Global Pulse 2010: Mwaliko wa kuzungumza na watoa uamuzi mtandaoni


Kuanzia tarehe 29 hadi 31 Machi, vuguvugu linalojulikana kama Global Pulse 2010, yaani Mapigo ya Moyo ya Ulimwengu 2010, linakusudia kuwakusanya jumla ya watu 20,000 kupitia mtandao ili wafanya mazungumzo kuhusu mada mbalimbali kuanzia zinazohusu maendeleo ya binadamu hadi sayansi na teknolojia.

Tukio hilo linadhaminiwa na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya Marekani (USAID),na lengo ni kuwapa raia wa ulimwengu fursa ya kutoa maoni yao na kushirikishana fikra za ufumbuzi za kushughulikia masuala mbalimbali ya kijamii. Kwa mujibu wa USAID, msukumo wa kuja na wazo hili la mazungumzo ya mtandaoni, lilitokana na hotuba aliyoitoa Rais Barack Obama mwezi Juni mwaka 2009 jijini Cairo, Misri, ambapo alisema kwamba angefanya juhudi kuhamasisha ushirikiano miongoni mwa binadamu duniani.

Mada kumi za majadiliano

Tukio hilo litadumu kwa muda wa saa 72 mfululizo bila kusimama, na washiriki wataweza kufuatilia na kutoa maoni moja kwa moja kupitia mijadala itakayokuwa ikiendelea yote moja kwa moja na kwa wakati mmoja. Majadiliano yote yatakuwa yakiendeshwa na watoa maoni viongozi walioteuliwa, watoa uamuzi na wanachama wa asasi zisizo za serikali, ikiwa ni pamoja na Youssou N'Dour [fr], mwimbaji maarufu wa kutoka Senegali, ambaye anajishughulisha sana na kupiga vita ugonjwa wa malaria, Iqbal Z. Quadir, ambaye ni mwanzilishi wa Grameenphone huko Bangladesh,na hata Ethan Zuckerman, ambaye ni mwanzilishi mwenza wa Global Voices online.

Washiriki watatoka katika nchi zipatazo 128 na watashirikishana na kujadiliana kuhusu mada 10 zilizo pana, nazo zimeorodheshwa hapa:

  • Kuwashajiisha watu wa kizazi kipya
  • Kuwawezesha wanawake na wasichana
  • Kuwezesha Elimu ya Msingi (Maalumu)
  • Ujenzi wa Ushirikiano zilizo Madhubuti zaidi
  • Kutumia Haki za Kisiasa na Kiraia
  • Kuhamasisha Afya ya Ulimwengu
  • Kuendeleza Ujasiriamali, Biashara & Fursa za Kiuchumi
  • Kuendeleza na Kulea Sayansi, Teknolojia na Ubunifu/Uvumbuzi
  • Kusaidia kuwa na Sayari iliyo Endelevu
  • Kufuatilia kwa karibu Changamoto zilizo kubwa

Kuibua Teknolojia Iliyo ya Uvumbuzi

Suala la kuwaleta pamoja maelfu ya watu kupitia mtandao ni jambo gumu kiasi chake. Kwa bahati nzuri, teknolojia ya jukwaa litakalotumika, linaloitwa IBM Jam, tayari limekwishafanyiwa majaribio katika matukio yaliyopita.

Bill Tipton alishiriki katika jukwaa lililojulikana kama Habitat Jam - ambalo nalo lilidumu mtandaoni kwa muda wa siku tatu mnamo mwaka 2005, lengo la tukio hilo lilikuwa ni kukusanya mawazo kuhusu uendelevu wa miji. Anatoa maoni yake kupitia blogu ya the Global Dialogue Center:

Najua kwamba jambo hili linawezekana maana nilipata kushiriki katika tukio kama hili mnamo mwaka 2005 […] Makumi elfu ya watu binafsi – wakiwamo viongozi wa serikali, wafanyabiashara, wana-asasi zisizo za serikali na wataalamu – wote walikuja kujadili masulaa yanayozikabili jamii zinazoishi mijini hapa duniani.

[…]

Bado naendelea kukutana na kufanya kazi na watu niliokutna nao katika Jukwaa lile kamambe na nina matarajio ya kukutana na watu wengine tena wenye vipawa vya pekee katika Global Pulse 2010.


Ili kushiriki

Ili kushiriki kwenye tukio hili la Global Pulse, unachohitaji ni kompyuta iliyounganishwa na mtandao – na pia huna budi kujiandikisha kabla (bila malipo). Kabla ya tarehe 29 Machi, unaweza kufuatilia kupitia Twita @globalpulse2010 na pia kupitia hashtag #gp2010. Pia kuna ukurasa wa Facebook wenye zaidi ya washabiki 700, ambapo tayari mapendekezo yamekwishaanza kutolewa.

Wazo moja la Olivier Mupila liko hivi:

Swali: Je, Global Pulse inaweza kupendekeza viashiria vyenye ufanisi katika kufuatilia na kukabiliana na maendeleo ya kesi za ufisadi mkubwa kutoka zinapoanza kutajwa mpaka kwa wakala zinazopeleleza, kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka, kuendelea mpaka kwenye mahakama na kuendelea wakati zikiwa mahakamani bado pasipo kuweka hatarini haki za mtu mmojammoja ili wapate hukumu ya haki au sifa yao isiharibike kabla ya kupatikana na hatia? Je, ni mambo gani yanachukuliwa kuwa utaratibu mzuri katika eneo hili na je kuna nchi ambazo huwa zinafanya jambo hili mara kwa mara? Na, je, kwa nini waandishi wazuri barani Afrika hawamo kwenye vitabu vizuri [vya] serikali?

Kwa mujibu wa Dkt. Rajiv Shah, Mtawala katika USAID, mkutano huo wa mtandaoni utawaleta pamoja “watu ambao huwa wameketi mezani kama wafanya uamuzi”. Je, jambo hili linaweza kuwa ndiyo mwelekeo wa demokrasi ya siku za usoni? Bila shaka litakuwa jambo la kupendeza kulichungua ili kujifahamisha.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.