Naijeria: Ghasia Zalipuka Huko Jos Kwa Mara Nyingine

Huko Jos, machafuko yanaelekea kujitokeza katika mizunguko inayozidi kuwa midogo: machafuko mabaya yaliukumba mji huo mwaka 1994, 2001, 2008, na – hata miezi miwili iliyopita – mnamo mwezi Januari 2010. Mgogoro wa sasa unasemekana kuwa ulianza katika tukio la kisasi kilichotokana na uharibifu uliotokea mwezi Januari – kumekuwa na ripoti za watoto na wazee kuwindwa na magenge ya watu wanaohaha wenye bunduki na mapanga.

Kama ilivyokuwa kwenye machafuko yaliyopita, mapambano ya sasa huko Jos yamekuwa yakipiginwa katika misingi ya kidini – Jos ipo kwenye mpaka kati ya kaskazini ya Naijeria yenye Waislamu wengi na Kusini kwenye Wakristu wengi. Upatikanaji wa ardhi na rasilimali kunategemea ikiwa mtu ni mwenyeji, au “mzawa”, wa mji Kikristu kihistoria, au “mhamiaji” kutoka sehemu nyingine (“wahamiaji” mara nyingi ni Waislamu kutoka Kaskazini’ angalia ripoti ya Human Rights Watch kuhusu suala hili hapa kwa taarifa zaidi juu ya suala hili).

Vyanzo vingi vimeweka idadi ya waliofariki katika mamia: Al-jazeera na BBC wote wameripoti vifo zaidi ya 500, japokuwa chanzo kimoja cha serikali kimetoa idadi rasmi ya vifo 55. mazishi ya haraka yasababisha ugumu katika kutathmini vizuri jumla ya waliofariki, wakati sababu za kisiasa pia zinapelekea kuwepo kwa makosa katika idadi. Shaibu Mohammed wa Reuters anatoa ufafanuzi:

Idadi ya waliofariki iliingiliwa na siasa katika matukio ya ghasia yaliyopita huko katikati ya Naijeria, huku makundi mbalimbali yakishutumiwa kwa ama kutia chumvi kwa kuzidisha idadi kutokana na malengo ya kisiasa au kwa kupunguza idadi hiyo ili kujaribu kuloanisha hatari ya visasi.

Katika ulimwengu wa blogu, vitisho, aibu na na imani ni hisia ambazo zilizotawala. Linda Ikeji aliposti picha kwenye blogu yake, ambayo ilionyesha wazi damu ilivyomwagika. Aliandika:

HAPANA, sitaiondoa picha. Hii ni aibu yet una kushindwa kwetu kama nchi. Hebu sote tuiangalie!

Mtoa maoni katika tovuti alikubaliana na uamuzi ule:

Ahsante kwa kuiacha hapa kwa sababu ni lazima tuache kujidanganya kuwa kila kitu kipo sawa… muda umefika kwa mambo haya kukomeshwa…

Wanablogu kadhaa walieleza yale yanayofonana kati ya tetemeko la ardhi kule Haiti na machafuko ya Jos. Tywo, mtoa maoni mwingine katika makala ya Ikeji aliandika:

Mungu ameibariki sana Naijeria. Yaani, ni nadra kwetu kukumbwa na majanga ya asili na mambo kama hayo. Tunavyo vifo vinavyosababishwa na watu wasio na mioyo. Ukweli ni kwamba hatusongi mbele.

Babajidesalu alitoa mtazamo unaofanana na huo:

Wakati dunia inakumbwa na majanga ya asili, Naijeria inakumbwa na majanga tuliyoyatengeneza wenyewe. Mauaji ya kinyama ya hivi karibuni katika Jos yanathibisha mtazamo huu.

Baada ya machafuko ya tarehe 10 Januari, mwanablogu mmoja alianzisha tovuti, Sisi Ni Jos, ili kuwasaidia walioathirika na machafuko. Alielezea msukumo wake kama ifuatavyo:

Zilikuwa ni jitihada za wyclef jean ambazo ziliwafanya wanamuziki nyota wengine kukusanyika ili kusaidia Haiti. Niliwaona hata wanablogu wengine wa Naijeria waliotoa kwa ajili ya Haiti wakati huo huo wanashutumu yaliyotokea huko Jos, KWA MANENO huku wakisema Mungu aisaidie Naijeria.

Nimejiuliza mara kwa mara ni kwa nini sisi Wanaijeria hulalamika na huwa hatutoi ufafanuzi au suluhu za matatizo yanayotukabili. Kwa njia yoyote ndogo niwezavyo, ninajaribu kutatua tatizo au kufanya jitihada.

F, mtoa maoni mwingine kwenye makala ya Linda Ikeji, aliliona tatizo kuwa kubwa zaidi ya dini, na lililotapakaa nchi nzima:

Upuuzi utakoma mjini Jos pale upuuzi utakapokoma kule Abuja. Siasa zote hizi za mizengwe zinapaswa kukoma ili kwamba watu waweze kupata huduma muhimu. Wnasema mtu mwenye njaa ana hasira. Ni vivyo hivyo kwenye bonde la mto Niger. Ikiwa kila mmoja angekuwa ameshiba, angekuwa na uwezo wa kupata elimu nzuri, umeme, maji safi na hali nzuri ya maisha, nani angefikiria kujaribu kuliua kundi jingine la dini/kabila ambalo linaonekana “kupigania nafasi”?

…Tutaendelea kuonyesha hasira zetu kwa mauaji haya – jambo ambalo halitasitisha kutokea kwa mauaji hayo. Kushughulikia mzizi wa tatizo ndiyo suluhisho pekee la janga hili linalojirudia rudia.

Adeola Aderounmu alitoa mtazamo unaofanana na huo, na kuzitupa lawama kwa viongozi wa Naijeria:

Suala la Jos si suala la Jos pekee. Ni taswira akisi ya kutokuwepo kwa demokrasia na kushindwa kwa mfumo. Hatuna mfumo unaoeleweka na nchi imejengwa kwa watu wasio na maana badala kujengwa kwa taasisi imara na kanuni nzuri za utawala.

Lakini kuna mtoa maoni katika makala hiyo ambaye hakuafiki:

Mara zote unatenganisha viongozi na umma. Katika wakati mmoja au mwingine viongozi walijitokeza kutoka katika umma. Kwa hiyo hauwezi kuwatenganisha. (watu wengi katika umma wanajitahidi kujiunga na uongozi).

Kushindwa kwa Naijeria na Wanaijeria kama watu kwa ujumla ni lazima kubebwe na wote.

Wanaijeria itabidi wajiangalie kama jamii na kujiuliza kwa nini hawajafanya lolote kimfumo kwa zaidi ya miaka 50 ili kuzuia kuteleza kuelekea kusahaulika na kukosa matumaini? Ni kwa nini wanapopata harufu ya madaraka, hafanya makosa katika kila kitu? Ukweli ni kwamba jamii yetu kwa kiwangi kikubwa imepotoka, na kwa kuwa vitendo potofu vinakubalika, na katika mifano mingine husherehekewa…

Tangu machafuko yaanze siku ya Jumapili, jeshi na polisi vimeudhibiti mji, na kuwatia mbaronizaidi ya watu 100. SolomonSydelle aliripoti juu ya uwezekano kuwa mahakama ya Kimataifa ya jinai inaweza kuingilia kati na kutoa suluhisho la kisheria kwa tatizo hili na kuepusha mzunguko wa visasi siku za baadaye.

Soma kuhusu machafuko ya Januari hapa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.