- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Misri: Wafanyakazi wa IslamOnline Wagoma

Mada za Habari: Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, Qatar, Habari za Hivi Punde, Habari za Wafanyakazi, Haki za Binadamu, Maandamano, Vijana

Baada ya uongozi mpya wa Qatari kutangaza kuwa wafanyakazi 250 watapunguzwa kazi katika mtandao wa habari unaosomwa sana wa IslamOnline (IOL), mamia ya wafanyakazi, wahariri, na waandishi wa habari walianza mgomo wa kuonyesha hasira yao [1]. Hali ilizidi kuwa mbaya kwa kasi sana pale uongozi ulipotishia kuita vikosi vya usalama ili kuvunjilia mbali mgomo huo baridi, lakini wafanyakazi walithibitisha kwamba walikuwa imara na kuwa wangeendelea na mgomo wao mpaka matakwa yao yatimizwe.

Pengine ni jambo linalostahili kutajwa kwamba huenda mgomo huu ni wa kwanza wa aina yake unaotumia kwa ufanisi na vizuri zaidi njia za kisasa za upashanaji habari ili kuvuta usikivu na uungwaji mkono, kuanzia na Twita inayoendelea [2] mpaka mmiminiko wa habari wa hapo kwa hapo [3].

Nadia El Awady, aliyekuwa mwandishi wa habari wa IOL, alikuwa akifuatilia kwa karibu hali ya mambo na alituma [4] kwenye blogu yake tamko lililotolewa na wafanyakazi wa Islamonline:

Hali imezidi kuwa mbaya ndani ya Makao Makuu ya IOL huko Cairo, baada ya kuwa menejimenti ya Qatari kutuma wanasheria kulishika jengo na mali zake zote pamoja na nyaraka, na kuwachunguza wafanyakazi 250 waliotuma tamko lao kwa Shehe Qaradawy, ambaye ni mwenyekiti wa Bodi, wakilalamikia vitendo visivyo vya haki vilivyofanywa na menejimenti mpya.
Baadhi ya vyanzo vilidokeza kuwa sababu iliyojificha ya kuwachunguza wafanyakazi hawa ni kuwafukuza kazi kisha kuwapiga marufuku kudai haki zao zozote za kifedha.

Watu walio vyanzo vya habari na walio na uhakika wa kile wanachokieleza ambao wamo ndani ya taasisi hiyo wanasema kwamba lengo la uchunguzi dhidi ya wafanyakazi ni kuwaondoa mara moja na kuwanyika madai yao mbalimbali ya fedha waliyo nayo.

Kwa upande wake Tadamon Masr alieleza [5] [Ar] kwamba mgogoro huo huenda umetokana na lengo la uongozi mpya wa Qatari kutaka kuhamisha makao makuu ya IOL kutoka Cairo kwenda Doha. AbdelMoniem alikuwa na wasiwasi [6] [Ar] na alijiuliza kama ilikuwa ni njama za wenye siasa kali kutaka kunyamazisha sauti zinazotaka maelewano zaidi zilizo katika tovuti kama ile ya IslamOnline.

Zeinobia [7] alitoa maoni yanayotaka kufanana na hayo kwa AbdelMoniem akisema:

Inasemekana kwamba Uongozi mpya wa Qatari ni ule wenye msimamo wa kihafidhina unaoamini kwamba uendeshaji wa tovuti hiyo hauna budi kushikilia mitazamo ya kidini yenye msimamo wa kihafidhina na kuondolea mbali vipengele vingine.

Kupitia Twita, mwandishi mwingine wa habari wa zamani wa IOL, Mohammed, alikuja na taarifa inayosema:

@MohammedY [8]: Kwa waandishi walio Misri na ulimwengu wa Kiarabu: Waandishi wa habari wanaofanya kazi katika Islamonline wanatendewa vibaya na uongozi wao mpya ili kuwanyamazisha kutoa matamko dhidi ya vitendo vibaya vya uendeshaji kampuni.
@MohammedY [9]: Kwa hiyo, pale wafanyakazi wanapotia saini maelezo kuhusu matatizo yanayowakabii, basi uongozi unawaweka wafanyakazi chini ya uchunguzi. Hivi jambo hili limesababishwa nini hapo Islamonline?

Abdullah El Shamy na Muhammad Ghafari, ambao ni miongoni mwa wanaogoma, walikuwa wakishughulikia taarifa zinazoingia moja kwa moja, kwa hiyo walikuwa wakituma taarifa hizo moja kwa moja kwenye akaunti zao za Twita na kutuma picha za eneo hilo la kazi.

@Ghafari [10]: Kwa wale wanaoguswa na hali hii, ili kupata taarifa mpya kuhusu mgomo wa wafanyakazi wa Islamonline, tafadhali bofya hapa: http://www.ustream.tv/channel/iol-on-air [3]

Ghafari hakusahau kueleza jinsi gani wanawake wanavyoshiriki katika kuupa mgomo huo nguvu:

@Ghafari
#IslamOnline #mgomo #wanawake
Hakuna sababu ya kueleza jinsi wanawake wanavyosaidia kuutia nguvu mgomo huu, zaidi ya hilo wanatunga nyimbo za hamasa pia!

Nadia El Awady vilevile alikuwa akiwapa taarifa rafiki zake kupitia Twita karibu kila dakika, alieleza:

@NadiaE [11]: Mfanyakazi wa kike pale Islamonline analeza nia yake ya kulala ofisini kutumia begi la kulalia ili kuendeleza mgomo.

@NadiaE [12]: #mfanyakazi wa islamonline, @mos3abof, anatoa wito wa wafuatiliaji kutoa uungaji mkono kwa yale yanayochapishwa na tovuti [mipango ya Bodi ya Qatar na uchukuaji wake haileweki]

Mwanablogu wa Misri, Ahmed Shokeir, alitoa maoni kwamba karibu kila mtu aliona, akielezea kuhusu zana za vyombo vya habari vya kisasa, jinsi vinavyotumiwa tofauti katika wakati huu:

@Shokeir
Nafikiri kuwa mgomo wa Islamonline huenda ukawa wa kwanza kutumwa moja kwa moja mtandaoni. Naamini njia hii itakuja kuwa yenye ufanisi na kuwa zana itakayotumiwa sana katika siku za hivi karibuni.

Pia inafaa kutaja kwamba kuna uvumi kwenye Twita kwamba huenda El Qaradawi akajiuzulu nafasi yake, hiyo ni kwa mujibu wa Mohammed:

@MohammedY [13] : #Menejimenti ya IslamOnline huko Qatar imekuwa ikikataa kupokea simu kutoka kwa Al-Qaradawi kwa sababu inamtuhumu kwamba alitaka kujiunga upande wa wafanyakazi (kupitia Fathi katika IOL)

Na hiyo ilipata uungaji mkono kutoka kwa mwanaTwita mwingine, Nadia:

@NadiaE [14]: Motaz Al-Khateeb, ambaye ni mtayarishaji wa kipindi cha televisheni cha Shehe Al-Qaradawi's katika Aljazeera alizungumza na katibu muhtasi wa Shehe huyo akimkariri akisema kuwa bado anafikiria kujiuzuru.

Kabla ya kwenda kulala, Ghafari alihitimisha utoaji taarifa zake za kila mara kwa kusema kwamba hawatasimamisha mgomo wao mpaka matakwa yao yote yatimizwe:

@Ghafari [15]: #Mgomo wa wafanyakazi wa IslamOnline utaendelea mpaka asubuhi, yaani mpaka uamuzi ufanyike unaothibitisha kwamba haki zetu zipo palepale.

Picha zaidi zipo hapa [16].