- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Kenya: Mafuriko Makubwa Yapasua Kingo za Mto Ewaso Nyiro Huko Samburu

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Kenya, Majanga, Mazingira, Uandishi wa Habari za Kiraia

Kituo Cha Utafiti Cha kikiwa chini ya maji

Kituo Cha Utafiti Cha STE kikiwa chini ya maji


Alfajiri siku ya Alhamisi, tarehe 4 Machi 2010, mafuriko makubwa yaliikumba Samburu huko kaskazini mwa Kenya na kuharibu nyumba 6 za kulala watalii watalii, baadhi ya kambi za utafiti wa wanyama pori na kuwaacha maelfu wakiwa katika paa za nyumba na kwenye miti. Wimbi hili la maji ya mafuriko lilikuja kutokea mto Ewaso Nyiro ambao kingo zake zilipasuka kufuatia mvua kubwa kwenye maeneo uya Mlima Kenya.

Blogu ya Simba wa Ewaso [1] inaandika:

Mnamo majira ya saa 11 leo alfajiri [tarehe 4 Machi], mafuriko makubwa yalikuja kutokea Mto Ewaso Nyiro na kufyeka nyumba za watalii na kambi. Rafiki zetu waliokuwa katika maeneo ya Elephant Watch na Okoa Tembo [STE] [2] waliweza kufika kwenye uwanda wa juu, lakini kambi zilifyekwa kabisa. Kwingineko, watu walikuwa juu ya miti na paa za nyumba wakisubiri msaada. Jeshi la uingereza, Shirika la Ndege la Tropic Air, na wengine walimaliza siku nzima wakiwaokoa watu kutoka katika eneo hilo.

Kwenye blogu ya Baraza [3], Paula Kahumbu ameweka mawasiliano kutoka Okoa Tembo ambayo kituo chake cha utafiti kiliangamia:

Leo tuliamka na ripoti kutoka kwa wenzetu walio kwenye kituo cha utafiti kwamba Samburu iko chini ya maji! Samburu yote imefurika! Mahema yetu yote yameswagwa na mafuriko! Kituo chetu cha utafitri kama tunavyokijua hakipo tena! Kwa bahati wenzetu hao wako salama lakini wananing’inia kwenye miti iliyo juu ya vilima wakisubiri kuokolewa na helikopta!

Blogu ya Paula inasema, “hivi sasa maji ya mafuriko bila ya shaka yameanza kupungua lakini watu wote wameondolewa kutoka kambi zote katika Samburu na Shaba “ Hii ni kutokana na kutarajiwa kwa mvua zaidi ambazo zinaweza kunyesha.Mwanablogu wa Simba wa Ewaso nasema, “jambo hasa linalotisha ni kuwa mvua nyingi zaidi inatarajiwa.”

Simba wa Ewaso iliweka picha kadhaa [4] – pamoja na wito – ambavyo vilitumwa na mwanablogu, Shivani, ambaye kwa sasa yupo Samburu. Wito huo unawataka watu watoe michango kupitia blogu yao au wawasiliane na ofisi yao ya Nairobi (kwa wale walio Nairobi na wangependa kuchangia chakula na mavazi). WildlifeDirect pia imetuma wito [5] kwa kutumia picha hizo hizo.

Moja ya vituo huru vya Televisheni nchini kenye NTV imepandisha video ya YouTube [6] ya janga hili.