Uganda: Wanafunzi Wacharuka, Kampala Yawaka Moto

Jumanne, majanga mawili tofauti yaliikumba Kampala, mji mkuu wa Uganda: wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere walifanya ghasia baada ya wanafunzi wenzao wawili kupigwa risasi. Na makaburi ya Kasubi, ambayo ni sehemu ya Urithi wa Dunia ya UNESCO na eneo la kaburi la mfalme wa moja ya makabila makubwa zaidi ya Uganda, liliteketea kwa moto.

Ghasia Chuo Kikuu cha Makerere

Kwa mujibu wa magazeti ya Uganda, ghasia katika Chuo Kikuu cha Makerere, chuo kikuu kikubwa zaidi nchini Uganda, zilianza baada ya wanafunzi wawili kupigwa risasi na mmoja kujeruhiwa vibaya na mlinzi wa usalama usiku wa Jumatatu wakati wa mkutano kuhusu uchaguzi wa wanafunzi. Gazeti la Daily Monitor linaripoti maelezo mawili tofauti ya tukio hilo:

Polisi wanasema kuwa wanafunzi wengi walikusanyika katika hosteli kwa ajili ya hatua za mwisho za kampeni ya uchaguzi wa wanafunzi wakati mlinzi aliyeshuku kuwa mmoja wa wanafunzi hao alikuwa ana nia ya kuiharibu gari iliyokuwa kwenye maegesho alifyatua risasi.

Ripoti za awali zinasema kuwa mashabiki wa Simon Kamau, mmoja wa washindani katika kinyang’anyiro cha urais, walipambana na wale wa John Taylor wa NRM, na kusababisha kupigwa risasi kwa wanafunzi hao wa ki-Kenya.

Gazeti la New Vision linasema kuwa kupigwa risasi kulitokana na kutokukubaliana kati ya mgombea na mmoja wa mashabiki wa mgombea mwingine:

Wakati kundi hilo lilipojiandaa kuondoka, lilibabatizwa na Nyongesa ambaye inaaminika kuwa yumo katika kambi ya John Kamau, mmoja wa WaKenya wawili waliokuwa kwenye mbio za uchaguzi.

Inasemekana kuwa alijaribu kumpiga [mgombea John] Teira kwa benchi wakati kundi hilo lilipokataa amri yake ya kuondoka hapo kwenye hosteli.

Ugomvi mdogo ulizuka, ambao kwa mujibu wa mashahidi, ulisababisha mlinzi kufyatua risasi ambayo iliwapiga wanafunzi watatu.

Wanafunzi walijibu mapigo siku ya Jumanne kwa kuandamana kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Makerere huku wamebeba mabango na jeneza ili kupinga mauaji hayo. Magazeti yote mawili yanaripoti kuwa maandamano hayo yaligeuka na kuwa ghasia na kwamba polisi walitumia mabomu ya machozi ili kuwasambaratisha watu.

Mwandishi wa habari, Ole Tangen Jr, anayeishi mjini Kampala alikuwa ni mmoja wa watu wa kwanza kublogu juu ya ghasia za Makerere. Alijiuliza ni kwa nini wanafunzi wengi hawatumii mitandao ya uanahabari wa kijamii kusambaza habari:

Jana usiku wanafunzi wawili wa Makerere walipigwa risasi na mlinzi wa usalama mwenye silaha jambo ambalo lilipelekea ghasia zilizosambaa sana katika maeneo ya chuo kikuu leo.

Hata hivyo hakuna aliyekumbuka kutumia Twita ili kupasha habari juu ya habari hii. Utafutaji katika Twita kwa kutumia alama ya #Makerere kwa siku nzima uliishia bila jibu lolote zaidi ya ripoti za habari hiyo. Inakuwaje hawa wanafunzi – hasa wanafunzi walio hai kwenye siasa – hawatumii vyombo vya habari vya kijamii ambavyo vinapatikana. Je ni kutofahamu kuhusu Twita? Au ni gharama kubwa za Intaneti? Ni nini kinachosababisha hivi?

Utafutaji katika twita wa neno “makerere” kwa kiasi kikubwa ulikubaliana na dai hilo, huku jumbe nyingi za twita zikiwa na makala za magazeti. Na pia, baadhi watumiaji wa Twita huko Kampala waliwza kuongezea mazingira:

@arthurnakkaka (masaa 18 yaliyopita): Risasi zinapigwa. Au ni mabomu ya machozi? #Makerere

@arthurnakkaka (masaa 18 yaliyopita): Wanafunzi wanapiga mayowe na kukimbia. Hali inakuwa mbaya #Makerere

@aspindler2 (masaa 18 yaliyopita): Maandamano katika Chuo Cha Makerere Kampala Uganda baada ya wanafunzi 2 kupigwa risasi na mlinzi wa usalama jana usiku. Polisi wanapiga mabomu ya machozi kutawanya watu

@mirembe_maria (masaa 14 yaliyopita): Maandamano ya Chuo kikuu cha makerere yamewaacha watu 2 wamefariki na mmoja katika hali mbaya, je ni njia ipi serikali itatumia kwenda mbele baada ya yote haya?


Makaburi ya Kasubi Yaungua Moto

Jumanne usiku, katika tukio lisilo na uhusiano na hili, makaburi ya Kasubi, eneo la makaburi ya wafalme wa kabila la Baganda, liliteketea kwa moto. Mfalme wa sasa wa Baganda amekuwa katika habari hivi karibuni kutokana na mapambano yake na rais wa Uganda, Yoweri Museveni. Mwezi Septemba 2009, hali mbaya ya uhusiano kati yao ilipelekea ghasia mbaya katika Kampala, na raia wanahofia kwamba moto huu unaweza kusababisha ghasia nyingine baadaye.

Mwanablogu wa Uganda 27th Comrade anaandika:

Kwa kawaida huwa ni njama za makusudi sehemu kama hii inapoungua moto. (paa) Imejengwa kwa nyasi, kwa hiyo moto utaangamiza kabisa.

Tayari, baadhi ya mapunguani Karibu yangu wameshaanza kusema “Serikali!” Mimi pengine nitasema “Upinzani!” lakini nahisi inawezekana kabisa ni mfanyakazi ambaye hakuwa makini na moto. Hebu tusubiri habari.

Mwanablogu na mwandishi wa habari Rosebell anaandika:

Uhusiano kati ya serikali ya Rais Museveni na Ufalme wa Buganda uko mbali na (uhusiano) waridi na hilo limekwishatoa mazingira yenye rutuba kwa wengi kufikiria kuwa kulikuwa na mchezo wa dhambi. Watu wengi wanatarajia ghasia kulipuka alfajiri. Tunatumaini kuwa kutakuwa na uchunguzi wa kina juu ya kuungua kwa makaburi hayo na kwamba hakuna atakayepoteza maisha na mali. Huu ni wakati muhimu kwa uongozi wa Buganda. Makaburi ya Kasubi pia ni urithi kwa nchi kwa hiyo natumaini pande zote zitalishughulikia suala hili kwa uangalifu wa hali juu.

Waganda walio kwenye Twita nao pia wana hofu:

@daphnzempire (masaa 6 yaliyopita): makaburi ya kasubi yanawaka moto.. Mungu wangu tunaelekea wapi

@Kakazi (masaa 6 yaliyopita): Makaburi ya Kasubi yachomwa moto kama masaa 2 yaliyopita.. Ninasali kwa dhati kwamba haikuwa kwa makusudi!! Hasara kubwa kwa urithi wetu..:-(

@mugumya (masaa 6 yaliyopita): Ninahofia kunaweza kutokea aina fulani ya machafuko kesho baada ya makaburi ya kasubi kuteketea mjini Kampala

Lauren, Mmarekani ambaye aliwahi kuishi Kampala, anakumbuka jinsi aliwapeleka wageni kutembelea makaburi hayo:

Makaburi ya Kasubi kwangu ni zaidi ya majengo muhimu ya utamaduni na historia. Wakati tulipokuwa tunaishi Uganda, yalikuwa jirani zangu. Nyumba yetu ilikuwa chini ya bonde la kasubi, tuliyapita Makaburi hayo kila siku tukienda na kurudi kutoka Kampala mjini. Tuliwapek\leka wageni wengi kuyaangalia Makaburi hayo na kujifunza zaidi juu ya kabila la Buganda, historian a utamaduni wake. Siku zote nilipenda kupita mbele ya walinzi wa makaburi; waliovalia mavazi ya kitamaduni ya rangi ya chungwa iliyokoza na kuegemea mti mkubwa ulikuwa mbele, walisubiri bila kuchoka ili kusalimu wageni wanaofuatia.

Makaburi ya Kasubi Oktoba 2008. Picha kwa hisani ya Lauren

Makaburi ya Kasubi Oktoba 2008. Picha kwa hisani ya Lauren

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.