhamasisha welewa na kupiga vita tatizo la VVU/UKIMWI, kameni hiyo inajulikana kama 46664 [3].

Mnamo mwaka 2009, mafanikio ya kampeni na sherehe hizo za 46664 zilipiga hatua ya juu zaidi na kuwa kile kinachofahamika kama “Mandela Day [4]”,yaani “Siku ya Mandela”, ambayo ni siku wanayotumia watu kila mahali duniani kutoa dakika 67 kwa ajili ya kupafanya duniani kuwa mahali bora zaidi pa kuishi. Waandaaji walieleza hivi:

Uamuzi ulifikiwa kwamba kusingekuwa na namna nyingine iliyo bora zaidi ya kusherehekea siku ya kuzaliwa Madiba kila mwaka zaidi ya kuwa na siku ambayo itatengwa maalumu kumkumbuka kwa kazi aliyofanya maishani mwake na kwa shughuli za asasi yake ya hisani na kuhakikisha kwamba urithi aliotuachia unaendelea daima.

Siku ya Mandela ya mwaka 2009 ilikuwa yenye mafanikio makubwa sana nchini Afrika ya Kusini. Ilikuwa yenye mafanikio kiasi hicho kwamba tarehe hii katika mwaka 2010 itakuwa ndiyo ya kwanza katika Siku ya Nelson Mandela ya Kimataifa kama Joburg [5] anavyoripoti:

Itakuwa ndiyo Siku Kimataifa ya Nelson Mandela ya kwanza tangu Umoja wa Mataifa ulipopitisha azimio mwezi Novemba mwaka 2009, likiitangaza tarehe 18 Julai kwamba ni siku inayotengwa kwa ajili ya shughuli za kuimarisha utu. Ni mara ya kwanza kabisa ambapo taasisi hiyo kubwa duniani imetangaza siku ya kimataifa kwa jina la mtu binafsi, likimtambua mtu huyo kama alama ya matumaini hasa kwa wale wanaokangamizwa na kutengwa.

Ingawa siku hiyo itasherehekewa kote ulimwenguni, Madrid, mji mkuu wa Hispania, umechaguliwa kuwa wenyeji wa tamasha kubwa la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya kwanza ya Nelson Mandela, na BB King [6]anatarajiwa kutumbuiza.

Wakazi wa New York nao wataendesha tamasha lao kubwa la kusherehekea. [7] Tukibaki hapo New York, kazi ya kutundika ya sanaa inayosherehekea maisha na urithi wa Nelson Mandela [8]iliwekwa hadharani katika Kituo Kikuu cha jiji la New York kwa heshim ya Mandela Day 46664. Tangazo hilo linaonyesha maneno sita yanayotoa mwanga mzuri wa rangi wa pande 3: tenda, sikiliza, ongoza, unganisha, jifunze na sema. Mbele ya kila neno kuna ujumbe unaoonyesha aliyothamini Nelson Mandela, ujumbe unaowahamasisha wasafiri wanaopita hapo kutenda.

Taasisi ya Nelson Mandela [9]inaripoti:

Nchini Italia, Halmashauri ya Jiji la Firenze, kwa kushirikiana na Jukwaa la Mandela, wameandaa onyesho la picha za video kuhusu Mandela, sinema na Siku ya Mandela, vyote hivyo vitarushwa katika Jukwaa la Mandela na vilevile katika eneo la wazi la kuonyeshea sinema la Florence. Halmashauri ya Jiji la Firenze imejitolea kusaidia Siku ya Mandela na kuhamasisha raia wa Florence kujihusisha katika vuguvugu hili la ulimwengu kwa ajili ya kutenda wema kwa kutia sahihi katika makubaliano yanayounga mkono kuwepo kwa Siku ya Mandela.

Wito wa Mandela wa kutenda pia umesikika kule Cuba: [10]

Tume ya Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge la Cuba leo, katika kikao cha dharura, imepitisha uamuzi wa kusherehekea Julai 18 kama Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela.

Raia wa Afrika ya kUsini nao wameitikia wito wa kutumia dakika 67 za siku yao ili kukuza ubora wa maisha nchini humo. Shughuli mbalimbali [11] zimeandaliwa nchini kote ambapo watu watajitolea muda wao.

PastorMosaSono [12] anauliza [13]:

Je, nani atajiunga na sisi pale Chris Hani Bara kesho saa @02h30 asubuhi kwa muda wa dakika 67 katika Siku ya Mandela katika kampeni ya kufanya usafi?

MuffinMegain [14] anaeleza kwa msisitizo [13]:

Tutakuwa tukisherehekea Siku ya Mandela siku ya Jumapili pale kwenye Zoo ya Lake na tutakuwa tukisaidia kufanya usafi katika jumuiya yetu!

Mwanablogu katika Hope Blog anasema kwamba tuamue kuifanya siku ya Mandela kuwa Siku ya Mapumziko [15]:

Kila mmoja wetu anaweza kuleta tofauti chanya, hata kama ni kidogo, na tukiweka zote hizo pamoja tunaweza kweli kuleta mabadiliko ulimwengui. Siku ya Nelson Mandela siyo siku ya mapumziko – ni siku ambayo sisi sote hatuna budi kuungana na kutenda.

Tusaidiane katika kueneza ndoto ya Nelson Mandela ya baadaye iliyo bora kwa wote, shiriki katika shughuli fulani mwisho wa juma hili, na utueleze kuhusu shughuli hiyo kupitia ukurasa wa Facebook. Je, unataka kutiwa matumaini? Wafanyakazi wetu watakuwa wakijitolea juhudi zao kwa ajili ya Nelson Mandela hata kupitia ukurasa wa Facebook, na hapa kuna fikra 67 za namna ya kuubadili ulimwengu.

Hivi ndivyo wafanyakazi wa mashambani [16] huko Stellenbosch, Afrika ya kusini, watakavyoienzi Siku ya Mandela:

Wafanyakazi wa mashambani wametoa wito kwa watu wa kujitolea kufanya nao kazi kwa dakika 67 siku ya Jumapili katika kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela.

Kundi la “Wanawake walio Mashambani” limetenga kipande cha ardhi kwa ajili ya wanawake wafanyakazi wasio na ajira, wakiwapa fursa ya kupata chakula kidogo cha kuweka mezani.

Kusudi la vuguvugu hilo ni kupunguza ubaguzi wa kijinsia katika sekta ya kilimo.

Mwanablogu wa nchini Tanzania, Simba Deo, anasisitiza thamani ya kujitoa sadaka [17]:

Ni katika kutoa ndiyo tunapokea
Katika kupenda ndiyo tunapendwa
Katika kujitoa sadaka ndiyo na wengine wanajitoa sadaka kwa ajili yetu
Kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine ni ufunguo wa kuendeleza amani, kuendeleza maendeleo, kuendeleza uhuru na haki. Kinyume cha kufanya hivyo ni kujitafutia utukufu binafsi. Kwa chochote tunachofanya, tukifanye kwa sababu tunaamini katika kitu hicho, na kwamba ni kwa ajili binadamu wenzetu na wala si kwa ajili ya kujitafutia utukufu binafsi.

Dorin na the Bush Warriors Clan [18] wanatutaka kumuenzi Mandela kwa kulinda wanyama pori na misiti na mazingira:

Mambo makubwa aliyofanya Nelson Mandela yanapita welewa wa binadamu wengi, maana amefanya mambo mengi kwa ajili ya viumbe pori na mazingira vilevile. Kama ilivyokuwa kwa ndoto zake kuhusu haki za binadamu, Nelson Mandela pia alikuwa na ndoto kuhusu maisha ya viumbe kwenye mapori ya Afrika ili viumbe hao waunganishwe kwa amani katika nchi nyingi. Aliwahi kumwambia mwandishi wa habari wa National Geographic, Peter Godwin, “Nina ndoto ya Afrika iliyo katika amani yenyewe kwa yenyewe … ninaota ndoto ya kuwezekana kwa muungano wa Afrika, ambapo viongozi wake wataunganisha juhudi zao ili kutatua matatizo yanayolikabili bara hili. Ninaota juu ya majangwa makubwa, juu ya misitu yetu, ya maisha yote yanayoendelea kwenye nyika na mapori yetu. Tusisahau kamwe kwamba ni wajibu wetu kulinda mazingira haya. Ni kupitia mbuga za wanyama zinazovuka mipaka ya nchi kwamba tunaweza kufanikisha jambo hilo.
Hivi karibuni tuliwaletea habari ya mpango wake wa kuokoa tembo wa Afrika ya Kusini kwa kuanzisha Kumbi (penu/njia) za Tembo. Ni kupitia ushiriki wake katika asasi yake ya the Peace Parks Foundation (Taasisi ya Mbuga za Wanyama za Amani), pamja na ile ya Sir Richard Branson, Mike Humphries, na Virgin Unite kwamba ndoto hiyo itatimia na kuwa kweli.

Pia kuna “Bikers for Mandela Day” (Waendesha Pikipiki kwa Ajili ya Siku ya Mandela) – kundi la waendesha pikipiki 21 (pamoja na Morgan Freema) ambao wapo katika safari ya siku sita kuizunguka Cape Town ili kusambaza ujumbe wa Siku ya Mandela.

Na kama bado hujashawishika, hebu tazama wito huu mtamu wa kutoka The Elders [19]

Madiba alisema katika safari yake ya mwisho kabisa ya kimataifa kule Landani, Uingereza, mwezi Juni 2008:

Sasa ni wakati wa vizazi vya sasa na vijavyo kuendeleza mapambano yetu dhidi ya utovu wa haki na kwa ajili ya haki za binadamu wote. Mapambano hayo sasa yapo mikononi mwenu.