Haiti: Kwa Nini Habari Zote Hizi Kuhusu Yatima?

Mwezi mmoja baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa poiti saba kuangamiza sehemu kubwa ya Haiti ya kusini, mustakabali wa watoto, na hasa hasa yatima, umekuwa ni habari kubwa katika kona mbalimbali. Lakini sauti za Wahaiti kwenye mada husika zimekuwa chache.

Katika taarifa hii ndefu ya video iliyowekwa kwenye Telegraph21, iliyorekodiwa siku chache baada ya tetememeko, mameneja wa vituo viwili vya watoto yatima nchini Haiti wanazungumzia suala hili katika njia mbili zilizotofauti sana. Katika dakika ya 2:30, meneja wa kituo cha yatima katika sehemu isiyotajwa nchini Haiti anaonyesha kuchanganyikiwa kwake kuhusiana na maslahi ya ghafla ya watoto wa Kihaiti, ambapo kabla hayakuangaliwa sana. Maombi kutoka kwenye familia za ughaibuni kuwaasili watoto yamekuwa ya kila siku. “Hata sijibu,” anasema. “Kila mmoja asikie, sitaki kupokea maombi ya baada ya janga.”

Mshirika mwenza aliyetambulika kama Ledice, hata hivyo, anayewalea watoto sitini katika vituo tofauti, anatoa wito wa kuwahamisha watoto haraka sana, na anaonyesha kutokuwepo kwa huduma za serikali kupitisha maombi ya kuwaasili watoto, hata yale yaliyokuwa yanatazamwa kabla ya janga. “Sasa ni shauri la kibinadamu,” anasema. “Tuwachukue watoto. Tutaona makaratasi baadae.”

Mingi ya mitazamo ya hivi karibuni kwa watoto, ile iliyo rasmi na ile isiyo, inatoka kwenye suala lililotangazwa sana la kikundi cha kanisa cha Kimarekani kukamatwa juma lililopita wakati wakijaribu kuwapeleka watoto thelathini kutoka Haiti kwenda Jamuhuri ya Dominika. Lakini mjadala mpana zaidi unaendela pia.

Conducive, blogu ya kikundi ambayo mara nyingi hujadili uasili wa kimataifa wa watoto, inaona kwamba uharaka wa kuasili watoto baada janga ulikwenda mrama:

Kuwahamisha watoto wakati wa majanga si jambo jipya. Tuliliona hilo katika operesheni Inuamtoto baada ya Vita ya Vietnam, ambapo serikali ya Marekani kwa haraka sana iliwaondoa watoto 3,000 kutoka nchini mwao wakati wa kuanguka kwa Saigon mwaka 1975. Kesi za kisheria kati ya wazazi wa kibaolojia na wazazi wa kuasili zilizikabili mahakama za Marekani kwa miaka mingi. Wazazi wa kibaolojia waliadai hawakuwahi kukubaliana na uasiliwaji wa watoto wao, na wazazi wa kuasili walidai kwamba uasiliwaji huo ulikuwa wa halali. Wanadharia wanaopinga uasiliwaji wa watoto wanaona mengi yanayofanana na uasiliwaji huu wa haraka haraka kwa watoto wa Haiti.

Katika posti yenye kichwa cha habari Yatima, Yatima, Yatima!, mwanablogu ResistRacism yu mahususi zaidi:

Wazazi watarajiwa wangapi wameshapata mafunzo kuhusiana na masuala ya kuasili watoto wa tamaduni na rangi tofauti? (Mzazi huyo huyo aliyezungumziwa hapo juu[kwenye posti] anajiuliza kuhusu namna ya kutunza nywele za mtu mweusi. Hivi sasa anapopokea mtoto. Unafikiri alitafakari masuala mengine kuhusu rangi na utamaduni?) (Wala usinifanye nianze kuhusu majeraha ya kisaikolojia. Hilo ni kubwa sana kulizungumzia. Lakini nina mawazo kuwa mtu wa kawaida hajaandaliwa kukabili athari kubwa za kisaikolojia kwa mtoto.)

Kwa nini mashirika hayo yasiwahamasishe wazazi watarajiwa wenye asili ya Haiti? Watu wenye uzoefu na namna ya kushughulikia majeraha ya kisaikolojia?

Posti hiyo hiyo inapendekeza utatuzi wa kibunifu zaidi.

Hapa kuna wazo fikirishi: Kama baadhi ya ‘yatima’ walitolewa kwa uasiliwaji kwa sababu wazazi wao hawawezi kuwatunza, vipi kuhusu kusafirisha familia nzima kutoka Haiti kwenda Marekani? Kama unazungumzia kwa kumaanisha kuhusu ustawi wa motto, je si vyema zaidi kwa familia nzima kuwa pamoja? Lakini hiyo haitafaa kwa matakwa ya familia hizo nyingine. Unajua, familia zile zinazotaka kuwasaidia yatima.

Mkazo mpya kwa mfumo ya Kihaiti wa Restavek imekuwa suala la mjadala. Katika posti iliyotoka kabla ya tetemeko, mwanablogu wa Repeating Islands anasema mfumo, “ambao kupitia kwa huo wazazi wanaoshindwa kuwatunza watoto wao huwapeleka kusihi na ndugu wenye ahueni au wageni ambako hupata chakula na, malazi na elimu kama malipo kwa kazi wanayofanya” umekuwa kama aina ya utumwa. Anamnukuu mchunguzi wa Umoja wa Mataifa ambae alitembelea Haiti mwakauliopita kuchunguza suala hilo la Restivek, akisema

…Ingawa kuwaweka watoto pamoja na wanafamilia nyingine ni mazoea ya siku nyingi nchini Haiti, siku hizi ‘waandikishaji wanaolipwa huzunguka nchi wakitafuta watoto kwa ajili ya kuwasafirisha ndani na nje ya nchi ya Haiti. Kitendohiki ni ukiukwaji mkubwa wa haki za msingi za mtoto.’

Mashirika mengi ya Kimataifa yanayojihusisha na kuwatunza watoto walio kwenye mazingira magumu, katika majuma mawili yaliyopita, yametoa tamko la kupinga uasiliwaji huu wa haraka nchini Haiti. Kamati ya Kimataifa ya shirika la Msalaba Mwekundu, katika tamko lililoweka kama mahojiano na mmoja wa maofisa wake wa matunzo ya mtoto, ilisema kwamba inaamini kwamba jitihada za kuwaunganisha watoto na familia zao nchini Haiti ni lazima zipewe kipaumbele, na kuasili watoto iwe ni hatua ya mwisho kabisa.

…Katika hali ambayo mtoto anahamishwa, zipo hatua za kufuata: mtoto lazim afuatane na ndugu yake au mtu anayemfahamu, ikiwezekana; taarifa za kina za mtoto lazima ziandikishwe na familia zao lazima zijue wapi mtoto amepelekwa na nani. Kwa bahati mbaya watoto wengine walichukuliwa kwa haraka bila taarifa zote za kina kuandikwa.

Makundi ya kutoa msaada pamoja na Save the Children, World Visison na Mfuko wa Shirika la Msalaba Mwekundu wa majanga (ambalo ni tofauti na Kamati ya Kimataifa), yalitoa tamko la pamoja kupinga kuchukuliwa kwa watoto pamoja na kuwaasili. UNICEF nayo ilifanya hivyo.

Kwa hiyo mkanganyiko ni upi? Suala la watoto kuzuiliwa mpakani likihusisha kukindi cha kuasili cha Kanisa la Protestanti, baadhi yao wakiwa wametumia uasili wa kimataifa kama namna ya kusambaza maoni yao ya kidini. Blogu nyingine za wakristo wa Kiinjili zimekuwa makini zaidi. Ukristo Leo, “Gazeti la Vuguvugu la Kiinjili” lilipinga uasili huo wa haraka wa kimataifa:

Katika hatua za miezi ya mwanzo baada ya tukio kama hili, hatutaki kuwasafirisha waotot mbali na maeneo yao ambako wanafamilia wao wanawatafuta. Baada ya tukio la tsunami la Asia ya kusini mashariki mwaka 2004, kulikuwa na watoto wengi wadogo wasiotambulika, na bado asilimia kubwa ya watoto hao, shukrani kwa vipimo vya Vinasaba (DNA) na njia nyingine, walirudishwa kwenye familia zao.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.