Upigaji kura mtandaoni umeanza kwa ajili ya Tuzo ya Blogu Bora Zaidi inayotolewa na Deutsche Welle (shirika la habari la Ujerumani), moja kati ya mashindano ya blogu yenye hadhi kubwa kimataifa na blogu zilizotajwa kushiriki ni za lugha kumi na moja tofauti. Unaweza kuipigia kura blogu uipendayo hadi April 14, 2010.
Jopo la majaji litakutana katikati ya mwezi Aprili ili kuamua washindi, na matokeo yatatangazwa Tarehe 15 April wakati wa kongamano la re:publica jijini Berlin, Ujerumani. Washindi watapokea tuzo zao kwenye sherehe za Kusanyiko la Wadau wa Habari Ulimwenguni la Shirika la Habari la Ujerumani litakalofanyika mwezi Juni 2010 huko mjini Bonn.
Miongoni mwa Waliopendekezwa
Katika kigezo cha “ Blogu bora zaidi”, mashindano ni makali baina ya blogu maarufu kutoka katika mtandao. Mwanablogu wa Jordan Osama Romoh hadi sasa ana zaidi ya asilimia 60 ya kura kura zote zilizopigwa. Anablogu masuala ya kijamii ya nchi yake kwa mzaha na kejeli.
Kwa kigezo hichohicho, AJI – Ação de Jovens Indígenas [pt] ya Brazil imebuniwa ili kuwapa nafasi wanablogu vijana wazawa wa eneo lililotengwa la Dourado na kuwasaidia waweze kuandika kuhusu matatizo ya eneo hilo maalum na vile vile kuchambua mambo ya kitaifa, kama vile nafasi ya wazawa nchini Brazil kwa ujumla.
Mshindani mwingine katika kigezo hiki ni Han Han, mwandishi wa riwaya mwenye ufanisi mkubwa ambaye pia ni dereva wa magari ya mashindano wa huko China ambaye ametokea kuwa mwanablogu aliyesomwa sana nchini China na mshiriki katika shindano la 100 bora wa gazeti la Time.
Global Voices na Tuzo ya Blogu Bora Zaidi
Global Voices ilishinda tuzo hiyo mwaka 2005, lakini wengi wa waandishi wa zamani na sasa wa Global Voices wanashiriki katika shindano hili mwaka huu kupitia shughuli zao nje ya Global Voices.
Miongoni mwa blogu zilizotajwa kushindania tuzo hiyo ni Ushahidi, blogu ambayo kwa kutumia tovuti inasaidia kutoa taarifa za maafa kupitia simu za mikononi na mtandao wa kijamii. Waandishi wa zamani wa Global Voices Juliana Rotich, Ory Okolloh walisaidia katika kuandaa mradi huu, ambao awali uliundwa ili kuorodhesha taarifa za mgogoro wa baada ya uchaguzi nchini Kenya mwanzoni mwa mwaka 2008. Hivi karibuni, ramani za Ushahidi zilitumika nchini Haiti baada ya tetemeko la ardhi kuikumba nchi hiyo, vilevile baada ya tetemeko nchini Chile.
HerdictWeb, ni mradi wa kituo cha Berkman cha Intaneti na Jamii cha chuo kikuu cha Havard (ilipoanzishwa Global Voices) ni mtajwa katika kigezo cha ‘Tuzo ya Wanahabari Wasio na Mipaka”. Tovuti ya Herdict inatafuta kujua kinachowapata watumiaji wa mtandao ulimwenguni hasa wanavyoweza au kushindwa kuzifikia tovuti.
Talk Morocco — jukwaa linalohaririwa lenye nia ya kuhamasisha mijadala ya wazi, inayoweka wazi ukweli na yenye uelewa mkubwa wa mambo yanayohusu Moroko na waMoroko walio ughaibuni iliyoanzishwa na waandishi wa Global Voices Jillian C. York na Hisham — wametajwa pamoja katika kigezo cha blogu za Kiingereza sambamba na Sauti kutoka Gaza, Haupo Hapa na nyingine nyingi.
Mwandishi mwingine wa Global Voices, Jorge Gobbi amekuwa akiblogu kuhusu vidokezo vya safari kwa kiHispania katika Blog de Viajes tangu 2003. Blogu hiyo imeshawahi kushinda tuzo blogu bora ya safari ya kiHispania na mwandishi wa mwongozo wa safari Lonely Planet. Tazama blogu nyingine zilizotajwa katika kigezo hiki hapa.
Mwanablogu mKanada anayetishiwa kifo
Michelle Blanc, mwanamke mKanada aliyebadili jinsia ambaye anablogu kwa Kifaransa kuhusu mabadiliko ya maisha yake ni miongoni mwa walipendekezwa katika kigezo cha blogu za Kifaransa. Michelle aligundua hivi karibuni [fr] vitisho kadhaa vinavyosumbua dhidi maisha yake vilivyotumwa kwenye YouTube na tovuti nyingine.
Sambamba na blogu ya Michelle iitwayo, Femme 2.0 ou le parcour transsexuel katika kigezo cha Kifaransa, kuna nyingine nyingi kama vile La Vigie du Web, Chez Gangoueus, Chroniques de la loose, Entendu à Paris na zaidi.
Usisahau kuzipigia kura zile unazozipenda!
Pia tazama: Arab World: Pulling all the Stops for the BoBs